Watanzania sasa wazigeukia diet na gym

Muktasari:
Lakini katika siku za hivi karibuni, wengi wamegeukia kupunguza unene na kutaka zaidi kuwa na maumbo ya wastani na baadhi kujikondesha kabisa.
Kwa mila za kiafrika, inaamika kuwa unene ni ishara ya afya njema au kuwa na fedha nyingi.
Lakini katika siku za hivi karibuni, wengi wamegeukia kupunguza unene na kutaka zaidi kuwa na maumbo ya wastani na baadhi kujikondesha kabisa.
Kasi ya watu kuacha kula, kula mbogamboga, kufanya mazoezi katika maeneo maalum (gym) kukimbia au kutembea kwa miguu ili kupunguza uzito imekuwa ni mtindo wa maisha kwa sasa.
Si ajabu sasa kukutana na mtu mwenye gari akalicha usafiri huo na kutembea kwa miguu kwa ajili ya kuweka sawa mwili wake.
Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha kuwa mwaka 2014 asilimia 39 ya watu wazima wote duniani walikuwa na uzito kupita kiasi. Kati ya hao wanaume ni asilimia 38 na wanawake asilimia 40.
Hali hiyo imeisukuma WHO kusisitiza wadau wa mataifa mbalimbali ambao ni wanachama wa Umoja wa Mataifa kuweka mkazo kwenye uhamasishaji wa kuzingatia mpangilio mzuri wa chakula na mazoezi.
Licha ya kuwa uzito mkubwa sio mzuri kiafya sababu kubwa inayotajwa kuwasukuma wengi kwa sasa kupungua ni kuwa na mwonekano mzuri.
Hivi sasa katika mitandao ya kijamii na matangazo kadhaa ya redio na televisheni, wengi wamekuwa wakizitangaza dawa za asili na za hospitali za kupunguza unene.
Kadhalika, watu maarufu hapa nchini wakiwamo wasanii, viongozi wa Serikali wameonyesha kasi ya kufanya mazoezi au kuonyesha namna wanavyoabudu mpangilio mzuri wa chakula ili kupunguza uzito.
Kwa mfano, mazoezi ya kukimbia (jogging) hivi sasa yanafanywa kila Jumamosi na Jumapili katika maeneo mbalimbali. Mazoezi hayo yanajumuisha vikundi vya vijana wenye sare za michezo.
Kadhalika, kupunguza uzito kumekuwa ni jitihada iliyoshika kasi katika mitandao kwa wanaotumia dawa au kupangilia mlo kuweka picha zao zinazoonyesha kabla na baada ya kupungua .
Hata barabarani kumekuwa na matangazo lukuki ya biashara yakizinadi dawa za kupunguza unene kupita kiasi.
Wanasaikolojia wameileza hali hii kuwa inasababishwa na kushamiri kwa mitandao ya kijamii inayowafanya watu kuhamasishana.
Mtaalam wa saikolojia Modesta Kimonga alisema wakati mwingine hali hiyo inasababishwa na tabia ya kuiga mwingine anachofanya.
“Kuna watu wameumbwa kupata hamasa kutoka kwa watu wengine, yaani unaweza kukuta hana nia lakini anafanya jambo kwa sababu mwingine amefanya ndiyo iko hivyo hata kwenye suala la kupungua uzito,” alisema
Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi umebaini kuwa mitandao ya kijamii imekuwa ikitumika kwa kiasi kikubwa kuhamasisha kupungua uzito.
Mkazi wa Tabata, Ledia Mwangosi alisema watu wengi wamepata elimu kwamba uzito mkubwa sio mzuri kiafya ndiyo sababu kasi ya kukabiliana na hali hiyo imekuwa kubwa.
“Kwa ninavyofahamu uzito mkubwa ni tatizo kiafya. Mwenyewe utaanza kujiona tofauti na huwezi kuwa mwepesi kama walivyo watu wembamba. Nahisi hilo limechangia kwa kiasi kikubwa kwa sasa watu wengi kutaka kupungua,”
“Nilichojifunza ni kwamba mtu mwenye uzito wa wastani huwezi kusumbuliwa na maradhi ya moyo, shinikizo la damu na hata maumivu ya mwili yasiyo na sababu. Kuwa na uhakika wa hali hiyo lazima mwili uwe unapata mazoezi na mpangilio mzuri wa vyakula,”
Kwa upande wake, Zainab Kahaya anataja umaridadi kama sababu kubwa inayowafanya wengi watamani kupunguza unene miaka hii.
Alisema hiyo inatokana na dhana kwamba ukiwa na mwili wa wastani unakuwa na mwonekano mzuri na mavazi yoyote yanakupendeza.
“Ukiwa na mnene kupita kiasi ni nadra sana kupendeza na kuna baadhi ya mitindo unaweza usipate saizi yako. Hii inawafanya wanaotaka kuwa na mwonekano mzuri, kufanya kadiri wanavyoweza ili wasinenepe,” alisema Kahaya
Wafanyabiashara nao wameona hiyo ni fursa, kila kukicha wamekuwa wakitoka na njia mbalimbali za kupunguza uzito zikihusisha dawa na virutubisho.
Wengine wameweka mkazo kwenye mpangilio wa chakula, kuzingatia kiwango na muda sahihi wa kula (diet).
Kundi kubwa lililoibuka sasa ni wale wanaouza dawa na virutubisho mbalimbali ambavyo wanadai vina uwezo wa kupunguza uzito kwa muda mfupi.
Moja ya bidhaa zinazotangazwa sana ni majani ya chai. Haya yapo ya aina mbalimbali kulingana na matakwa ya mtumiaji.
Majani haya yanadaiwa kuwa na uwezo wa kupunguza uzito na kumfanya mtu anayetumia kuwa na mwonekano wa kuvutia.
Pita pita yangu mitandaoni inanipeleka kwenye ukurasa mmoja unaomilikiwa na mfanyabiashara wa majani hayo.
Ukurasa huo una tangazo linalosomeka “Kupunguza tumbo na nyama pembeni ya tumbo, kutoa mafuta yaliyoganda tumboni, kufanya mmeng’enyo wa chakula kwa haraka na kulainisha choo”.
Tangazo hilo halikuishia hapo linaeleza kuwa dozi ya wiki mbili inapunguza kilo tatu hadi tano ndani ya wiki ya kwanza na siku zinazosalia unene wote unakwisha.
Baada ya kumhoji mfanyabiashara huyo (ambayealiomba jina lake lihifadhiwe) ili kujua namna majani hayo yanavyofanya kazi alijibu kwa kifupi kuwa mtumiaji atatoa mafuta yaliyopo mwilini kupitia haja kubwa.
“Kama unahitaji njoo uchukue utapata na maelekezo ila kwa kifupi ukishayatumia utaona unapata choo laini, hapo mafuta yatakuwa yanatoka na matokeo utayaona ndani ya siku tano,” alisema mfanyabiashara huyo .