Watatu mbaroni kwa tuhuma za kubaka

Muktasari:
- Polisi mkoani Manyara, inawashikilia watu wa watu wakazi wa mjini Babati kwa tuhuma za kumbaka msichana mmoja.
Babati. Polisi Mkoani Manyara, inawashikilia watu watatu wakazi wa mjini Babati kwa tuhuma za kubaka kwa kundi kwa msichana mmoja mwenye umri wa miaka 18.
Pamoja na kumbaka msichana huyo vijana hao wanadaiwa kufanya uharibifu wa eneo hilo walilofanya ubakaji kwa kuharibu baadhi ya samani za nyumba iliyofanyika tukio hilo.
Mmoja kati ya ndugu wa msichana aliyefanyiwa tukio hilo Richard Hotay akizungumza na Mwananchi leo Novemba 10, amesema pamoja na watu hao kushikiliwa na Polisi bado kuna sintofahamu ya tukio hilo lililotokea kona ya Nakwa.
Hotay amesema vijana hao watatu waliombaka msichana huyo wakiongozwa na Mathayo God (24) maarufu kwa jina la Rasi walitaka kumaliza kesi hiyo kwa kumpa msichana aliyebakwa Sh800,000.
"Wazazi wa vijana waliobaka walitaka kutoa hiyo fedha ili kesi irudi nyumbani ila bado wanashindwana bei hivyo tunaiomba Serikali ichukue hatua ili wafikishwe mahakamani," amesema.
Hata hivyo, msichana aliyebakwa ambaye tunahifadhi jina lake amesema yeye hakubaliani na chochote zaidi ya kutaka watuhumiwa hao waliombaka wafikishwe mahakamani.
"Umeona wapi kesi ya kubaka ikawa na mazungumzo ya pande mbili, mimi polisi waliniambia nisubirie wataniita hivyo bado nasubiri ili twende mahakamani," amesema msichana huyo aliyebakwa.
Jirani wa eneo hilo, Mustafa Hassan amesema ndugu wa vijana waliobaka wameanza kulipa gharama za uharibifu walioufanya kwa kulipia fedha za matengenezo.
"Kwenye grocery hiyo wameshatengeneza mlango, madirisha, meza na redio ila bado sabufa na meza ya kioo cha mlango walioharibu kabla ya kufanya ubakaji huo," amesema Hassan.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Kamishna Msaidizi ACP, George Katabazi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo la ubakaji.
Kamanda Katabazi amesema tukio hilo lilitokea mjini Babati Novemba 3, mwaka huu saa 6 usiku kwenye mtaa wa Ngarenaro, kata ya Bagara.
Amesema watuhumiwa watatu wanashikiliwa na Polisi na pindi uchunguzi wa tukio hilo ukikamilika watawafikisha mahakamani watu hao.