Kwa nini Serikali igawe pedi bure kwa wasichana

Muktasari:

Siku saba za kila mwezi hazijawahi kuwa rahisi na haki kwa msichana Najma (15) tangu alipobalehe mwaka 2020, anachokipitia kinabaki kuwa hadithi ambayo hatamani msichana yeyote akumbane nayo.

Dar es Salaam. Siku saba za kila mwezi hazijawahi kuwa rahisi na haki kwa msichana Najma (15) tangu alipobalehe mwaka 2020, anachokipitia kinabaki kuwa hadithi ambayo hatamani msichana yeyote akumbane nayo.

Najma ‘si jina halisi’ ambaye ni miongoni mwa wasichana wanaosoma Shule ya Sekondari Bundikani iliyopo Kibaha mkoani Pwani amesimulia adha anayoipitia anapokuwa hedhini, hali inayomlazimu wakati mwingine kukosa masomo.

“Nimezaliwa kwenye kaya maskini na wazazi wangu hawana uwezo wa kuninunulia sodo ‘pedi’ ili kujihifadhi ninapokuwa kwenye siku zangu. Ninamudu kupita kipindi hicho nikitumia vipande vya kanga chakavu ambazo hata hivyo sioni vikinisitiri,” anasimulia Najma.

Si hayo pekee. Yeye ni miongoni mwa wasichana wanaotegemea matundu machache ya vyoo shuleni hapo, lakini hukosa kujiamini kutokana na vifaa anavyotumia wakati wa hedhi kwa kushindwa namna ya kuvihifadhi ili akavifue kwa ajili ya matumizi mengine.

“Hakuna majisafi na sabuni pamoja na mafuta, hivyo naona aibu na nashindwa kujiamini,” anasema Najma.

“Ninapokuwa kwenye siku zangu husubiri wote watoke darasani ninakuwa wa mwisho na wakati mwingine nashindwa kusimama kujibu swali mwalimu akiuliza, ninahofu huenda nimechafua sketi yangu ya shule.”

Kauli ya Najma inasimama mbadala wa maelfu ya wasichana wanaosoma shule za msingi na sekondari ambao hawajui wapi pa kuipata pedi ambayo itawahifadhi na watabaki kuwa huru pasi na shaka wala wasiwasi wakiendelea na masomo wala matundu ya kutosha ya vyoo shuleni.

Kwa mujibu wa takwimu msingi zinazotolewa na ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Tamisemi (BEST) za mwaka 2020, wasichana katika halmashauri 181 nchini wanatumia tundu moja katika kila shule kuliko kiwango kilichowekwa na Serikali

Baadhi ya wasichana waliozungumza na Mwananchi wamesema wanavaa pedi zaidi ya saa 6 kwa kipindi chote wanachokuwa shuleni, hali ambayo ni hatari kwa afya zao na wanapokosa wamekuwa wakitumia mbinu mbalimbali mbadala.

Wakati taulo za kike zinapokuwa ghali, bidhaa yenye gharama nafuu ambayo huikimbilia ni karatasi za chooni ‘toilet paper’, mazingira duni na umasikini ni sababu ya kutumiwa kwa njia hizi.

Mwanafunzi wa kidato cha pili shule ya sekondari ya wasichana Jangwani anasema baadhi ya wanafunzi shuleni hapo wamekuwa wakitumia mbinu mbadala ikiwa hawana vifaa vya kujihifadhi.

Anasema mazingira duni na umaskini ni sababu, kwa kuwa baada ya karatasi hizo soksi ni ya pili kutumika.

“Soksi hutumika pia kama mbadala wa pedi, vitambaa pia ambavyo hufyonza damu ya hedhi na vinaweza kutumika tena baada ya kufua, nguo kuukuu huwa tunachana na kuifua vizuri, lakini kuna nyakati vyooni tuliwahi kushuhudia mtu ametupa kipande cha gazeti kwenye dustbin kikiwa kimetumika kama mbadala wa pedi,” anasema msichana huyo wa miaka 16.

Utafiti uliowahi kufanyika na Shirika la Plan International mwaka 2018 ulibaini asilimia 40 ya wanawake walio chini ya miaka 21 hutumia ‘tissue’ wakati wa hedhi.

Hata hivyo, wataalamu wa afya wanasema kuna madhara kwa wanawake kutumia vitu visivyo safi wakati wa hedhi.

Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na uzazi kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, Living Colman anasema kutumia kitu chochote kisicho safi kukinga hedhi huleta madhara, ikiwemo magonjwa na fangasi ukeni.

“Hedhi inapotoka inakuwa ni kama uchafu, ikikaa muda mrefu inatengeneza bakteria na ndiyo maana huona inatoa harufu, hivyo ni rahisi kupata maambukizi katika njia ya mkojo (UTI) au kwenye uke baadaye yakapanda mpaka kwenye kizazi, mirija, akapata maambukizi ya bakteria ya shingo ya kizazi (PID),” anasema Dk Colman.


Ripoti

Wakati wasichana wakiwa hawana uhakika wa kujihifadhi, bado wanakumbana na changamoto ya matundu machache ya vyoo.

Ripoti ya tathmini ya maji shuleni na usafi wa mazingira ya mwaka 2018 iliyotolewa na Ofisi ya Rais Tamisemi inaonyesha ufikiwaji mdogo wa huduma za maji na usafi shuleni ambalo limekuwa tatizo la kudumu kwa miongo kadhaa na inachangia ujifunzaji duni.

Ripoti inaonyesha kuna vyoo vya aina tatu, vinavyoweza kuoshwa vyenye sinki maalumu asilimia 41.8, vyoo vya shimo asilimia 19.7 na vile vya shimo vilivyoboreshwa asilimia 14.0, huku zaidi ya asilimia 1 ya shule hazikuwa na vyoo.

Hata hivyo ripoti inaonyesha asilimia 94 ya shule zote za wasichana zilikuwa na huduma za msingi za usafi wa mazingira ikilinganishwa na asilimia 65.2 shule za wavulana na asilimia 28.7 ya shule za pamoja.

Takwimu zinaonyesha kuwepo kwa upungufu katika halmashauri nyingi na ili kumaliza upungufu huo, matundu ya vyoo 303,932 yanahitaji kujengwa nchini katika shule za msingi ili kufikia viwango vilivyowekwa na Serikali kwa tundu moja la choo kutumiwa na wanafunzi 25 kwa wavulana na 20 wasichana.

Kati ya matundu ya vyoo yanayohitaji kuongezwa 125,445 ni kwa ajili ya wavulana na 178,487 kwa ajili ya wasichana.


Hali halisi nchini

Miongoni mwa visa vya wasichana hawa wale waishio pembezoni wapo ambao hujihifadhi katika mazizi ya ng’ombe, hasa maeneo ya wafugaji mpaka siku zao zikome na wapo ambao hukatisha masomo kwa kuwa hata vitambaa vya nguo chakavu vimekosekana.

Utafiti wa shirika lisilo la kiserikali la Usawa wa Wanawake na Wasichana (Foepa) umeonyesha Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro wasichana hasa wa wajamii ya wafugaji wamekuwa wakiacha masomo na wengine kukosa vipindi kwa siku kadhaa wanapopata hedhi.

Utafiti uliofanywa na Shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa (Unicef), ulionyesha wasichana hukosa masomo siku nne hadi tano kwa mwezi kutokana na hedhi.

Pia, msichana mmoja kati ya kumi huacha shule kila mwaka kutokana na kukosa vifaa vya kujihifadhi wakati wa hedhi.

Baadhi ya maeneo yaliyotajwa kuwa na changamoto hiyo ni Nchinga Lindi vijijini, Ntuntu Singida, Izimbia Bukoba, Ngarenaro na Serioni mkoani Kilimanjaro, huku maji na sabuni vikitajwa kuwa changamoto, licha ya kuwa msaada kwa wasichana hao.

Mtafiti katika Taasisi ya Taifa ya Magonjwa ya Binadamu (Nimr), Angela Shija anasema utafiti umeonyesha kuwa asilimia 80 ya wanafunzi waliopo mijini wanatumia pedi mchana wakiwa shuleni na usiku wanatumia vitambaa kutokana na sababu za kiuchumi.

“Vijijini huko walionekana wanaoweza kupata huduma ya pedi ni asilimia 40 pekee, nao changamoto ni ileile kama mijini,” anasema Angela na kuongeza kuwa shule nyingi zimekuwa hazina miundombinu ya maji na choo.


Wadau waishauri Serikali

Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji katika taasisi ya Msichana Initiative, Rebecca Gyumi anasema Serikali inaweza kuchukua mikakati miwili kwenye kurahisisha upatikanaji wa bidhaa ya pedi kwa kundi la wasichana ili kuwaondolea changamoto ambazo wavulana hawakutani nazo.

“Kugawa pedi bure kwa wanafunzi, maana kwa sasa wasichana hukosa siku nne mpaka tano kwa sababu ya hedhi, ikiwamo upatikanaji na mmoja kati ya 10 huacha shule kabisa. Kwa hiyo kutoa vifaa bure ni kuongeza wigo wa wasichana kubaki shule na kusoma na kukabiliana na changamoto za mdondoko wa watoto wa kike kwenye elimu,” anapendekeza Gyumi.


Nini kifanyike

Ongezeko la gharama kwa bidhaa ya pedi imekuwa ikipaa kwa kasi kutoka Sh1,500 mwaka 2017 mpaka kufikia Sh2,000 - 3,000 mwaka 2022.

Kupaa kwa bei hiyo kunawafanya wasichana kutumia Sh6,000 hadi Sh9,000 kila mwezi ili kujihifadhi katika siku nne mpaka saba za hedhi, ikiwa zitatumika kama inavyoshauriwa kitaalamu.

Mwananchi iliangazia takwimu za Best za mwaka huu, zinazoonyesha wasichana walio zaidi ya umri wa miaka 13 ambao wanakadiriwa kuwa wamebalehe au kuelekea hatua hiyo ya ukuaji waliopo katika shule za msingi ni 413,955 na waliopo shule ya sekondari ni zaidi ya milioni 1.47.

Ikiwa Serikali itagawa pakiti ya pedi yenye thamani ya Sh2,000 kwa kila msichana aliyepo shuleni itatumia Sh827.91 milioni kwa mwezi; kwa mwaka itatumia Sh8.28 bilioni. Kwa upande wa shule za sekondari itatumia Sh29.53 milioni ambayo ni sawa na Sh29.53 bilioni kwa mwaka.

Takwimu hizo zinaashiria kuwa iwapo Serikali itafanya maamuzi ya kugawa pakiti moja ya pedi kwa kila msichana kwa kipindi cha miezi 10 ya mwaka anayokuwepo shuleni itatumia Sh3.781 bilioni kwa mwezi, ambayo ni sawa na Sh37.806 bilioni kwa mwaka, kiwango ambacho Wizara ya Elimu na Sayansi inaweza kutenga kwenye bajeti ya mwaka wa fedha.


Wafanyabiashara

Mwaka 2018 Serikali ilipiga hatua kubwa yenye mwelekeo sahihi wa kupunguza gharama anazoingia msichana na mwanamke kwenye kununua bidhaa za kujihifadhi wakati wa hedhi kwa kutoa kodi kwenye bidhaa ya pedi.

Lakini mwaka 2019 ukiwa umepita mwaka mmoja tangu kutolewa kwa kodi, Serikali iliirudisha tena kutokana na kudai kuwa wafanyabiashara hawajapunguza bei kama ilivyokusudiwa.

Hata hivyo, wafanyabiashara hao wanasema imefika wakati Serikali iangalie namna ya kupunguza utitiri wa kodi kwenye bidhaa hiyo.

Mkurugenzi wa Kasole Secrets, wazalishaji wa pedi za Glory, Hyasintha Ntuyeko anataja changamoto wanazopitia wasambazaji wa pedi nchini.

Anasema changamoto ya kwanza ni bidhaa za pedi kuhesabiwa kama kifaa tiba, hali inayowalazimu kulipia leseni ya biashara kila mwaka ambayo ni Sh300,000 ili kukidhi vigezo, ikiwa ni pamoja na kumlipa mfamasia.

“Bado hatujaomba kibali cha kuruhusiwa kuingiza pedi hizi nchini; tunalipia asilimia 10 kulingana na thamani ya mzigo tuliouingiza, hizi zote ni gharama ambazo pia zinachangia kuongeza gharama ya pedi hizi sokoni,” anasema. Utitiri wa kodi unawafanya wafanyabiashara kuuza bidhaa hiyo kwa bei ya juu.

Wafanyabiashara hao wanasema wanalazimika kulipia ushuru mwingi kwa taasisi za Serikali, lakini bado wanalipia manispaa wanakolazimishwa kulipia leseni ya biashara pia.

“Bidhaa moja ina leseni mbili za biashara, tunashindwa kuelewa kuna mikakati gani hasa ambayo imewekwa ili kumpunguzia msambazaji na mzalishaji gharama na tukiweka kodi ya ongezeko la thamani hapo ambayo ni asilimia 18 ya gharama ya mzigo, bei inazidi kupanda zaidi, hivyo inakuwa vigumu kuuzwa kwa bei nafuu,” anasema Hyasinta.


Mikakati ya Serikali

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima anasema katika maadhimisho ya kilele cha Siku ya Mtoto wa Kike zitakazofanyika katika Halmashauri ya mji wa Babati Oktoba 12 (mwakani), suala hilo ni miongoni mwa mambo yatakayozungumziwa.

Hata hivyo, anasema wizara itaratibu ajenda ya bei elekezi ya vifaa vya hedhi bila kuathiri ubora.

“Hili ni muhimu, hasa tukizingatia kwamba kwenye utafiti wa NIMR imebainika kuwa asilimia 60 ya wasichana walionekana kutomudu gharama za taulo za kike,” anasema Dk Gwajima.