Watumishi watatu wasimamishwa kazi kifo cha mjamzito Handeni
Muktasari:
- Kifo cha mama mjamzito aliyekuwa akipatiwa huduma katika Kituo cha Afya Kabuku kilichopo Handeni mkoani Tanga kimesababisha watumishi watatu waliokuwa wakimhudumia kusimamishwa kazi kupisha uchunguzi.
Dar es Salaam. Watumishi watatu wa afya wilayani Handeni mkoani Tanga wamesimamishwa kazi kutokana na kifo cha mjamzito waliyekuwa wakimpatia huduma.
Kupitia taarifa iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Handeni, Omary Mkangama, jana Novemba 13, 2023, watumishi hao wanapisha uchunguzi wa kina kupitia tume huru na bodi za kitaaluma.
Taarifa imesema endapo itabainika kuna uzembe ulifanyika hadi kusababisha kifo hicho basi hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yao.
“Halmashauri imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha Mariam Zahoro Mohamed (39). Kifo hicho kilitokea alfajiri ya Novemba 11, 2023 katika Kituo cha Afya Kabuku ambapo mama huyo alikuwa akipatiwa huduma,” imeeleza taarifa hiyo.
Katika kusisitiza utolewaji wa huduma za afya kwa wananchi Halmashauri imesema kwa kusisitiza kuwa huduma zote za afya kwa makundi maalumu ikiwemo kwa akina mama wajawazito ni bure.
“Halmashauri inaendelea kuhakikisha makundi hayo yanapatiwa huduma za afya kulingana na sheria, taratibu na kanuni za afya.”
Aidha, imesema endapo patakuwa na uvunjifu wowote wa taratibu za utoaji wa huduma hizi, katika vituo vya kutolea huduma ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, wananchi wasisite kutoa taarifa.
Awali, zimekuwepo taarifa katika mitandao ya kijamii zikidai kuwa mama huyo alikosa fedha za upasuaji kiasi cha Sh150,000 kwa ajili ya upasuaji jambo linalodaiwa ndiyo chanzo cha kifo chake.