Watembelea kilometa 16 kufuata shule Kisarawe

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge.

Muktasari:

  • Zaidi ya watoto 320 wilayani Kisarawe wamekuwa wakitembelea umbali wa kilometa 16 kwenda na kurudi shule, kutokana na kata wanayoishi ya Kitanga kukosa shule ya sekondari.

Kisarawe. Halmashauri ya Wilaya Kisarawe mkoani Pwani imepewa siku 14 kukamilisha ujenzi wa shule ya sekondari ya Kitanga iliyopo Kata ya Msimbu ili watoto zaidi ya 320 wa vitongoji vitatu wasitembee umbali wa kilomita 16 kila siku kwenda na kurudi shule.

Agizo hilo limetolewa jana Novemba 10 na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge baada ya kutembelea kata hiyo na kubaini kuwepo uhitaji mkubwa wa Sekondari kwenye eneo hilo.

"Nimeambiwa lengo la shule hii inapofika Januari mwaka ujao shule hii ianze kutumika, sasa nitoe maagizo haya, nitatoa siku 14 yaani wiki mbili kuanzia sasa nilipofikia hapa hii shule ikamilike kabla au ifikapo Novemba 23 ili kuwezesha watoto wetu wa vitongoji vitatu wasome na wasitembelee kilomita 16,” amesema Kunenge.

Ametaka pia shule hiyo ifikishiwe umeme kabla ya kufika Desemba 15 mwaka huu.

“Katika hili mtaangalia utaratibu wenu ulivyo, kuna utaratibu wa Serikali ambapo wananchi wanapata nishati ya umeme sasa muangalie kitakachowezekana itapendeza zaidi hata wale wananchi wanaopitiwa na umeme nao wakaweza kunufaika na nishati hii kwa kupitia shule," amesema.

Katika hatua nyingine, RC Kunenge ammtaka Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi Vijijini (RUWASA) wilayani Kisarawe kuhakikisha huduma ya maji safi na salama yanapatikana shule hiyo.

Awali akitoa taarifa ya ujenzi wa shule hiyo, msimamizi wa mradi huo ambaye pia mkuu wa shule hiyo, Anicet Sauli amesema inajengwa kwa zaidi ya Sh529.99 milioni na ipo chini ya programu ya kuboresha elimu ya sekondari (SEQUIP) 2022/2023.

Kaitaba Sule anaishi katika eneo hilo, ameishukuru Serikali kwa ujenzi wa shule hiyo.

“Itaondoa kabisa mdondoko wa wanafunzi wa kike waliokua wanaacha shule kutokana na kupata ujauzito za lifti, utaongeza chachu ya kuongezeka kwa huduma nyingine za kijamii eneo hilo,” amesema.