Watatu wafikishwa mahakamani kwa kukutwa na nyama ya nguruwe pori

Muktasari:
Watu watatu wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka mawili ikiwemo la kukutwa na nyama ya nguruwe pori na swala pala.
Dar es Salaam. Watu watatu wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka mawili ikiwemo la kukutwa na nyama ya nguruwe pori na swala pala.
Washtakiwa hao ni Angela Kyoma, Dorice Mwamasangula na Elias Mputa wakazi wa Keko Magulumbasi wanakabiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi.
Wakili wa Serikali, Mussie Kaima akisoma hati ya mashtaka leo Alhamisi Februari 3,2022 mahakamani hapo amedai kuwa washtakiwa hao Januari 27, 2022 walikutwa na vipande 22 vya nguruwe pori bila kibali cha mkurugenzi wa wanyama pori vyenye thamani ya Sh970,053.
Alidai katika shtaka la pili kati ya Januari27 walikutwa na vipande nane vya swala pala vyenye thamani ya Sh 900,773 bila ya kuwa na kibali cha mkurugenzi wa wanyama pori.
Kaima ameiomba mahakama hiyo ipange tarehe nyingine ya kutajwa kwa kesi hiyo kwa sababu upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika.
Hakimu Mkazi Mkuu, Ramadhani Rugemalira amesema dhamana kwa watuhumiwa hao ipo wazi ambapo wanatakiwa kila mmoja awe na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya Sh1 milioni na barua zinazowatambulisha.
"Hii ni kesi ya uhujumu uchumi na fedha mnazoshtakiwa nazo ni chini ya Sh10 milioni hivyo mnayo haki ya kupata dhamana. Kila mmjoa alete wadhamini wawili watakaosaini bondi ya Sh1 milioni” amesema Rugemalira.
Washtakiwa hao wameshindwa kutimiza masharti ya dhamana wamepelekwa gerezani hadi Februari 16, 2022.