Watu 130 mbaroni kwa tuhuma za kufanya uhalifu
Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania, David Misime. Picha na Mtandao
Muktasari:
- Miongoni mwao ni makada na viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) waliokamatwa kati ya Julai 4 na 7, 2026.
Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Tanzania linawashikilia watu 130 kwa tuhuma mbalimbali ikiwamo kudaiwa kushiriki katika vikao vya ndani, kupanga na kuhamasisha vitendo vya kihalifu nchini.
Mbali na hivyo, limeapa kuendelea kulinda wananchi kwa kuwapa usalama wa kutosha wakati wote huku likiendelea kuwasaka watuhumiwa wengine ambao bado hawajakamatwa ili wachukuliwe hatua za kisheria
Ingawa jeshi hilo halijaweka wazi majina ya watuhumiwa hao wanaoshikiliwa katika vituo mbalimbali vya polisi, lakini miongoni mwao ni makada na viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) waliokamatwa kati ya Julai 4 na 7, 2026.
Akizungumza kupitia taarifa kwa umma iliyotolewa leo Alhamisi, Julai 9, 2026, kuhusu hali ya usalama nchini, Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime amesema hali ya usalama inaendelea kuwa shwari kutokana na ushirikiano kati ya jeshi hilo na vyombo vingine vya ulinzi na usalama.
Misime amesema taarifa zilizotolewa Juni 19 na Julai 5, 2026 zilieleza hatua zinazoendelea kuchukuliwa ili kuhakikisha wananchi wanaendelea na shughuli zao za kila siku katika mazingira ya amani, utulivu na usalama.
Amesema katika kipindi hicho, jeshi hilo liliendelea kufuatilia kwa karibu taarifa za uhalifu uliokuwa ukihamasishwa kupitia mitandao ya kijamii na majukwaa mengine, vikiwamo vikao vya ndani.
"Kufuatia ufuatiliaji huo, jumla ya watuhumiwa 130 waliokuwa wakipanga, kushiriki katika vikao vya ndani, kuandaa na kusambaza taarifa za kuhamasisha vitendo hivyo vya kihalifu wamekamatwa katika mikoa mbalimbali nchini. Uchunguzi unaendelea kukamilishwa ili hatua nyingine za kisheria zifuate," amesema Misime.
Misime amesema vitendo vinavyodaiwa kupangwa na watuhumiwa hao ni kuandaa na kusambaza taarifa za uchochezi kupitia mitandao ya kijamii, kuhamasisha mauaji ya viongozi na wananchi.
“Pia, walikuwa wanahamasisha kuchoma shule moto, kulipua transfoma za umeme ili kusababisha nchi kuwa gizani, kuharibu na kupora mali za umma na binafsi, pamoja na kuua askari wa vyombo vya ulinzi na usalama kwa lengo la kupora silaha,” amesema.
Misime amewataka wananchi kutosambaza ujumbe wowote unaohamasisha vitendo vya kihalifu wanapoupokea kupitia mitandao ya kijamii, bali wauondoe na kutoa taarifa kwa mamlaka husika.
“Jeshi la Polisi linaendelea kuwahakikishia wananchi usalama wa kutosha wakati wote na linaendelea kuwafuatilia watuhumiwa wengine ambao bado hawajakamatwa ili wachukuliwe hatua za kisheria,” amesema.
Wakati Jeshi la Polisi likitoa taarifa hiyo, Chadema kupitia kanda zake mbalimbali imelaani kukamatwa na kuendelea kushikiliwa kwa viongozi na wanachama wake, ikidai hatua hizo hazina msingi wa kisheria.
Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Yohana Kaunya amesema viongozi wanne wa chama hicho kutoka mikoa ya Tanga na Manyara walikamatwa Julai 4 na 5 kwa tuhuma za kuratibu maandamano yaliyokuwa yamepangwa kufanyika Julai 7.
Viongozi hao ni Katibu wa Chadema Handeni Vijijini, Ramia Kisalazo; Katibu wa Bawacha Mkoa wa Tanga, Nusura Kihiyo; Mwenyekiti wa Chadema Jimbo la Korogwe, Ezekiel Mbwilo; na Katibu wa Bavicha Wilaya ya Mbulu, Emanuel Hhari.
"Maandamano yenyewe hayakufanyika, hivyo hatuelewi walikuwa wanaratibu nini. Ndiyo maana tunalaani vikali vitendo hivi vya kuwakamata viongozi wetu," amesema Kaunya.
Kwa upande wa Kanda ya Pwani, Chadema imedai makada wake 12, akiwamo Abdala Mnyulu, Pendo Kileo na wanachama wengine 10 kutoka Jimbo la Kibamba, wanaendelea kushikiliwa katika Kituo cha Polisi Chang'ombe baada ya kukamatwa kati ya Julai 4 na 7.
Chama hicho kimesema kimewapeleka mawakili kufuatilia mwenendo wa kesi hizo na kutoa msaada wa kisheria.
Chadema Kanda ya Magharibi imesema Katibu wa Wilaya ya Mpanda, Richard Mponeja, anaendelea kushikiliwa tangu Julai 6, 2026 licha ya juhudi za viongozi wa chama hicho kufuatilia dhamana yake, huku ikilitaka Jeshi la Polisi kumuachia kwa mujibu wa sheria.
Wakati huohuo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilitangaza kuwakamata makada wanne wa Chadema Julai 4, 2026 kwa tuhuma za kupanga na kuhamasisha vurugu na vitendo vingine vya kihalifu katika Jiji la Mbeya.
Jeshi hilo limesema uchunguzi unaendelea kabla ya hatua nyingine za kisheria kuchukuliwa dhidi yao.
Mkoani Geita, Mwenyekiti wa Chadema Jimbo la Geita, Neema Chozaire anashikiliwa tangu Julai mosi, 2026. Polisi mkoani humo ilithibitisha kumshikilia Chozaire kwa makosa ya kijinai.
Suala hilo la Chozaire limefikishwa mahakamani na Chadema kwa kesi iliyofunguliwa Julai 8, 2026 katika Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Geita kwa shauri namba 15077 la mwaka 2026, chini ya hati ya dharura baada ya mwenyekiti huyo kushikiliwa kwa zaidi ya siku kumi bila kufikishwa mahakamani wala kupewa dhamana.
Mahakama hiyo imewataka Julai 14, 2026, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kufika mahakamani na kueleza sababu za kuendelea kushikiliwa Chozaire.
Mbali na hao, wengine ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita (RPC) na Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Geita (RCO).