Watu wasiojulikana wadaiwa kumbaka mwanamke hadi kufa Iringa

Tuesday November 02 2021
kubaka pic
By Berdina Majinge

Iringa. Watu wasiojulikana wamedaiwa kumbaka mwanamke mmoja hadi kufariki dunia na mwili wake kukutwa kwenye shimo la taka (dampo) katika Mtaa wa Mtwivila C uliopo Manispaa ya Iringa.

Mwili wa mwanamke huyo aliyetambuliwa kwa jina la Rehema Lukosi (57) mfanyabiashara maarufu wa mboga mboga na bagia kwenye mtaa huo umekutwa eneo la tukio na wapita njia waliokuwa wanapita asubuhi.

Vilio na simanzi vilitawala miongoni mwa wakazi wa Mtaa wa Mtwivila C, ambao wengi ni wateja wa mboga na bagia wa mjasiriamali huyo.

Shughuli za wakazi wa Mtwivila zilisimama kwa muda kutokana na mshangao wa tukio la unyama lililofanywa na watu wasiojulikana, ambapo pembeni ya mwili wa marehemu zilipatikana baadhi ya mboga ambazo zinadaiwa kubaki kwenye mauzo ya jana jioni.

Mtendaji wa Kata ya Mtwivila, Thadei Muhanga amesema kuwa alipata taarifa ya tukio la kukutwa mwili huo mapema asubuhi na kuarifu vyombo vya ulinzi.

“Kwa mujibu wa mumewe anasema jana jioni alimuaga anakwenda kuuza mboga lakini akitoka atapitia kwenye msiba kwahiyo hata mumewake hakuwa na wasiwasi aliamini mke wake amelala kwenye msiba”

Advertisement

“Alipata mshtuko baada ya kupigiwa simu kuja eneo la tukio na kushuhudia mkewe akiwa tayari amefariki dunia baada ya kufanyiwa unyama huo”amesema Muhanga

Mashuhuda wa tukio hilo wamesema kuwa marehemu hakuwa na shida na mtu na alikuwa mcheshi kwa kila aliyemuuzia mboga zake hivyo tukio hilo limewashangaza na kuwatia simanzi.

“Kwa kweli hakuwa na sida na mtu alikuwa ni mama anayejitafutia kipato chake na kuhudumia familia yake kwa sababu alikuwa ni mjasiriamali ambaye anaondoka asubuhi kwenda kutafuta riziki yake na kurudi jioni”

Kufuatia tukio hilo, wakazi wa Mtwivila wameiomba Serikali kushirikiana na wananchi kuimarisha ulinzi eneo hilo lenye historia ya vitendo vya uahalifu.

Romana Kitosi amesema “Tunaomba Serikali itusaidie kufyeka vitindi hivi vya ulanzi kwa nguvu ili eneo hili liwe wazi na salama majira ya jioni kwa sababu kumekuwa na matukio mengi yakitokea katika eneo hili hasa ya wizi na ubakaji”amesema

Ofisa Upelelezi Polisi Iringa, Gabriel Mukungu ametoa rai kwa wananchi kutoa taarifa zitakazowezesha kukamatwa kwa watuhumiwa ili wafikishwe kwenye vyombo vya sheria.

“Jeshi la Polisi mkoani Iringa linawapa pole wakazi wa Mtaa wa Mtwivila C kwa tukio hilo na tunaomba ushirikiano ili watuhumiwa wa matukio haya waweze kukamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria”amesema Mukungu

Mwili wa marehemu umepelekwa kuhifadhiwa chumba cha maiti katika Hospitali ya Rufaa Iringa huku uchunguzi ukiendelea.

Advertisement