Watanzania wahimizwa kuanza maandalizi ya kustaafu mapema
Mtendaji Mkuu wa CORE Securities Limited, wasimamizi wa Mfuko mpya wa Uwekezaji wa Kustaafu wa FPRF, George Fumbuka (kulia) akifafanua jambo mbele ya waandishi wa habari, jijini Dar es Saaam. Kushoto ni Meneja wa Mfuko wa FPRF, Richard Matekele.
Muktasari:
- FPRF yaanza kampeni ya Taifa kuhamasisha uwekezaji wa kustaafu.
Dar es Salaam. Mfuko wa uwekezaji wa kustaafu wa Foresight Private Retirement Fund (FPRF) umezindua kampeni ya kitaifa ya elimu ya fedha inayolenga kuwahamasisha Watanzania kuanza kuwekeza mapema kwa ajili ya maisha ya baada ya kustaafu.
Kampeni hiyo itatekelezwa kupitia warsha, semina na mikutano ya wadau mbalimbali nchini ikiwa na lengo la kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa uwekezaji wa muda mrefu na namna ya kujenga uhuru wa kifedha baada ya kuacha kufanya kazi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Jumanne, Julai 14, 2026, Ofisa Mtendaji Mkuu wa CORE Securities Limited, wasimamizi wa FPRF, George Fumbuka amesema mfuko huo unalenga kujenga utamaduni mpya wa kifedha kwa kuwahimiza wananchi kuanza kujiandaa kwa ustaafu mapema badala ya kusubiri wanapokaribia kuacha kazi.
Amesema kwa muda mrefu mifumo ya pensheni imewanufaisha zaidi walio katika ajira rasmi, huku wananchi wengi wanaojishughulisha na shughuli za sekta isiyo rasmi wakikosa fursa za kujenga akiba na uwekezaji wa muda mrefu.
"Tunataka kuanzisha utamaduni mpya wa kifedha nchini. Kwa muda mrefu watu wamekuwa wakifikiria kustaafu pale wanapokaribia kuacha kazi. Sisi tunasema maandalizi ya maisha ya baada ya kustaafu yanapaswa kuanza mapema.
“Swali si kama utastaafu, bali utaishije baada ya kustaafu. Ndiyo maana tunawahamasisha Watanzania waanze kuwekeza leo ili waishi kwa uhuru kesho," amesema Fumbuka.
Amesema FPRF imeundwa kuwahudumia makundi mbalimbali yakiwemo wafanyakazi wa sekta ya umma na binafsi, wafanyabiashara, wakulima, wavuvi, wajasiriamali, vikundi vya kijamii, Saccos, kampuni na taasisi.
Kwa mujibu wa Fumbuka, mafanikio ya mfuko huo hayatapimwa kwa idadi ya wanachama pekee, bali pia kwa kiwango cha uelewa kitakachojengwa kuhusu umuhimu wa kupanga maisha ya kifedha ya baadaye.
Amesisitiza FPRF haikusudiwi kuchukua nafasi ya mifuko ya hifadhi ya jamii iliyopo, bali kuongeza fursa za uwekezaji wa hiari zitakazowawezesha wananchi kujenga utajiri wa muda mrefu.
Tofauti na mifuko ya hifadhi ya jamii inayotegemea michango ya lazima, FPRF inatoa nafasi kwa mwananchi kuchagua kiwango cha uwekezaji kulingana na uwezo wake na namna ya kupokea mafao baada ya kutimiza masharti ya mfuko.
"Mwekezaji anaweza kuchagua kulipwa mafao kwa mkupuo, kwa malipo ya kila mwezi kama pensheni au kwa mchanganyiko wa njia hizo kulingana na mahitaji yake," amesema.
Kwa upande wake, Meneja wa FPRF, Richard Matekele amesema mfuko huo una mipango mitatu ya uwekezaji inayolenga makundi tofauti ya umri, ambayo ni Youngsters' Plan kwa walio chini ya miaka 35, Middle-Agers' Plan kwa wenye umri wa miaka 35 hadi 50 na Seniors' Plan kwa wenye zaidi ya miaka 50.
Mipango hiyo imeandaliwa ili kukidhi mahitaji tofauti ya wawekezaji kulingana na hatua zao za maisha na malengo ya kifedha.
Matekele amesema wanachama wanaweza kuchangia kwa mkupuo au kwa michango ya kila mwezi, huku fedha zao zikiwekezwa katika hisa, hati fungani, dhamana za Serikali na vyombo vingine vya masoko ya mitaji kwa lengo la kuongeza thamani ya uwekezaji kwa muda mrefu.
Amesema kampeni ya elimu ya fedha itawafikia waajiri, wafanyakazi, taasisi za elimu, vyama vya wafanyakazi, Saccos, vikundi vya kijamii, wafanyabiashara, wanawake, vijana na wakulima ili kuongeza uelewa wa umuhimu wa kuwekeza mapema kwa ajili ya maisha ya baada ya kustaafu.
FPRF ni mfuko wa uwekezaji wa kustaafu ulioidhinishwa na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), unasimamiwa na CORE Securities Limited, huku NMB Bank Plc ikihudumu kama Mdhamini na Mlezi wa mali za mfuko.