Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Watumia ugoro kama mbadala wa tendo la ndoa


Muktasari:

  • Wadai unakata hamu ya tendo na wanaweza kuishi muda mrefu kupata ashki.

Dar es Salaam. Kama unadhani ugoro hutumika mdomoni na puani pekee kama sehemu ya kilevi, basi fahamu umeongezewa matumizi mengine kwa wanawake, wanautumia kukata hamu ya tendo la ndoa.

Iwapo utapewa kiburudisho hicho kwa mara ya kwanza, hakika hutothubutu kukigusa kutokana na ukali wake, lakini hivi sasa baadhi ya wanawake mkoani Tabora wanauweka sehemu zao za siri kukata kiu ya tendo la ndoa.

Mwanaidi Nyagumbi, mkazi wa Kijiji cha Kadata wilayani Nzega ni mmoja wa waliohamisha penzi kutoka kwa mumewe kwenda kwenye ugoro.

Mwanaidi alichuku uamuzi huo baada ya kukimbiwa na mumewe na amedumu kwenye kiburudisho hicho kwa takriban miaka minane sasa anayosema hajawahi kushiriki tendo la ndoa.

“Nimekaa miaka nane bila kushiriki tendo la ndoa, faraja yangu ni ugoro. Umekuwa ukinisaidia kumaliza shida zangu. Kwa mwezi naweza kuweka mara mbili, muwasho ninaoupata kisha nanawa na maji ya baridi ndio hunisaidia kukata hamu ya tendo la ndoa,” anaeleza mwanamke huyo.

Mwanamke mwingine ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini anakiri kuutumia ugoro kama kimbilio kutokana na kumkosa mtu wa kuwa baba watoto wake baada ya wazazi wake kuweka pingamizi kwa mwanamume aliyebahatika kuzaa naye mtoto.

“Ugoro ni kitu pekee ambacho siwezi kuacha kukitumia maana ndio mbadala wa mwanamume. Nikiutumia, hamu zote zinaisha na ni miaka mingi nimekuwa nautumia,’’ anasema.

Halima Abbasi anatumia ugoro kama njia ya kujikinga na magonjwa ya zinaa yanayosababishwa na muingiliano wa mwanamume na mwanamke kutokana na baadhi ya wanaume kutotaka kutumia kinga.

“Magonjwa yamekuwa mengi miaka hii, kuliko kuwa na mwanamume ni bora kutumia ugoro ambao ukiuweka sehemu za siri unapata ladha nzuri na tofauti kuliko hata kulala na mwanamume,” anasema Halima.

Halima anasema mwanamke akishatumia ugoro hana haja ya kukutana na mwanamume kwa sababu hamu ya tendo inakata kabisa.

Ally Makelele, mzaliwa wa Kijiji cha Kadata mkoani Tabora anasema tangu miaka ya nyuma wanawake wamekuwa wanatumia ugoro, hasa wajane au waliotengana na waume zao ingawa hufanya hivyo kwa siri.

“Mara nyingi huwa ni siri kubwa, wanaweka akina mama ambao wanatumia ugoro sehemu za siri, huficha kama binti anavyojificha anapoingia kwenye siku zake (akiwa kwenye hedhi) hivyo sio rahisi kumbaini kama anatumia,’’ anasema Makelele.


Ugoro kama kiburudisho

Akizungumza na Mwananchi, Valerina Protas wa Dar es Salaam anasema hutumia ugoro kama kiburudisho kwa kuuweka chini ya fizi na kuunusa. Akifanya hivyo kwa saa mbili, anasema hahitaji kilevi kumaliza siku yake.

“Zamani nilikuwa nakunywa pombe ila nikawa nateseka sana na maumivu ya tumbo, ndipo nilipohamia kwenye ugoro kama mbadala na sasa sipati maumivu yoyote zaidi ya kuburudika,’’ anasema Valerina.

Eriki Philipo (24), makenika eneo la Buguruni jijini Dar es Salaam anasema huvuta ugoro, kwani ndio burudani yake hata anapofanya shughuli haimuathiri mwingine.

“Ukivuta sigara moshi utawasumbua watu wengine, huwezi kufanya kazi huku unavuta ila ugoro unaweka mdomoni na kuendelea na shughuli zako,’’ anasema.

Vilevile, anasema huwa anachanganya ugoro na pombe ili alewe haraka, kwani kwa kufanya hivyo analewa kwa gharama ndogo.


Kauli ya wafanyabiashara

Akizungumza na mwandishi wa gazeti hili, mfanyabiashara ya ugoro katoka Soko la Kariakoo, Joram Mtei anasema inampa faida kubwa, kwani wateja wake wengi ni vijana.

“Mimi bidhaa yangu ina ubora wa hali ya juu, kama ni toleo basi ni la kwanza mbapo wateja wangu ni vijana, wakija kuonja na kukuta bidhaa ni nzuri huambiana na kuniletea wateja wengine, jambo linaloniongezea kipato,’’ anasema.

Mfanyabiashara mwingine sokoni hapo, Shamsia Zuberi anasema hupata faida kubwa kwenye biashara ya ugoro, kwani huuza kwa jumla na rejareja.

“Ndoo kubwa ya lita 20 nanunua kwa Sh40,000, faida napata mpaka Sh20,000 huku rejareja nikiuza Sh300 kwa pakiti koja. Kupitia hii biashara watoto wangu wanapata huduma zote za msingi kama chakula, malazi na nguo. Napata ada ya shule pia,’’ anasema.

Mtaalamu anena

Dk Kelvin Masumbuko wa Hospitali ya Rufaa KCMC anasema kuna vijana na wazee wanaotumia ugoro pasipo kujua athari zake.

“Siku hizi vijana wengi wanatumia ugoro kama kilevi, kwani bei yake ni nafuu mno na upatikanaji wake ni rahisi, kwani wanashindwa kuelewa kuwa ugoro upo kwenye kundi la dawa za kulevya, kwani una kemikali za nicotine na nitrosamines pamoja na kemikali nyingine nyingi,” anasema Dk Masumbuko.

Dk Masumbuko anasema madhara yanayotokana na matumizi ya ugoro kwa binadamu ni kuchubuka kwa midomo, kung’oka meno ya mbele, magonjwa ya mfumo wa hewa na saratani, ikiwamo ya utumbo, ulimi na nyinginezo.

Mbali na madhara hayo, anasema mtumiaji huwa na harufu mbaya ya kinywa kutokana na kemikali zinazopatikana kwenye ugoro.

Kwa kuweka ugoro kwenye fizi, anasema chembechembe zake hupenya na kujikusanya kwenye mapafu na kusabababisha ugonjwa wa kifua kikuu, kwani kiburudisho hicho kina unga mwepesi ambao hupenya kirahisi.

Dk Masumbuko pia aliwaasa akina mama wanaotumia ugoro sehemu za siri kukata hamu ya tendo la ndoa waache, kwani wako kwenye hatari ya kupata saratani ya kizazi.

“Viungo vya uzazi vya mwanamke ni sehemu laini sana ambayo inalindwa na bakteria, sasa unapotumia ugoro wenye kemikali inaviweka viungo hatarini kushambuliwa na magonjwa, ikiwamo kupata saratani ya kizazi,” anasema daktari huyo.

Dk Masumbuko aliwataka vijana, wazee na wanawake wanaotumia ugoro kupata elimu itakayowawezesha kujua madhara yake ili kupunguza uwezekano wa kupata maambukizi ya magonjwa, ikiwamo saratani.


Umuhimu wa tendo

Licha ya uamuzi wa wanawake hao kutumia ugoro kukata hamu ya tendo la ndoa, wataalamu wa afya wanasema lina umuhimu wake katika maisha ya binadamu.

Dk Christopher Mshana wa Hospitali ya Seliani jijini Arusha anazibainisha faida na hasara za binadamu kufanya mapenzi.

Miongoni mwa madhara ya kutofanya tendo la ndoa, Dk Mshana anasema ni mhusika kuwa na msongo wa mawazo, hasa vijana ambao damu inachemka.

“Tendo la ndoa ni tiba kubwa sana kwa mwili wa binadamu. Ikiwa watu watatumia mbinu mbadala ili kutoshiriki tendo hilo inaweza kusababisha msongo wa mawazo na kusahau, kwani akili haichangamki,’’ anasema Dk Mshana.

Mtaalamu huyo anasema madhara mengine ni uwezekano wa kupata tezi dume kwa wanaume. Ili kujiondoa kwenye uwezekano wa kupata maambukizi ya tezi hilo, anasema mwanamume anatakiwa kushiriki tendo la ndoa na kufika kileleni angalau mara 21 kwa mwezi.

“Wanawake wanatakiwa kuelewa kuwa wao wana tiba ya magonjwa mengine, sio lazima watu waende hospitali hivyo wakiamua kutumia ugoro watasababisha shida kwa binadamu wenzao,’’ anasema Dk Mshana.

Mtu mzima kutoshiriki tendo la ndoa kwa muda mrefu, anasema hupunguza uwezo wake wa kufanya kazi kutokana na mwili kuwa mzito. Hata umakini katika kazi, anasema nao hupungua huku mhusika akiwa na tabia ya kudakia mambo yasiyomhusu, hasa kwa wanawake.

Madhara mengine ya kutoshiriki tendo la ndoa kwa muda mrefu, Dk Mshana anasema ni mhusika kupenda kuangalia picha za utupu kupita kiasi.

Aidha, Dk Mshana anasema ikitokea mtu hajafanya mapenzi kwa muda mrefu kuna uwezekano wa kinga za mwili kupungua au kuzifanya kutokuwa na uwezo wa kushambulia bakteria watakaoshambulia mwili muda wowote.

“Mtu asiyefanya tendo la ndoa mara kwa mara ni rahisi kupata maambukizi ya VVU, hasa atakapokutana na mtu aliyeathirika na Ukimwi kwani kinga zake zinakuwa chini sana na haziwezi kupambana na virusi au bakteria wanaoingia mwilini,” anasema.

Kuhusu faida, mtaalamu huyo anasema kufanya mapenzi hupunguza msongo wa mawazo, kwani ni starehe kama zilivyo starehe nyingine ambayo kila mtu anastahili kuipata pindi anapoihitaji.

“Binadamu kwa kawaida huwa na mawazo na wengine hupata msongo wa mawazo kiasi cha kutakiwa kutafuta tiba ili kulimaliza tatizo hilo. Tendo la ndoa ni muhimu sana kwa binadamu,’’ anasema Dk Mshana.

Daktari huyo anasema tendo la ndoa humfanya mtu kuwa na furaha wakati mwingi, hivyo kutumia ugoro ili kukwepa ashki ya kushiriki tendo hilo si sahihi, kwani ugoro humfanya mwanamke awashwe na huenda akapata matatizo katika njia ya kizazi.

Dk Mshana anasisitiza umuhimu wa kuwa na mwenza unayependana naye ambaye mtashiriki tendo la ndoa kwa furaha na kujikuta katika tabasamu hivyo kuwa na afya njema.

Vilevile, anasema kufanya mapenzi husaidia kupunguza maumivu, kwani huchangamsha mwili na kuvisaidia baadhi ya viungo kufanya kazi vizuri.

“Wengine hupata maumivu ya mgongo na kiuno, magonjwa ambayo tiba yake kubwa ni kushiriki tendo la ndoa, kwani hunyoosha viungo na kuvifanya vifanye kazi vizuri na kwa wakati,’’ anasema daktari huyo.

Kushiriki tendo la ndoa pia kunahusishwa na kupata usingizi mnono ambao kwa siku za hivi karibuni umekuwa mtihani kwa watu wengi kutokana na mawazo, ugonjwa au matatizo mengine ya afya.

Ushauri wa wataalamu wa afya wanapendekeza mtu mzima kulala kwa kati ya saa sita mpaka nane ili kuujenga mwili vyema.

“Tendo la ndoa lina faida kubwa katika kumfanya mtu apate usingizi mnono na kuimarisha kinga za mwili. Pia husaidia kumwepusha mtu kupata shinikizo la damu na magonjwa mengine yasiyoambukiza,” anasema Dk Mshana.

Kutokana na faida zake mwilini hata kijamii, Dk Mshana anawashauri wanawake kuacha kutumia ugoro kuzuia hamu ya tendo la ndoa, kwani kila kiungo katika mwili wa binadamu kimewekwa kwa ajili ya kazi maalumu.

“Ugoro huweza kumsababishia mtumiaji athari za kisaikolojia hata kushindwa kufanya shughuli zake hasa kwa wanawake. Tendo la ndoa lina nafasi katika maisha ya binadamu kuliko ugoro,’’ anasema.