Watoa tiba kwa kutumia vyakula wapigwa 'stop'

Watoa tiba kwa kutumia vyakula wapigwa 'stop'

Muktasari:

  • Serikali imesema  watu wanaojiita watoa tiba kwa kutumia vyakula wanatakiwa kuendesha shughuli hiyo kwa kibali cha Wizara ya Afya.

Dodoma. Serikali imesema  watu wanaojiita watoa tiba kwa kutumia vyakula wanatakiwa kuendesha shughuli hiyo kwa kibali cha Wizara ya Afya.

Katazo hilo limetolewa na  mganga mkuu wa Serikali,  Dk Aifello Sichwale jana Ijumaa Septemba 11, 2021  jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu magonjwa yasiyoambukiza ambayo baadhi amesema yanatokana na ulaji wa vyakula usiofaa.

Dk Sichwale amesema kumeibuka wimbi kubwa la wanaojiita watoa tiba mbadala kwa wananchi wakitumia mchanganyiko wa vyakula na hawana  utaalamu wowote.

Amesema siyo dhambi  mtu kutoa elimu ya mchanganyiko wa chakula lakini anapaswa kuwa amepewa kibali na Wizara ya Afya.

“Hatuwezi kuruhusu watu wakaendelea kujitangaza katika mambo yenye kuhatarisha afya za watu, kama kuna mtu ana uwezo wa kutoa elimu ya mchanganyiko huo aje kwetu na tutakapojiridhisha kuwa anaweza kusaidia jamii, tutampa kibali cha kufanya hivyo ili asisumbuliwe,” amesema Dk Sichwale.

Ameeleza sababu za kutoa zuio hilo ni kutokana na kuibuka kwa magonjwa yasiyoambukiza yanayotokana  na ulaji wa vyakula usiofaa chanzo kikiwa washauri wa mchanganyiko wa chakula.

Amesema Serikali itaanza kuwachukulia hatua kali watu watakaokaidi agizo hilo ili iwe fundisho kwa wengine akisema wakati utafika ambao vyombo mbalimbali vitaanza kufuatilia jambo hilo na kuwakamata.