Watu wawili wafariki dunia ajali baada ya magari kugongana uso kwa uso Daraja la Wami
Muktasari:
- Watu wawili wamefariki dunia na magari mawili kuharibika baada ya kugongana uso kwa uso katika Daraja la Wami, Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani.
Bagamoyo. Watu wawili wamepoteza maisha katika ajali iliyohusisha magari mawili kugongana uso kwa uso katika eneo la Daraja la Wami, Kata ya Mandela, Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani.
Ajali hiyo imetokea Juni 6, 2026 saa 5:45 usiku katika Barabara Kuu ya Dar es Salaam–Morogoro ikihusisha gari aina ya Toyota Hilux lililokuwa likitokea Dar es Salaam kuelekea Tanga na lori aina ya Shacman lililokuwa likitokea Tanga kuelekea Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani Salon Morcase kwa vyombo vya habari leo Juni 7, 2026 uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa Toyota Hilux ambaye alijaribu kulipita gari lililokuwa limesimama mbele yake baada ya kupata hitilafu, bila kuchukua tahadhari, hivyo kwenda kugongana uso kwa uso na lori hilo.
Waliofariki dunia ni Hidaya Mgema Mzireni (51), mkazi wa Mtoni Kijichi, Dar es Salaam, aliyefariki papo hapo eneo la tukio, na Juma Ridhiwani Juma (35), dereva wa Toyota Hilux, mkazi wa Dar es Salaam, aliyefariki dunia akiwa anapatiwa matibabu katika Kituo cha Afya Msata.
Miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Msoga wilayani Chalinze huku magari yaliyohusika yakipata uharibifu mkubwa.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani limewataka madereva wote kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani ili kuepusha ajali zinazotokana na uzembe, likisisitiza kuwa hatua kali zitaendelea kuchukuliwa dhidi ya madereva watakaokiuka sheria hizo.