Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Watoto 626 wafanyiwa ukatili Maswa ndani ya miezi 12

Moja ya mabango yenye ujumbe mbalimbali yaliyobebwa na watoto wakati wa maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika wilayani Maswa. Picha na Samwel Mwanga

Muktasari:

  • Matukio 447 sawa na asilimia 71.4 ya matukio yote, huku watoto wa kiume wakihusika katika matukio 179 sawa na asilimia 28.6.

Maswa. Jumla ya watoto 626 katika Wilaya ya Maswa, Mkoa wa Simiyu, wamefanyiwa vitendo mbalimbali vya ukatili katika kipindi cha Julai 2025 hadi Juni 2026, huku wa kike wakiongoza kuathirika zaidi kuliko watoto wa kiume.

Takwimu hizo zimetolewa leo Jumane, Juni 16, 2026 na Kaimu Ofisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Maswa, Salome Bahati wakati akisoma taarifa ya hali ya vitendo vya ukatili dhidi ya watoto katika maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yaliyofanyika wilayani humo.

Bahati amesema kati ya matukio 626 yaliyorekodiwa, watoto wa kike walihusika katika matukio 447, sawa na asilimia 71.4 ya matukio yote, huku watoto wa kiume wakihusika katika matukio 179, sawa na asilimia 28.6.

Amesema ongezeko la matukio yaliyoripotiwa linachangiwa na kuongezeka kwa mwamko wa wananchi kutoa taarifa za vitendo vya ukatili vinapotokea, hali inayowezesha mamlaka husika kufuatilia matukio hayo na kuwachukulia hatua wahusika.

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dk Vicent Naano amekemea vitendo vya ukatili dhidi ya watoto na kusisitiza kuwa Serikali haitamvumilia mtu yeyote atakayebainika kujihusisha na vitendo hivyo.

Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dk Vicent Naano, akizungumza katika maadhimisho ya sherehe ya mtoto wa Afrika katika kijiji cha Kinamwigulu. Picha na Samwel Mwanga

Amewataka wananchi kuendelea kutoa taarifa za matukio ya ukatili mara yanapotokea ili wahusika wachukuliwe hatua za kisheria, huku akisisitiza umuhimu wa wazazi na walezi kutekeleza wajibu wao wa kuwalea watoto katika misingi bora ya maadili, ulinzi na malezi.

“Malezi bora yanaanzia nyumbani. Wazazi na walezi wanapaswa kuwa karibu na watoto wao ili kubaini changamoto wanazokutana nazo na kuzitatua kwa wakati,” amesema Dk Naano.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Maisha Mtipa amesema mapambano dhidi ya ukatili wa watoto yanahitaji ushirikiano wa jamii nzima.

Amesema jamii inapaswa kuhakikisha watoto wanalindwa dhidi ya aina zote za ukatili na wanapata haki zao za msingi, ikiwemo elimu, huduma za afya, ulinzi na malezi bora.

“Mtoto anahitaji mazingira salama ili aweze kukua na kutimiza ndoto zake. Ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha watoto wanalindwa na wanapatiwa haki zao za msingi, hususan elimu ambayo ni msingi wa maendeleo yao ya baadaye,” amesema.

Kaimu Afisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Maswa, Salome Bahati akisoma taarifa ya vitendo vya ukatili kwa watoto wilayani humo wakati wa maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika. Picha na Samwel Mwanga

Baadhi ya wananchi waliohudhuria maadhimisho hayo wamesema takwimu zilizotolewa zinaonyesha bado kuna haja ya kuendelea kutoa elimu kuhusu ulinzi wa watoto.

Mkazi wa Kata ya Buchambi, Mariam Shabani amesema kuongezeka kwa taarifa za ukatili kunadhihirisha kuwa wananchi wameanza kupata ujasiri wa kuripoti matukio hayo, ingawa elimu zaidi bado inahitajika kwa wazazi na walezi.

Naye John Magesa mkazi wa Maswa Mjini, amesema viongozi wa vijiji na vitongoji wanapaswa kushirikiana na wananchi kufuatilia mazingira yanayoweza kuhatarisha usalama wa watoto.

Kwa upande wake, Neema Senzia amesema wazazi wanapaswa kutumia muda mwingi kuzungumza na watoto wao ili waweze kueleza changamoto wanazokumbana nazo na kusaidiwa kwa wakati.

“Mtoto anapokuwa karibu na mzazi wake ni rahisi kubaini mapema kama anapitia changamoto au kufanyiwa ukatili. Malezi bora yanaanzia nyumbani,” amesema.