Matatizo ya ujauzito yanayoendana na umri

Muktasari:

Kujua muda mzuri unaofaa kupata mtoto kutakufanya upange mipango ya maisha kwa namna ambayo mambo mengine hayataingiliana na kusababisha baadhi kuvurugwa.

Kwa miaka mingi, wataalamu wengi wa afya ya uzazi bado wanaamini miaka 20 hadi 35 ndio umri sahihi kushika mimba na kujifungua.

Pia, wengi wakifikiri matatizo mengi ya uzazi huongezeka baada ya miaka 35 na huwa zaidi baada ya miaka 40.

Kwa wenzi wawili wanaoishi pamoja, kuchelewa kujifungua huathiri pia wenza wa kiume na mbegu za uzazi za mwanaume hudhorota kila mwaka upitao na watoto wanaotokana na wanaume wazee huwa na hatari zaidi ya kupata matatizo ya akili na matatizo ya chembe za urithi.

 

Kubalehe

Kubalehe ni hatua muhimu kwa binadamu kupitia katika kufikia hatua ya kuweza kuendeleza uzazi. Wastani wa kubalehe na kuvunja ungo kwa wasichana ni miaka 9 hadi 12 kwa sasa, ingawa miaka ya zamani ilikuwa kuanzia miaka 12 hadi 14. Baada ya kubalehe binti anakuwa na uwezo wa kushika mimba, japokuwa uwezekano huongezeka zaidi kati ya miaka 20 hadi 30, baada ya hapa uwezekano huanza kupungua.

Kulingana na The American College of Obstricians & Gynecologists uwezo wa wanawake kujifungua hupungua katika umri wa miaka 32 na hupungua kwa kasi katika umri wa miaka 37.

Uwezo wa wanawake kujifungua hupungua vile umri unaongezeka kwa kuwa wanawake wanapobalehe wanakuwa na idadi kamili ya mayai katika ovari zao. Namba hii hupungua kadiri mwanamke anavyozeeka. Pia, mayai hayazalishwi kiurahisi kwa wanawake wenye umri mkubwa ukilinganisha na mabinti wadogo.

Kulingana na National Institute for Health & Clinical Excellence (NICE) ya Umoja wa madola (UK), kwa wanawake wenye miaka 35, ni wanawake 94 kati ya 100 wanaweza kupata ujauzito wakifanya ngono kwa ukawaida ndani ya miaka 38, ni wanawake 77 kati ya 100 wanaweza kushika ujauzito.

Magonjwa ya njia za uzazi kama Endometriosis na Uterine fibroids yanawatokea zaidi wanawake wenye umri mkubwa. Hali hii husababisha mwanamke kutoshika mimba.

Wanawake wenye umri zaidi ya miaka 35 wanaoamua kushika ujauzito wanakabili hatari ya kupanda kwa shinikizo la damu. Kupanda kwa shinikizo la damu wakati wa ujauzito huathiri kondo la nyuma (placenta) ambalo hutoa lishe kwa kijusi (kitoto kilicho tumboni) hali ambayo huathiri moja kwa moja ukuaji wake.

Hatari ya kupata kisukari kwa wanawake wanaoshika ujauzito wakiwa na miaka 35 na zaidi, pia huongezeka. Kisukari kipindi cha ujauzito huongeza hatari ya kutoka mimba (miscarriage), kujifungua mtoto mwenye kasoro au kujifungua mtoto mkubwa kupita kiasi. Jambo la kushtusha, ni matokeo ya utafiti uliofanyika Sweden, ambapo watafiti wanadai hatari ya matatizo ya uzazi huanza mapema mwanamke anapofikisha miaka 30.

Utafiti uliochapishwa kwenye jarida la magonjwa ya uzazi (Journal of Obstetrics & Gynacology) uliofanywa na watafiti kutoka Taasisi ya Karolinska ya Sweden umegundua katika nchi tajiri duniani wanawake huzaa wakiwa na umri mkubwa kitu kinachosababisha kuongezeka kwa hatari ya kujifungua watoto njiti (Preterm birth), ukuaji hafifu wa vichanga na kujifungua watoto wafu (Stillbirth). Ili kubainisha hatari kati ya makundi tofauti ya umri ya wanawake wanaozaa kwa mara ya kwanza, watafiti walitumia takwimu za vizazi milioni moja katika hospitali za Sweden na Norway kati ya mwaka 1990 na 2010.

Hatari ya kujifungua watoto njiti na kujifungua watoto wafu huongezeka kuanzia miaka ya 30 ingawa toka zamani, miaka 35 ndio ilitambulika kuwa mwanzo wa hatari kwa wanawake kupatwa na hali hiyo.

Kwa kulinganisha kati ya kundi la umri wa miaka 25 hadi 29 na 30 hadi 34, wanawake wa miaka 30 hadi 34 wenye mimba za kwanza walikuwa na hatari ya kujifungua watoto njiti kwenye wiki ya 22 hadi ya 31 ya ujauzito au kujifungua wenye ulemavu wa kuona.

Kikosi cha watafiti kiligundua pia sababu nyingine zinazoweza kuleta matatizo ya uzazi ni uvutaji wa sigara au kuwa mnene kuliko kawaida.

Ulla Waldenstrom, Profesa wa Kitengo cha Afya ya Wanawake na Watoto katika Taasisi ya Karolinska anasema: “Tumeshangazwa na kuongezeka kwa hatari za uzazi katika umri mdogo.”

Profesa Waldenstrom aliendelea: “Wanawake wanaweza ona hatari ni ndogo ila kwa jamii kiujumla kuna idadi kubwa ya matatizo yasiyo ya lazima kwao wanawake wanaozaa baada ya miaka 30. Hivyo nashauri wanawake na wanaume wapewe taarifa shuleni juu ya umuhimu wa umri katika uzazi.”

 

Kukoma hedhi

Wataalamu wa afya wanasema kwamba mwanamke amekoma hedhi anapokosa kupata hedhi kwa miezi 12 mfululizo. Ni wanawake wachache hukoma kupata hedhi ghafla, yaani, wanakosa hedhi mwezi mmoja unakuwa mwisho wa kuipata. Wanawake wengi huanza kipindi hiki wakiwa na umri wa miaka 40 na zaidi, lakini kwa wengine huanza wakiwa wamechelewa wakiwa na miaka 60 au zaidi.

Kutokana na mabadiliko ya kiwango cha homoni kinachotokezwa, huenda mwanamke akakosa hedhi wakati ambao hakutarajia au akavuja damu nyingi isivyo kawaida wakati wa hedhi. Pia huenda mwanamke akashuka moyo, hisia zake zikabadilika na hilo linaweza kumfanya alie mara kwa mara bila sababu na pia asiwe makini na asahau mambo.

Kipindi cha kukoma hedhi huwa tofauti kwa kila mwanamke. Dalili zinaweza kuonekana kipindi hicho ni pamoja na joto la ghafula mwilini, ambalo huenda likafuatiwa na kuhisi baridi. Dalili hizo zinaweza kumfanya mtu akose usingizi na kuishiwa na nguvu. Baadhi ya wanawake hupatwa na joto la ghafla mwilini kwa mwaka mmoja au miaka miwili wakati wa kipindi hicho cha kukoma hedhi.

Wengine hupatwa na hali hiyo kwa miaka mingi na wachache sana husema kwamba wao hupatwa na joto la ghafla mara kwa mara maisha yao yote. Ni busara mtu afanyiwe uchunguzi wa kiafya kabla ya kuamua kwamba joto la ghafla linasababishwa na kukoma kwa hedhi.

 

Makala hii imeandaliwa na Dk Joachim Mabula 0712366660. Maoni au maswali waweza pia kutuma [email protected] au 0713247889