Watumishi Mkalama watakiwa kuongeza ubunifu, uwajibikaji kuendana na Dira 2050
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, Hajjat Asia
Muktasari:
- Pia, wametakiwa kuisoma na kuielewa mipango ya maendeleo ya halmashauri hiyo ili waweze kuiwekea mikakati madhubuti ya utekelezaji katika maeneo wanayoyahudumia.
Mkalama. Watumishi wa umma wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama mkoani Singida wametakiwa kuongeza kasi ya utendaji kazi, ubunifu na uwajibikaji ili kuendana na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.
Rai hiyo imetolewa leo Alhamisi, Julai 2, 2026, na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, Hajjat Asia Messos wakati akiwasilisha mafanikio ya mwaka mmoja ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2025/26 katika halmashauri.
“Nitoe rai kwa watumishi wote ndani ya Halmashauri ya Mkalama kuongeza kasi ya utendaji kazi, ubunifu na uwajibikaji ili kuendana na malengo yaliyomo kwenye Dira 2050,” amesema.
Akizungumzia uwezeshaji wa wananchi kiuchumi, Messos amesema katika mwaka wa fedha 2025/26 halmashauri ilitoa mikopo ya asilimia 10 yenye thamani ya Sh500.598 milioni kwa vikundi 52 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Kati ya fedha hizo, vikundi 24 vya wanawake vilipokea Sh208 milioni, vikundi 19 vya vijana vilipokea Sh259.78 milioni huku vikundi tisa vya watu wenye ulemavu vikipokea Sh32.8 milioni.
Mbali na hilo, wanachama 289 wa vikundi vilivyonufaika na mikopo walipatiwa mafunzo ya ujasiriamali na usimamizi wa biashara, wakiwemo wanawake 146, vijana 124 na watu wenye ulemavu 19.
Pia kitengo cha biashara kilifanya ziara katika maduka 560 kwa lengo la kutathmini mwenendo wa biashara na kutoa elimu kwa wafanyabiashara walioonekana kuhitaji maboresho.
Hatua hiyo imechangia kuongezeka kwa idadi ya wawekezaji kutoka sita mwaka 2024/25 hadi tisa kufikia Juni 30, 2026, katika sekta za madini, nishati, kilimo na ufugaji.
Katika sekta ya elimu, amesema shule mpya nne zimejengwa, zikiwemo shule za sekondari za Kinyambuli na Kidarafa pamoja na shule za msingi za Mlumba na Gracemesaki kwa gharama ya Sh1.304 bilioni
Amesema halmashauri imepokea ruzuku ya elimu yenye thamani ya Sh1.692 bilioni, vitabu vya kiada 45,848, vifaa vya Tehama 115 pamoja na walimu wapya 65, kati yao walimu 38 wa shule za sekondari na walimu 27 wa elimu ya awali na msingi.
Katika sekta ya afya, Messos amesema zahanati nne zimejengwa katika vijiji vya Makulo, Yulanson, Kitumbili na Tumuli, huku ujenzi wa Kituo cha Afya Iguguno ukiendelea pamoja na ukarabati wa majengo mbalimbali ya kutolea huduma za afya kwa gharama ya Sh719 milioni.
Kwa sasa halmashauri ina vituo 55 vya kutolea huduma za afya, ambapo 49 ni vya Serikali, vikiwemo hospitali moja, vituo vya afya vitano na zahanati 43, huku vituo sita vinamilikiwa na sekta binafsi.
Katika mwaka wa fedha 2025/26, wazee 5,501 walinufaika na huduma hizo, wakiwemo wanaume 1,762 na wanawake 3,739, huku watoto 15,664 wakipatiwa matibabu bila malipo. Thamani ya huduma zilizotolewa kupitia msamaha wa matibabu ilikuwa Sh104 milioni.