Watoto wa vigogo CCM wapenya ubunge Eala

Muktasari:

Wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamepitisha majina manane kati ya 26 kwenda kugombea ubunge wa Bunge la Afrika Mashariki (Eala).


Dodoma. Wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamepitisha majina manane kati ya 26 kwenda kugombea ubunge wa Bunge la Afrika Mashariki (Eala).

CCM inaungana na vyama vya ACT-Wazalendo na Chama cha Wananchi (CUF) kuhitimisha michakato ya ndani ya kuwapata wagombea wa nafasi hizo.

Katika Bunge la Eala, Tanzania ina nafasi tisa, kati ya hizo CCM inazo nane na moja itakuwa ya upinzani itakayowaniwa na ACT-Wazalendo yenye wagombea wawili na Chama cha Wananchi (CUF) iliyowapitisha wagombea 12.

Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda, ndiye aliyesimamia mchujo wa majina ya makada hao na kutangaza matokeo hayo.

Akizungumza na waandishi wa habari, Pinda alisema wamehitimisha vizuri na katika upande wanawake Zanzibar waliopiga kura ni 222 kura zilizoharibika mbili hivyo kura halali ni 220 ambapo Nadra Juma Mohamed alipata kura 150

Kwa wanaume kura zilizopigwa ni 222 zilizohabika 6 na halali ni 216 ambapo Dk Abdula Hassan Makame alipata kura 204, Machano alipata kura 180

Wanawake Tanzania bara ziliharibika 3, 217 zilibaki ambapo Angela Kizigha alipata kura 179 na Dk Shogo Mlonzi alipata kura 178 huku kwa wanaume Dk Ng’waru Maghembe alipata 128, James Milya alipata kura 133 na Anar Kachwamba alipata 130

Uchaguzi wa wabunge hao utafanyika kwenye mkutano wa Bunge utakaoanza keshokutwa na Bunge limeshatoa taratibu za uchaguzi huo utakaofanyika Septemba 22 mwaka huu, saa 5 asubuhi mara baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu.

Wagombea hao wanane wa CCM, walipatikana jana katika uchaguzi uliofanyikia Makao Makuu ya chama hicho ikiwa ni siku mbili zimepita tangu Kamati Kuu ya CCM, kupitisha majina hayo kati ya 179 waliojitokeza kuomba nafasi hiyo.

Baadhi ya waliopitishwa ni watoto wa vigogo akiwemo, Dk Ng’waru Maghembe anayetetea nafasi hiyo, mgombea huyo ni mtoto wa aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe.

Yupo pia James Millya ambaye kwa nyakati tofauti alishika nyadhifa mbalimbali ndani na nje ya chama hicho.

Mwaka 2015, alitimkia Chadema ambako kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huo alishinda ubunge wa Simanjiro lakini ilipofika Oktoba 2018 akajiuzulu na kurudi CCM na uchaguzi mdogo ulipofanyika akafanikiwa kushinda na kurudi bungeni.

Mwingine aliyeshinda katika wanaume watatu Tanzania Bara ukiwaacha Dk Ng’waru na Millya ni Anar Kachwamba ambaye anatajwa kuwa na uhusiano wa karibu wa kifamilia na Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dk Ashatu Kijaji.

Upande wa wanawake walioshinda ni Angela Kizigha, aliyewahi kushika wadhifa huo huku Dk Shogo Mlonzi anayeelezwa naye kuwa na nasaba na Queen Mlozi, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake (UWT) wa CCM.

Kwa upande wa Zanzibar, wanaume waliopitishwa ni Machano Ali Machano na Dk Abdulla Hasnuu Makame. Kundi la wanawake ni nafasi moja na aliyeshinda ni Maryam Said Mussa.

Wagombea hao wa CCM wanaungana na wale wa ACT-Wazalendo ambao ni Pavu Abdallah na Ado Shaibu akiwania nafasi hiyo huku CUF yenyewe ikipitisha majina 12.