Watahiniwa 1,330 wa Uuguzi, Ukunga wafutiwa matokeo
Muktasari:
- Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania liliendesha mitihani ya usajili na leseni kwa wauguzi na wakunga 1,434 wa ngazi zote. Watahiniwa wa Astashahada walikuwa 44, Stashahada 1,330 na Shahada 60.
Dar es Salaam. Wizara ya Afya imetangaza kufuta matokeo ya watahiniwa 1,330 wa Stashahada ya Uuguzi na Ukunga baada ya kujiridhisha kulikuwa na uvujaji wa mitihani.
Matokeo yote ya mtihani wa usajili na leseni wa wauguzi na wakunga kwa watahiniwa hao, yamefutwa kwa mujibu wa Sheria ya Uuguzi na Ukunga ya Mwaka 2010, kanuni ya mafunzo ya mwaka 2010, kifungu cha 22 (3).
Hii si mara ya kwanza kufutwa kwa mitihani hiyo, kwani Novemba 5, 2021, Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (Nacte) iliyafuta matokeo yote ya mitihani ya nadharia ya programu ya utabibu ngazi ya Stashahada (NTA level 5), kwa vyuo vyote nchini baada ya kuthibitika mitihani hiyo kuvuja.
Taarifa iliyotolewa leo Jumanne, Januari 16, 2024 na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Afya, Englibert Kayombo imeeleza Septemba, 2023, baraza liliendesha mitihani ya usajili na leseni kwa wauguzi na wakunga 1,434 wa ngazi zote.
“Wizara ya Afya ilipata taarifa za kuvuja kwa mtihani na kuchukua hatua za haraka kushirikiana na vyombo vya usalama kufanya uchunguzi na ilithibitika ni ukweli mtihani ulivuja na kusambaa kwa watahiniwa wa Stashahada,” amesema.
Kayombo amesema mtuhumiwa aliyehusika katika uvujishaji wa mtihani huo tayari amebainika na kusimamishwa kazi, huku taratibu za kinidhamu na kisheria zikiendelea kutekelezwa.
“Wizara inautangazia umma kuwa matokeo yote ya mtihani wa usajili na leseni wa wauguzi na wakunga kwa watahiniwa wa stashahada 1,330 yamefutwa kwa mujibu wa sheria,” amesema.
Kayombo amesisitiza hatua hizo zimechukuliwa kwa lengo la kuhakikisha baraza linathibitisha wataalamu wenye sifa stahiki kulingana na taaluma zao ambao watatoa huduma bora za matibabu kwa wagonjwa pamoja na kuzingatia usalama wa mteja anayetegemea kupata huduma za uuguzi na ukunga.
Amesema hiyo ni kwa mujibu wa sheria ya uuguzi na ukunga ya mwaka 2010, ambalo ndilo jukumu kubwa la baraza.
Hata hivyo, Kayombo amesema watahiniwa watapewa nafasi ya kufanya mtihani mwingine bila malipo Februari 16, 2024 jijini Dodoma na hawatahitajika kujisajili tena.
“Kuhusu taratibu za kurudiwa kwa mtihani huu zitatolewa na baraza, watahiniwa wote wanatakiwa kujiandaa na mtihani huo kwa kufuata taratibu kanuni na sheria,” amesema.
Ameeleza kwa upande wa watahiniwa wa ngazi za astashahada na shahada, matokeo yameshatoka na watahiniwa wamepata matokeo yao.
Watahiniwa wa astashahada walikuwa 44, stashahada 1,330 na shahada 60. Mitihani hiyo ilifanyika katika vituo vitatu katika mikoa ya Dar es Salaaam (DUCE), Mwanza (Mwanza University) pamoja na Dodoma (St. John University).