Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mfuko mpya wa pensheni wafungua milango kwa sekta isiyo rasmi

Ofisa Mtendaji Mkuu wa CORE Securities Limited, George Fumbuka (kushoto), akimkabidhi Mjumbe wa Kamati ya Utendaji Taifa ya Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Nelson Mabula (kulia), nyaraka za Mfuko wa Uwekezaji wa Kustaafu wa Foresight Private Retirement Fund (FPRF) kama ishara ya uzinduzi rasmi wa mfuko huo jijini Dar es Salaam. Katikati ni Mtaalamu Mbobevu wa Masoko ya Mitaji na Dhamana, Dk Ibrahimu Mwangalaba.

Muktasari:

  • Mfuko wa FPRF ulioidhinishwa na CMSA umeanza rasmi kutoa fursa kwa Watanzania wa sekta rasmi na isiyo rasmi kuwekeza kwa ajili ya maisha ya baada ya kustaafu kwa kuanzia Sh10,000, huku ukiwa na mfumo unaoruhusu mwanachama kupata mafao yake baada ya miaka mitano.

Dar es Salaam. Mamilioni ya Watanzania wanaojishughulisha na biashara ndogondogo, kilimo, bodaboda na kazi nyingine za sekta isiyo rasmi sasa wanatarajiwa kupata fursa mpya ya kujiwekea akiba ya uzeeni baada ya kuzinduliwa kwa Foresight Private Retirement Fund (FPRF), mfuko unaolenga kupanua wigo wa hifadhi ya jamii nchini.

Mfuko huo ulioidhinishwa na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) unalenga kuwafikia wananchi ambao kwa muda mrefu wamekuwa nje ya mifumo rasmi ya pensheni, ukitoa nafasi ya kuwekeza kuanzia kiasi cha Sh10,000 pekee.

Akizungumza leo Jumanne Juni 16, 2026 wakati wa uzinduzi uliofanyika Dar es Salaam, mtaalamu wa masoko ya mitaji, Dk Ibrahimu Mwangalaba, amesema mfuko huo ni hatua muhimu katika kuimarisha ujumuishaji wa kifedha nchini, akibainisha kuwa wananchi wengi wa sekta isiyo rasmi wamekuwa wakikosa fursa ya maandalizi ya maisha ya baada ya kustaafu.

Amesema FPRF inaleta jukwaa jumuishi linalomwezesha kila Mtanzania, bila kujali aina ya ajira, kuwekeza kwa uhuru na kupanga maisha ya baadaye kwa heshima, akisisitiza kuwa utamaduni wa kuweka akiba ya muda mrefu unapaswa kuimarishwa.

Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa CORE Securities Limited, George Fumbuka, amesema mfuko huo umeundwa kukamilisha mifumo iliyopo ya hifadhi ya jamii kwa kutoa chaguo zaidi za uwekezaji, hususan kwa wananchi ambao hawajafikiwa na mifuko ya kawaida ya pensheni.

Amebainisha kuwa mfuko huo umeidhinishwa kukusanya hadi shilingi bilioni 10 kupitia vipande milioni 100 vya uwekezaji, huku ukitoa mipango mitatu ya uwekezaji kulingana na umri wa wawekezaji, hatua inayolenga kuendana na mahitaji tofauti ya kifedha.

Fumbuka ameongeza kuwa tofauti na mifumo mingi ya pensheni, mfuko huo unaruhusu mwekezaji kupata fedha zake baada ya miaka mitano, aidha kwa mkupuo, malipo ya kila mwezi au mchanganyiko wa njia hizo, hatua inayotoa unyumbufu zaidi kwa wanachama.

Uwekezaji katika mfuko huo utafanyika kupitia mifumo ya kidijitali ya CORE Securities, matawi ya NMB Bank Plc pamoja na mawakala walioidhinishwa wanaounganishwa na Dar es Salaam Stock Exchange (DSE), huku wadau wakisema hatua hiyo inaweza kuongeza ushiriki wa wananchi katika masoko ya mitaji na kuimarisha ustawi wa kifedha wa muda mrefu.