Watoto, vijana milioni 1.2 walivyosaidiwa kukabili umaskini

Mkurugenzi wa Shirika la kimataifa la Compassion Tanzania, Merry Lema

Muktasari:


  • "Zaidi ya watoto na vijana milioni 1.2 wamepatiwa msaada wa elimu na ujuzi kupitia Compassion Tanzania, kuwawezesha kujiajiri na kujikwamua kiuchumi.

Arusha. Zaidi ya watoto na vijana milioni 1.2 kutoka kaya maskini wamepatiwa msaada wa kielimu na ujuzi uliowasaidia kujiajiri na kuweza kujikwamua kiuchumi.

Vijana hao wamesaidiwa kupitia huduma ya maendeleo ya mtoto na kijana inayotekelezwa na makanisa washirika kwa kushirikiana na shirika la kimataifa la Compassion Tanzania.

Akizungumza kwenye hafla ya vijana 65,000 wahitimu wa programu ya maendeleo ya mtoto na vijana nchini Tanzania leo Aprili 18, 2024, Mkurugenzi wa Shirika la Compassion Tanzania, Merry Lema amesema mbali na wahitimu hao, zaidi ya watoto na vijana milioni 1.2 wamesaidiwa kupata elimu na ujuzi uliowasaidia kujiajiri na kuendesha maisha yao na sasa hawagemei tena ufadhili.

“Nitoe wito kwenu mliojiweza, msikae mbali na kituo kilichowasaidia kujikwamua kimaisha, bali muwe sehemu ya wafadhili wa wenzenu ambao kwa sasa wanasaidiwa katika vituo hivi vya maendeleo ya mtoto na vijana,” amesema Merry.

Amesema kupitia programu hiyo, pia wamefanikiwa kuboresha maisha ya watoto na vijana, hasa wanaotoka katika familia zenye uhitaji kupitia miradi inayolenga kuboresha afya na lishe ya mama na mtoto, elimu, uzalishaji pamoja na usafi wa mazingira.

Mbali na kusaidia vijana na watoto, shirika la Compassion Tanzania, katika operesheni zake za robo karne nchini, pia limezikwamua zaidi ya kaya 200,000 kutoka katika umaskini uliokithiri na kuziwezesha kiuchumi.

“Uwezeshaji huo ni pamoja na mafunzo ya kuanzisha na kuendesha biashara ndogondogo, kilimo na ufugaji wa kisasa pamoja na benki za jamii za vijijini,” amesema Merry.

Meya wa jiji la Arusha, Maximillian Irage, aliyehudhuria mkutano wa vijana wa chuo cha Compassion amesema Serikali iko katika mapambano makubwa ya kukabiliana na watoto wa mitaani, hivyo kwa wale waliosadiwa wakafanikiwa wajitokeze kuwasaidia wenzao, ili Taifa liwe na vijana wanaoweza kutegemewa baadaye na si tegemezi.

Pia amesema ni wakati wa halmashauri zote nchini kuanzisha mfuko maalumu wa kuwasaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu, ili kuwapunguzia mzigo wa michango kwenye taasisi za elimu wanazosoma au kuwagharamia mafunzo ya ufundi na ujasiriamali ili wasikwame.

“Niwatake vijana nao kuunda vikundi na kubuni mawazo na kutengeneza andiko la miradi ya kujikwamua kiuchumi na kuziwasilisha katika halmashauri, ili kupatiwa fedha za mikopo,” amesema Lyimo.

Naye Abdulazizi Ndela, maarufu kama “Dogo Janja” amesema wameandaa hafla hiyo kwa ajili ya kuwatia moyo wenzake wanatoka familia duni.

“Tumekuja kuwaambia kuwa wasiangalie historia ya maisha yao kuwa wamezaliwa katika hali duni, bali watie nguvu katika ndoto zao na watafanikiwa kujikwamua kimaisha,” amesema Dogo Janja.