Watumishi watano wafutwa kazi Tanesco kwa madai ya rushwa

Fadhili Chilombe, Meneja Tanesco Mkoa wa Morogoro. Picha na Johnson James

Muktasari:

  • Watumishi hao wanadaiwa walikuwa wakiomba fedha kwa wananchi ili wawaunganishie umeme kwenye nyumba zao.

Morogoro. Shirika la umeme Tanzania (Tanesco) mkoa wa Morogoro limewafuta kazi watumishi wake watano kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya rushwa.

Watumishi hao wanadaiwa walikuwa wakiomba fedha kwa wananchi ili wawaunganishie umeme kwenye nyumba zao.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Aprili 15, 2024, Meneja wa shirika hilo Mkoa wa Morogoro, Fadhili Chilombe amesema wamefikia uamuzi huo baada ya kuweka mitego na kufanikiwa kuwanasa.

“Tumekuwa tukipokea malalamiko kutoka kwa wateja wetu kwamba kuna baadhi ya watumishi wa shirika letu hapa Morogoro wanajihusisha na vitendo vya kuomba rushwa kwa wateja, lakini kwakua tulikua hatuna uthibitisho tulikuwa tunakosa namna ya kuwashughulikia,” amesema meneja huyo.

Amesema juzi walipata taarifa kwamba watumishi hao walienda Mlimba, wilayani Mvomero na kuomba rushwa ya Sh800,000.

“Tukaweka mtego, yule mteja akatoa hizo fedha kwa wale watumishi tukawanasa na wakarudisha fedha kwa mwenye nazo,” amedai Chilombe na kuongeza;

 “Hawa watumishi walikuwa wafanya kazi wa shirika la umeme Tanesco mkoa wa Morogoro kupitia kikundi ambacho walikisajili, kazi yao kubwa ilikuwa ni kwenda kufanya utafiti wa namna ya kuweka umeme kwenye nyumba za wateja, wakawa wanatumia fursa hiyo kuchukua rushwa kwa wateja wetu,” amedai chilombe.

Lakini amesema kazi ya shirika hilo ni pamoja na kupambana na rushwa na itakuwa endelevu, ameonya watumishi wenye tamaa ya kuomba rushwa kwa wateja dawa yao ilishachemka na sasa sheria inafuata mkondo wake.

“Kwa siku za karibuni shirika limeingia kwenye mtafaruku na wananchi na hawatuamini tena, na hilo linatokana na watumishi wachache ambao sio waaminifu, hivyo tutaendelea kuwatoa wote ili shirika letu liwe safi na liwahudumie wananchi inavyotakiwa,”amesema.

Rashid Abas ni mkazi wa Kihonda manispaa ya Morogoro anasema hata yeye aliwahi kuombwa rushwa wakati anakamilisha ujenzi wa nyumba yake iliyoko Bigwa lakini hakutoa.

“Ninawapongeza Tanesco kwa kuwafukuza kazi hao maofisa ambao walikua wanakuja kuomba fedha kwa wananchi, maana hata mimi wakati najenga nyumba yangu iliyoko Bigwa waliwahi kuniomba maji ya kunywa kama Sh150,000 hivi  ili fomu yangu ipitishwe haraka, kufukuzwa kwao kazi labda kutasaidia wengine waliobaki kuogopa mchezo huo,” amesema Mwananchi huyo.

Kwa upande wake Eva Mashauri mkazi wa Tungi Manispaa ya Morogoro ameiambia Mwananchi Digital kuwa tabia hiyo imekuwa sugu kwa baadhi ya watumishi.