Watumishi wapya zaidi ya 200 wapelekwa Njombe

Waziri wa Nchi Ofisi ya Raia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Innocent Bashungwa akizungumza na wananchi wa Mtwango Halmashauri ya Wilaya ya Njombe wakati Rais Samia Suluhu Hassan aliposimama kusalimiana na wananchi wa eneo hilo akitokea mkoani Njombe kuelekea mkoani Iringa.

Muktasari:

Waziri wa Nchi Ofisi ya Raia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Innocent Bashungwa amesema watumishi zaidi ya 200 wa kada za elimu na afya wamepelekwa katika Mkoa wa Njombe kupitia ajira mpya zilizotolewa na Tamisemi mwezi Julai, 2022.

Dar es Salaam. Waziri wa Nchi Ofisi ya Raia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Innocent Bashungwa amesema watumishi zaidi ya 200 wa kada za elimu na afya wamepelekwa katika Mkoa wa Njombe kupitia ajira mpya zilizotolewa na Tamisemi mwezi Julai, 2022.

Waziri Bashungwa ameyasema hayo leo Alhamisi Agosti 11, 2022 wakati akizungumza na wananchi wa Mtwango wilayani Njombe wakati Rais Samia Suluhu Hassan aliposimama kusalimiana na wananchi wa eneo hilo akitokea mkoani Njombe kuelekea mkoani Iringa.

Amesema “Nimeskia kilio cha wana njombe kupitia Mbunge wenu, Edwin Swale kuhusiana na upungufu wa vifaa tiba pamoja na watumishi katika Halmashauri ya Wilaya hii.

Niwape habari njema wananchi wote wa Mkoa huu kuwa Ofisi ya Rais-Tamisemi tumepokea Sh149 bilioni kwa ajili ya vifaa tiba, magari ya kubebea wagonjwa na magari ya kusimamia shughuli za Afya hivyo kwa hapa Njombe DC niwahakikishie kuwa mtapata vifaa tiba pamoja na magari hayo.

Na kwa ujumla Mkoa wote wa Njombe umepata watumishi zaidi ya 200 wa kada ya Elimu na Afya na kupitia Mkoa watafanya msawazo na kila halmashauri itapata watumishi wa kada hizo kwa ajili ya kutoa huduma bora kwa wananchi” amesema Waziri Bashungwa .