Watumishi Mahakama wafundwa mfumo wa kielektroniki

Mkurugenzi wa Menejimenti ya mashauri Mahakama ya Tanzania, Desderi Kamugisha akizungumza na waandishi wa habari wakati wa mafunzo kwa viongozi, watendaji na Maofisa Tehama kutoka kote nchini, leo Jumamosi Machi 18,2023, jijini Arusha. Picha na Janeth Mushi

Muktasari:

  • Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Jaji Joachim Tiganga amesema mahakama kwa kutumia wataalam wake wa ndani imejenga mifumo ya kielektroniki itakayotumika kuratibu shughuli zote za kimahakama ikiwemo usajili na uendeshaji wa mashauri.

Arusha. Katika kuhakikisha wanarahisisha na kuboresha huduma mahakamani, viongozi na watendaji wa mahakama nchini wamepewa mafunzo ya matumizi ya mfumo wa kushughulikia mashauri wa kielektroniki (ECM).

Mafunzo hayo ya siku moja yamefanyika leo Jumamosi Machi 18, 2023 katika Kituo Jumuishi cha utoaji haki Arusha, washiriki walikuwa ni Manaibu Wasajili, Wakurugenzi na wakurugenzi wasaidizi, Mahakimu wakazi wafawidhi ngazi zote, viongozi na maofisa Tehama kutoka Mahakama zote nchini.

Akizungumza katika mafunzo hayo Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Jaji Joachim Tiganga, amesema mahakama kwa kutumia wataalam wake wa ndani imejenga mifumo ya kielektroniki itakayotumika kuratibu shughuli zote za kimahakama na za kiutawala.

"Mifumo hii itarahisisha sana upatikanaji wa taarifa mbalimbali za utendaji wa Mahakama kwa usahihi na kwa wakati, taarifa hizi zinakwena kusaidia kwenye upangaji wa rasilimali watu, usimamizi wa shughuli za kimahakama pamoja na kufanya maamuzi ya haraka pale itakapotakiwa.

Amesema mfumo wa E-CMS sio tena kwa ajili ya makarani bali unakwenda kutumika kwa asilimia 100 kwa majaji na mahakimu wote na lengo la mafunzo ni kujua matumizi yake.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Menejimenti ya mashauri Mahakama ya Tanzania, Desderi Kamugisha, amesema mfumo huo wa kuratibu shughuli za mashauri kuanzia hatua ya ufunguaji na kuwa baada ya kuanza kutumika hatuaruhusu tena ufunguaji wa mashauri kwa njia ya kawaida.

"Safari ya ujenzi wa matumizi ya mfumo ni ndefu, wataalam wa ndani wamekamilisha kazi kubwa tunaenda kupitishwa katika mfumo na yapo mabadiliko makubwa yamefanyika katika mfumo ikiwemo moduli mpya ya mashauri ya familia," amesema.

Naye Msajili Mkuu wa Mahakama, Wilbard Chuma, amesema mahakama mtandao itaongeza ufanisi wa kazi, kutoa na kupata huduma za mahakama kwa urahisi na kuwa hatua hii ya mafunzo inafikisha karibu na mwisho wa safari wa kuwa mahakama mtandao ambao shughuli zake zote zitafanyika kidigitali.

Naye Ofisa Tehema ambaye pia ni mjenzi wa mfumo wa Tehama Mahakama ya Tanzania, Said Hussein amesema mfumo wa sasa umekuja na mabadiliko makubwa yenye lengo la kusaidia upatikanaji wa haki kwa wakati.