Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Watatu wafariki dunia, wengine 48 kuokolewa ajali ya boti Ziwa Victoria

Muktasari:

  • Watu watatu wamefariki dunia na wengine 48 kuokolewa baada ya boti iliyokuwa imebeba zaidi ya abiria 50 kuteketea kwa moto usiku wa kuamkia leo katika Ziwa Victoria, ikiwa safarini kutoka Kisiwa cha Gozba mkoani Kagera kuelekea Mwanza. Miongoni mwa waliofariki ni mtoto wa miaka 10 huku uchunguzi wa chanzo cha moto ukiendelea.

Mwanza. Watu watatu wamefariki dunia na wengine 48 wameokolewa baada ya boti iliyokuwa imebeba zaidi ya abiria 50 kuteketea kwa moto katika Ziwa Victoria usiku wa kuamkia leo Alhamisi, Julai 9, 2026.

Waliofariki ni watu wazima wawili na mtoto mmoja mwenye umri wa miaka 10, huku manusura wakinusurika baada ya juhudi za uokoaji zilizofanywa na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kushirikiana na wavuvi wa eneo husika.

Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mwanza,  Elisa Mugisha, amesema katika taarifa iliyotolewa leo Alhamisi Julai 9,2026  kuwa operesheni ya uokoaji ilifanikiwa kuwaokoa watu 48.

Manusura wa ajali ya boti iliyoteketea kwa moto katika Ziwa Victoria, Emmanuel Aloyce, akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza kuhusu namna alivyonusurika katika tukio hilo. Picha na PraiseGod Mgumba.

"Waliofariki ni watu wazima wawili wanaokadiriwa kuwa na umri wa miaka 70, mwanaume, na miaka 45, mwanamke, ambao utambulisho wao bado haujafahamika, pamoja na mtoto Godson Stephen mwenye umri wa miaka 10," amesema Mugisha.

Amesema boti hiyo inayomilikiwa na Paschal  Ng'hwang'hwa, iliteketea kabisa pamoja na mizigo iliyokuwa ndani yenye uzito unaokadiriwa kufikia tani 6.5.

Mugisha amesema uchunguzi wa kubaini chanzo cha moto unaendelea na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kushirikiana na mamlaka nyingine husika.

Aidha, ametoa pole kwa familia zilizopoteza ndugu na jamaa zao katika tukio hilo na kuwataka wananchi, wamiliki wa vyombo vya usafiri majini na wadau wa sekta hiyo kuendelea kuzingatia kanuni na taratibu za usalama ili kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza wakati wa dharura.

Wananchi wakishuhudia manusura wa ajali ya boti iliyoteketea kwa moto katika Ziwa Victoria wakifikishwa nchi kavu jijini Mwanza. Picha na PraiseGod Mgumba.

Kwa mujibu wa Kaimu Ofisa Mfawidhi wa Ofisi ya Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (Tasac) Mkoa wa Mwanza, Paul Msokwa, taarifa za tukio hilo zilipokewa  saa 11:00 alfajiri, na mara moja vikosi vya uokoaji vikaanza operesheni iliyowezesha kuwaokoa watu 48.

Amesema katika awamu ya kwanza waliokolewa watu 33 na kupelekwa Bwiro, huku watu wengine 15 wakiokolewa baadaye na kupelekwa Kisiwa cha Lyamwenge kilicho jirani na Kisiwa cha Kunene.

"Watu waliookolewa katika awamu ya kwanza walipelekwa Hospitali ya Wilaya ya Nansio kwa ajili ya kupatiwa matibabu, huku waliobaki wakipelekwa eneo la Bwiro lililopo kati ya visiwa vya Kunene na Lyamwenge ambako tukio hilo lilitokea," amesema Msokwa.

Akizungumzia usalama wa usafiri wa majini, Mwenyekiti wa Soko la Samaki la Kimataifa la Kirumba Mwaroni, Fikiri Makafu, ameiomba Serikali kufanya jitihada za kurejesha huduma ya meli ya MV Clarias, akisema ilikuwa msaada mkubwa kwa wakazi wa visiwa vya Ziwa Victoria.

"Kuwepo kwa meli hiyo kulikuwa mkombozi mkubwa kwa wakazi wa visiwa. Ikiendelea kutoa huduma, kiwango cha usalama kitaongezeka kwa kiasi kikubwa," amesema.

Baadhi ya manusura wamesema safari ilianza  saa 3:00 usiku kutoka Kisiwa cha Gozba, lakini ilipofika saa 7:00 usiku boti hiyo ilikumbwa na moto uliosababisha taharuki kubwa.

Manusura wa ajali ya boti iliyoteketea kwa moto katika Ziwa Victoria, Elia Samweli, akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza kuhusu tukio hilo. Picha na PraiseGod Mgumba.

Emmanuel Aloyce, ambaye alikuwa baharia wa boti hiyo, amesema awali waligundua mfumo wa maji wa kupoza injini ulikuwa umeziba na baadaye moto ukazuka.

"Baada ya kugundua moto umetokea, nilitumia mafunzo niliyopata kuwaelekeza abiria wote kuvaa maboya. Hatua hiyo ndiyo iliyochangia kwa kiasi kikubwa kuokoa maisha yetu," amesema.

Naye manusura mwingine, Elia Samweli, amesema alikuwa amelala wakati tukio hilo lilipotokea na alishtuliwa na sauti ya mhandisi aliyekuwa akiwataka abiria waamke haraka.

"Nilikuwa nimelala. Kilichonishtua ni sauti ya mhandisi akisema, 'Amkeni, tumekwisha.' Nilipoamka nilikuta moto umewaka kwenye boti. Sikujua chanzo chake, lakini nilichukua boya langu na kuruka majini kama walivyofanya wengine. Namshukuru Mungu nimepona," amesema.

Boti hiyo ilikuwa ikisafirisha abiria pamoja na mizigo kutoka Kisiwa cha Gozba mkoani Kagera kuelekea Mwanza kabla ya kuteketea kwa moto katikati ya Ziwa Victoria.