Fahamu ujauzito usiokuwa na mtoto

Muktasari:

  • Josephine ni miongoni mwa baadhi ya wanawake waliokumbwa na tatizo hili, jambo linalosababisha wengine kupata msongo wa mawazo.

Dar es Salaam. "Baada ya kutafuta mtoto kwa takribani miaka mitatu katika ndoa, Aprili 25, 2023 ilithibitika hospitalini kuwa nimepata ujauzito.

“Ilikuwa ni siku ya furaha sana kwangu, mume wangu na hata familia kwa ujumla, kwani lilikuwa ni tarajio letu la muda mrefu,” anaeleza Josephine Nunda.

Hata hivyo, anasema zilipita wiki kadhaa akaenda kufanya kipimo cha 'ultrasound' kama alivyoshauriwa na daktari na majibu yalionyesha kuwa ni mjamzito wa wiki saba, lakini hakuna maendeleo ya mimba kukua, hivyo akashauri kufanya kipimo hicho baada ya wiki nne.

Hata alipokwenda majibu yalibaki vilevile, hivyo alielezwa kuwa amepata mimba isiyokuwa na kiini au mimba hewa, hivyo alishauriwa kusafishwa.

Josephine anasema haikuwa rahisi kukubaliana na hali hiyo, kwani alishapata matumaini ya kuitwa mama siku zijazo, hivyo ilimchukua muda kukubali hali hiyo.

Josephine ni miongoni mwa baadhi ya wanawake waliokumbwa na tatizo hili, jambo linalosababisha wengine kupata msongo wa mawazo.

Akizungumza na Mwananchi, daktari bingwa wa magonjwa ya kina mama na afya ya uzazi Hospitali ya Bochi, Pantaleo Kavishe anasema tatizo hilo kitaalamu hujulikana kama anembryonic pregnancy au brighten ovum, ambayo ni mimba inayotokea baada ya yai la kike lililorutubishwa kugawanyika na kushindwa kufanyika kwa kiini ipasavyo na hujishikiza kwenye ukuta wa mji wa uzazi na kushindwa kukua.

Dk Kavishe anasema vitu pekee ambavyo huwa vimetengenezeka katika aina hii ya mimba ni mfuko wa uzazi pamoja na placenta.

Anasema bado sababu halisi inayochangia kutokea kwa tatizo hilo haijajulikana, lakini kitaalamu hulihusianisha na kutokea kwa hitilafu katika vinasaba, hususan wakati wa ugawanyikaji na ukuaji wa kiini kinachounda kijusi katika hatua za mwanzo za ujauzito.

“Hakuna sababu maalumu inapelekea kutokea kwa tatizo hilo na humpata mwanamke yeyote. Kwa mujibu wa tafiti zilizofanyika, tatizo hili huchangia asilimia 50 ya mimba zinazoharibika, hasa katika kipindi cha miezi mitatu ya kwanza," anasema.

Anaeleza kuwa mara nyingi hugundulika ndani ya miezi mitatu ya mwanzo ya ujauzito ambayo kitaalamu hujulikana kama "first trimister" baada ya kipimo cha ultrasound.

Dalili zake

Akizungumzia dalili, Dk Kavishe anasema mimba isiyokuwa na kiini au mimba hewa huwa ni zilezile ambazo anazipata mjamzito yeyote kama kutokupata hedhi, kujisikia kichefuchefu na kutapika, uchovu wa mara kwa mara na nyinginezo, hivyo njia pekee ya kugundulika ni kupitia kipimo cha ultrasound.

Matibabu yake yakoje?

Dk Kavishe anasema hatima ya mimba ya aina hiyo huwa ni kutoka yenyewe, hivyo mwanamke anapogundulika amepata changamoto hiyo matibabu hufanyika kwa kuiacha itoke yenyewe. “Anapewa dawa za kufungua mlango wa uzazi na kuchochea utolewaji wa uchafu kutoka kwenye mji wa uzazi kupitia mlango wa uzazi.

"Matibabu mengine hufanyika kwa kusafishwa kwa kutumia vifaa vitakavyoingizwa kwenye mji wa uzazi kwa ajili ya kutoa uchafu kabla ya kusafishwa. Utahitaji kutanuliwa kwa mlango wa uzazi," anasema.

Baada ya mimba isiyo na kiini kuharibika au kutoka, mwanamke huyo anaweza kubeba mimba tena? Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake katika Hospitali ya Salaaman, Abdul Mkeyenge anasema baada ya mimba hiyo kutoka mhusika hushauriwa kusubiri baada ya miezi sita na kuendelea ndipo abebe mimba nyingine.

"Miezi sita hiyo inashauriwa kwa ajili ya kusaidia kuupumzisha mwili na hata mfuko wa uzazi na baadaye anaweza kubeba mimba nyingine na akajifungua salama mtoto mwenye afya njema," anaeleza.

Mtaalamu wa masuala ya saikolojia, Charles Nduku anashauri pamoja na matibabu hayo, mtu aliyepata changamoto hiyo ni vema kupatiwa pia msaada wa kisaikolojia, kwani baadhi yao huwa ni ngumu kukubali kuwa wamepata hali hiyo.