Watatu wakamatwa kwa tuhuma wizi wa kaboni, uvamizi

Mkuu wa Wilaya ya Chunya Mkoa wa Mbeya, Saimon Mayeka.

Muktasari:

  • Mbali na kufanya uharifu huo pia wamejeruhi wafanyazi watatu kwa mapanga waliokuwa zamu sambamba na kumbaka mwanamke mmoja.

Chunya. Mkuu wa Wilaya ya Chunya Mkoa wa Mbeya, Saimon Mayeka amethibitisha  kutokea kwa tukio hilo na kwamba  watu watatu wamejeruhiwa kwa mapanga  baada ya kuvamiwa kwenye  mgodi wa mfanyabiashara Emmanuel Mwandolela.

Mayeka ameliambia Mwananchi leo Jumatatu, Oktoba 9, 2023 na kwamba limetokea katika Mtaa wa Kalungu Juu Kata ya Makongorosi Wilaya ya Chunya Mkoa wa Mbeya na kwamba licha kujeruhi wamefanikiwa kuiba kaboni kilo 350.

“Tukio limetokea umbali wa kilometa 4 kutoka Makao Makuu ya mji wa Makongorosi na kwamba kaboni iliyoibiwa ilikuwa kwenye hatua za uchakataji wa madini ya dhahabu na kufafanua kuwa  kati ya watu watatu waliojeruhiwa mmoja  hali mbaya na kukimbizwa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya,” amesema.

Ameongeza kuwa, “Tayari watu watatu wanashikiwa kuhusika na tukio hilo ambao wamekamatwa wakiwa na pikipiki mbili na kaboni kilo 200 ambazo zinasadikika kuibiwa katika tukio hilo la uvamizi,” amesema.

Ameongeza kuwa, “Watuhumiwa hao watatu wanaoshikiliwa siyo wakazi wa Chunya kwa sasa tunaendelea na  uchunguzi kwa hatua zaidi,”amesema Mayeka.

Amesema kama Serikali ilishaweka utaratibu kwa kila kata kutenga maeneo kwa ajili kuchenjulia madini ya dhahabu ili kuepuka changamoto kama hizo za uvamizi.

Makamu Mwenyekiti Umoja wa wenye  migodi katika Mamlaka ya Mji mdogo wa Makongorosi, Antigone Kavishe amesema kumekuwepo na matukio ya uvamizi ambayo  yanatishia amani na kwamba mbali na kujeruhi pia wamembaka mfanyakazi wa kike.

Amesema katika uvamizi huo mfanyakazi mmoja ambaye alikatwa katwa mapanga na na kuwa na majeraha makubwa mwilini mwake kahamishiwa Hospitali ya Rufaa Kanda kwa matibabu zaidi.