Watu watano wadaiwa kupotea Lindi
Muktasari:
Watu watano wakazi wa Kijiji cha Rutamba Halmashauri ya Mtama wanadaiwa kuwa ni wanachama wa Chama cha Wananchi (CUF), wamepotea tangu Oktoba 30, 2021.
Lindi. Watu watano wakazi wa Kijiji cha Rutamba Halmashauri ya Mtama wanadaiwa kuwa ni wanachama wa Chama cha Wananchi (CUF), wamepotea tangu Oktoba 30, 2021.
Katibu wa CUF Wilaya ya Lindi, Shadhil Bosha amesema kuwa watu hao waliopotea ni wanachama wa chama hicho akidai kuwa walichukuliwa na watu wasiojulikana nyumbani kwao Oktoba 30, 2021 saa saba usiku.
"Tunaliomba Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa haraka ili familia na jamii iondolewe hofu," amesema Bosha.
Bosha aliwataja watu hao wanaodaiwa kupotea kuwa ni pamoja na Musa Fukutu, Hamisi Liendeka, Shaziri Chileu, Baraka Ali na Isumail Yahaya.
Mke wa Ismail Yahaya, Husna Litapwachi amesema Oktoba30, 2021 saa saba usiku walisikia mlango uikgongwa na watu watano huku akidai kuwa wawili wakiwa na silaha waliingia chumbani na kuwakuta wamelala kitandani na kuwaamuru washuke chini .
Litapwachi anasema baada ya hapo walikusanya simu na wakaondoka na mumewe.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, Foka Dinya amekiri kutokea kwa tukio hilo akisema kwamba Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi.
"Jeshi la polisi linaendelea na uchaguzi ili kubaini chanzo cha tukio na kujua wapi waliko" amesema Kamanda Dinya