Watu kadhaa wanusurika kifo, basi la B One Coach likiteketea kwa moto Hai
Muktasari:
- Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kilimanjaro, Jeremiah Mkomagi amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo, ambapo amesema chanzo chake ni kupasuka kwa tairi la ekseli ya nyuma upande wa kulia wa basi hilo, hali iliyosababisha tanki la mafuta kupasuka na gari hilo kushika moto.
Hai. Watu kadhaa wamenusurika kifo baada ya basi la Kampuni ya B One Coach kupata ajali na kuteketea kwa moto katika Wilaya ya Hai, Mkoa wa Kilimanjaro.
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kilimanjaro, Jeremiah Mkomagi amethibitisha kutokea ajali hiyo, ambapo amesema ilitokea usiku wa Juni 9, 2026, katika eneo la Rosinde, Kata ya Romu, Wilaya ya Hai.
Kwa mujibu wa Kamanda Mkomagi, chanzo cha ajali hiyo ni kupasuka kwa tairi la ekseli ya nyuma upande wa kulia wa basi hilo, hali iliyosababisha tanki la mafuta kupasuka na gari hilo kushika moto.
Basi kampuni ya B One Coach, wakati likiteketea kwa moto usiku wa Juni 9, 2026 katika eneo la Rosinde, kata ya Romu Wilaya ya Hai, Mkoani Kilimanjaro.
Kamanda Mkomagi amesema katika ajali hiyo, ambapo kulikuwa na abiria 23 na wafanyakazi watatu, hakuna majeruhi wala vifo, na kwamba hakuna abiria hata mmoja aliyeweza kuokoa chochote katika ajali hiyo, kwani mali zote ziliteketea kwa moto.
Kamanda Mkomagi amesema kuwa katika ajali hiyo hakuna majeruhi wala vifo, na kwamba hakuna hata abiria mmoja aliyefanikiwa kuokoa mali zake, kwani mizigo na vitu vyote vilivyokuwamo ndani ya basi hilo viliteketea kwa moto.
"Muda wa saa 4:41 usiku, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Kituo cha Hai tulipokea taarifa ya tukio la moto wa gari la abiria la Kampuni ya B One Coach. Askari walifika eneo la tukio na kukuta moto unawaka na kufanikiwa kuuzima," amesema Kamanda Mkomagi.
Basi kampuni ya B One Coach, baada ya kuteketea moto usiku wa Juni 9, 2026 katika eneo la Rosinde, kata ya Romu Wilaya ya Hai, Mkoani Kilimanjaro.
Kamanda Mkomagi amesema hasara iliyopatikana kutokana na ajali hiyo ni gari kuteketea kwa moto pamoja na mizigo ya abiria iliyokuwemo ndani ya basi hilo.
"Jeshi linaendelea kutoa elimu kwa wamiliki wa vyombo vya moto kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya majanga ya moto, pamoja na kufanya ukaguzi wa vyombo vyao mara kwa mara na kutoa taarifa mapema kwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kupitia namba ya dharura 114," amesema Kamanda Mkomagi.