Watendaji sekta za mifugo, uvuvi wawekwa kitimoto

Watendaji sekta za mifugo, uvuvi wawekwa kitimoto

Muktasari:

  • Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amewataka watendaji wanaofanya kazi ya ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali katika minada, mialo na vituo vya Ukaguzi kufanya kazi hiyo kwa uaminifu na uadilifu huku akionya kuwa hawataweza kuendelea kuwa na mtendaji atakayejihusisha na vitendo vinavyosababisha upotevu wa mapato ya Serikali.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amewataka watendaji wanaofanya kazi ya ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali katika minada, mialo na vituo vya Ukaguzi kufanya kazi hiyo kwa uaminifu na uadilifu huku akionya kuwa hawataweza kuendelea kuwa na mtendaji atakayejihusisha na vitendo vinavyosababisha upotevu wa mapato ya Serikali.

Waziri Ndaki aliyasema hayo katika kikao cha tathmini ya ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali kwa mwaka uliopita na kuweka malengo mapya ya ukusanyaji mapato kwa mwaka 2021/22 kilichofanyika jijini Dodoma jana Julai 23, 2021.

Akiongea na watendaji hao aliwaeleza bayana kuwa ili waweze kufikia malengo ya kukusanya Sh90 bilioni walizojiwekea kukusanya kwa mwaka huu wa fedha ni lazima wafanye kazi hiyo kwa uaminifu na uadilifu kinyume na hapo hawatafanikiwa kufikia malengo.

"Katika kipindi ambacho nimekuwa hapa wizarani nimepata taarifa nyingi kuhusu baadhi yenu kujihusisha na vitendo vya upotevu wa mapato, acheni kufanya hivyo kwa sababu tukikugundua hatutaweza kuendelea na wewe," alisema Ndaki

Aliongeza kuwa kumekuwa na vitendo vingi vya upotevu wa maduhuli ya Serikali ambavyo vimekuwa vikifanywa na baadhi ya maafisa  wasiokuwa waaminifu na  kupelekea serikali kutopata mapato yanayostahili.

Waziri Ndaki aliendelea kusema kuwa Rais, Samia Suluhu Hassan amewaahidi Watanzania mambo mengi mazuri na  ili mambo hayo yaweze kutekelezeka yanahitaji pesa, na miongoni mwa pesa zinazotegemewa na Serikali ni pamoja na zile zinazokusanywa kutoka kwenye minada, mialo na vituo vya ukaguzi.

Aliendelea kubainisha kuwa kwa mwaka huu atafuatilia kwa karibu utendaji kazi wa watendaji hao na amepanga kukutana nao kila robo mwaka ili kupima utendaji kazi wa kila mmoja ili kuona kama malengo yaliyowekwa yanafikiwa.

"Nitaendelea kuwatembelea katika vituo vyenu vya kazi, nitakuja kwa taarifa na wakati mwingine bila taarifa na nikifika nitataka kujua mmefikia wapi kuhusu ukusanyaji wa maduhuli," alisisitiza Ndaki

Aidha, Waziri Ndaki aliwaelekeza Watendaji hao kupelekea taarifa ya minada isiyo rasmi ili aitambue na kuifuta kwa sababu imekuwa ni kikwazo kwa minada inayotambulika kisheria.

 Pia aliwasisitiza watendaji hao kuendelea kufanya kazi ya Serikali kwa haki ikiwa ni pamoja na kuzuia uvuvi haramu na utoroshaji wa mifugo kwani vitendo hivyo vimekuwa ni sehemu ya upotevu wa mapato ya Serikali.