NSSF kukamilisha ujenzi wa hoteli ya nyota tano, faida zake zatajwa
Wajumbe Kamati ya Kudumu ya Ustawi na Maendeleo ya jamii wakiwa ghorofa ya 33 ya mradi wa Mzizima Tower kuangalia ujenzi wa hoteli inayojengwa ndani ya jengo hilo.
Muktasari:
- Mradi huo wa uwekezaji unaojengwa kwa asilimia 100 na NSSF unahusisha ujenzi wa minara miwili, ikiwemo mnara wa biashara wenye ghorofa 35 na mnara wa makazi wenye ghorofa 32, ukiwa na jumla ya eneo la ujenzi la mita za mraba 95,018.15.
Dar es Salaam. Hatimaye hoteli ya nyota tano itakayokuwa na vyumba 156 vya kulala wageni na vyumba 132 vya makazi ya muda mfupi (hotel apartments), inayojengwa na Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF), inatarajiwa kukamilika na kuanza kazi rasmi Desemba 2026.
Hayo yamebainishwa Machi 16, 2026 na Waziri wa Kazi, Ajira na Uhusiano wa Kazi, Deus Sangu alipokuwa akitoa taarifa kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii ilipofanya ziara katika mradi wa Mzizima Tower uliopo katikati ya Jiji la Dar es Salaam.
Sangu amesema mradi huo wa uwekezaji unaojengwa kwa asilimia 100 na NSSF unahusisha ujenzi wa minara miwili, ikiwemo mnara wa biashara wenye ghorofa 35 na mnara wa makazi wenye ghorofa 32, ukiwa na jumla ya eneo la ujenzi la mita za mraba 95,018.15.
Kwa upande wa hoteli, amesema itakapokamilika itaendeshwa kwa ubia kati ya NSSF na wamiliki wa hoteli za Radisson Blu, ambao wana hoteli za aina hiyo katika nchi mbalimbali duniani.
“Mradi huu, mbali na hoteli, utakuwa na makazi ya muda, ofisi, kumbi za mikutano na maeneo ya biashara. Ujenzi wake ulianza Aprili 2013 na ulitarajiwa kukamilika Machi 2017,” amesema Sangu.
Akieleza sababu ya kuchelewa kumalizika, Sangu amesema kumechangiwa na sababu mbalimbali, ikiwemo Serikali kusimamisha ujenzi wake mwaka 2016 kupisha ukaguzi wa SSRA, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ukifuatiwa na ukaguzi maalumu wa PPRA uliofanywa mwaka 2019.
Sababu nyingine ni ujenzi wa hoteli kuanza bila uteuzi wa mwendesha hoteli, jambo ambalo ni moja ya masharti ya uendeshaji wa hoteli za nyota tano. Hata baada ya kupatikana mwendesha hoteli, kulikuwa na mabadiliko aliyotaka yafanyike katika ujenzi wa hoteli hiyo na kulazimika kurekebisha baadhi ya maeneo.
“Niseme baada ya Serikali kuruhusu ujenzi kuendelea tangu mwaka 2022, hivi sasa umefikia asilimia 91 na Desemba 2026 utakuwa umekamilika na hoteli hiyo kuanza kazi rasmi kwani umebaki kumalizia mambo madogo madogo, ikiwemo mifumo ya maji na umeme,” amesema Sangu.
Akieleza chimbuko la kuanzisha mradi huo, Sangu amesema ni kutokana na tathmini iliyobaini eneo zima lina nafasi ya uwekezaji wa majengo ya kibiashara na makazi.
Pia, amesema ni kutokana na ukuaji wa shughuli za kiuchumi na ongezeko la mahitaji ya ofisi, huduma za malazi na makazi jijini Dar es Salaam.
“Pia, miundombinu bora ya barabara, huduma za kijamii na kuwepo karibu na taasisi nyingi za kibiashara na kumbi za mikutano zimesababisha kuongezeka kwa thamani ya uwekezaji wa eneo hilo,” amesema Waziri huyo.
Hata hivyo, amesema mradi huo wote umegharimu zaidi ya Sh326 bilioni na fedha za uwekezaji wake zinatarajiwa kurudi ndani ya miaka 14 au chini ya hapo.
Mbali na hilo, pia amesema umeweza kutoa ajira zaidi ya 300 wakati wa ujenzi wake na utakapokamilika unatarajiwa kutoa zaidi ya ajira 250.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Hawa Mchafu, amepongeza mradi huo na kueleza kuwa wajumbe wake wakipewa nafasi ya kuuelezea bungeni kwa dakika 10 wanazopewa huenda zisiwatoshe.
Hawa amesema kukamilika kwake wanaamini kutapunguza kasi ya watu kila inapofika Desemba kwenda kupumzika nchini Dubai, na sasa si Watanzania tu wataahirisha hilo, bali hata wageni kutoka nje ya nchi watakwenda hapo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Hawa Mchafu akizungumza mara baada ya kuhitimisha ziara ya kutembelea mradi wa Mzizima Tower kuangalia maendelwo ya ujenzi wake.
Pia, mwenyekiti huyo amesema jambo jingine lililowafurahisha ni kusikia kuwa fedha za uwekezaji wa mradi huo wa Mzizima Tower zinaweza kurudi hata kabla ya miaka 14 iliyowekwa.
“Haya matarajio mliyoweka ya kurudisha fedha za uwekezaji kabla ya miaka 14 ni jambo la heri, kwa kuwa miradi inayochelewa kurudisha fedha huwa ikituumiza sisi wawakilishi wa wananchi, ukizingatia hizi fedha ni za wanachama wanaotarajia wakistaafu wapewe fedha zao,” amesema.
Wakichangia maoni kwa nyakati tofauti, mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo, Kangi Lugola, amesema alitilia shaka marekebisho ya mwendesha hoteli ukizingatia tayari washauri wa ujenzi walishaweka muundo wa jengo.
“Vipi huyu akishindwa kuendesha akaja mwingine akataka ibomolewe na kuweka mtindo mwingine? Ina maana jengo hili litachanwa tena?
“Naomba tujifunze kwa hoteli nyingine za nyota tano ambapo wamepita wawekezaji wengi. Hivyo sisi tunachofanya ni kuweka tu angalizo katika hilo,” amesema Lugola.
Katika hilo, Waziri Sangu amemuondoa shaka Lugola akisema katika kuingia mkataba na mwekezaji huyo wamezingatia mambo hayo yote.
Mjumbe mwingine, Kafiti Kafiti, ameipongeza NSSF kwa uwekezaji wa mradi huo mkubwa, akieleza kuwa unatarajiwa kuleta manufaa makubwa kwa taifa na jamii kwa ujumla.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba, amewashukuru wajumbe wa kamati hiyo kwa kufanya ziara ya kikazi na kujionea maendeleo yaliyofikiwa katika mradi huo.