Watumia dawa kuongeza, kupunguza mwili watahadharishwa
Muktasari:
Katika mtindo wa maisha wa sasa si ajabu kukutana na baadhi ya watu wakitumia dawa za kuongeza mwili au kupunguza, kitendo ambacho madaktari wamesema kina hatari kwa afya za wahusika.
Dar es Salaam. Katika mtindo wa maisha wa sasa si ajabu kukutana na baadhi ya watu wakitumia dawa za kuongeza mwili au kupunguza, kitendo ambacho madaktari wamesema kina hatari kwa afya za wahusika.
Mtaalamu wa lishe, Dk Sweetbert Njuu alisema mara nyingi matumizi ya dawa hutakiwa kufanyika kulingana na tatizo husika na kwa kufuata ushauri wa daktari.
Alisema matumizi ya dawa hizo bila ushauri wa daktari huweza kuleta athari kwa mtumiaji kwa kuwa wakati mwingine huwa na madhara tofauti, ikiwamo kuchosha figo na ini.
Dawa hizo maarufu mitandaoni ambazo matangazo yake huambatanishwa na picha za watumiaji zinazowaonyesha kabla na baada ya kutumia zimekuwa zikiwavuta watu wengi zaidi kutaka kujaribu kuzitumia.
Kwa wale wanaotaka kuongezeka mwili, baadhi ya wauzaji huuza dozi kwa Sh100,000 ambazo huwaongezea hamu ya kula huku wale ambao hutaka kupunguza mwili baadhi huharisha.
“Niliharisha, nilihisi kuishiwa nguvu kwa sababu muuzaji alisahau kunipa angalizo la suala hili, lakini nilipungua tumbo kiasi baada ya wiki,” alisema Jenny Michael ambaye alitumia dawa za kupunguza unene.
Alisema dawa hizo ambazo zimetengenezwa kwa miti shamba zilimsaidia kupungua kwa kiasi kabla ya kurudia hali yake ya kawaida miezi kadhaa baadaye.
Shadya Yusuph ambaye sasa anajivunia mwili alionao akisema: “Kwa sababu dawa nilizochagua kutumia ni za kuharisha hivyo nilikuwa nikizitumia siku ambazo nipo nyumbani, niliogopa kutumia zile ambazo hazikuonyeshi namna zinavyofanya kazi.”
Alisema japo haikuwa rahisi kuvumilia lakini alihakikisha hakati tamaa na kuacha kutumia dawa badala yake anapata matokeo aliyokuwa anayahitaji.
“Ilikuwa safari ya matumaini, nilitaka kuhakikisha nafanikisha azma yangu na nipo hapa sasa,” alionyesha kujivunia baada ya kutoka kilogramu 85 hadi 68.
Hata hivyo, Dk Njuu alisema: “Ikiwa mtu hatofanya mabadiliko endelevu atarudi alikotoka, unaweza kutumia dawa za kupunguza unene au kuongeza mwili unapokuja kuacha dozi ukarudia hali yako ya kawaida.
“Kwa sababu mtu anaweza kutumia dawa za kupungua, akishapungua anarudi katika kula chipsi mayai kila siku, lazima atarudia mwili wake wa zamani.”
Alisema mabadiliko anayotakiwa kutafanya mtu ni pamoja na aina ya ulaji na kubadili mtindo mzima wa maisha.
Mtaalamu mwingine wa lishe kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas) Elibariki Kapinda alishauri kabla ya matumizi ya dawa hizo mtu apate ushauri wa daktari.
“Pia, ajue kwa nini anataka kuongeza uzito au kupunguza, je, anataka kufikia kiwango kinachotakiwa kitaalamu, hivyo ni lazima apate ushauri nasaha,” alisema Kapinda.
“Bila kufanya hivyo atajikuta katika tatizo lingine huenda la kupata uzito uliopitiliza au kuwa na uzito usioendana na urefu alionao.”