Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Waufuatao matakwa ya mwili ni vigumu kumpendeza Mungu

Bwana Yesu asifiwe! Leo tunatafakari neno la Mungu kutoka Warumi 8:12–17, tukikumbushwa ukweli  kwamba ndani ya Kristo tunakuwa wapya. Hii ni habari njema inayotupa tumaini, lakini pia tunaitwa kuishi maisha yanayompendeza Mungu. Mtume Paulo anaweka wazi tofauti kubwa kati ya kuishi kwa mwili na kuishi kwa Roho, akisema wazi, “Waufuatao mwili hawawezi kumpendeza Mungu.”

Ni muhimu kuelewa maana ya mwili kama Paulo anavyotumia. Hapa haimaanishi mwili wa kawaida wa kibinadamu, bali asili ya dhambi ndani ya mwanadamu.

Ni ile hali ya kuishi bila kumtegemea Mungu, kufuata tamaa binafsi na kufanya uamuzi bila kuongozwa na mapenzi ya Mungu. Maisha ya namna hii huzaa mauti, huleta uadui na Mungu na humfanya mwanadamu kushindwa kabisa kumpendeza Muumba wake.

Kwa upande mwingine, Roho humaanisha Roho Mtakatifu pamoja na maisha ya mtu anayeongozwa naye. Haya ni maisha ya uzima, amani, na utii kwa Mungu. Ndani ya Roho ndipo tunapata nguvu ya kushinda dhambi, kuomba sawasawa na mapenzi ya Mungu, na kuthibitishwa kuwa sisi ni watoto wake. Hapa ndipo tunapoona kwamba Ukristo si tu kufuata sheria au taratibu za kidini, bali ni uhusiano hai na Mungu kupitia Roho wake.

Paulo anatukumbusha kuwa hatuna deni kwa mwili. Hatulazimiki kuishi kwa kufuata tamaa za dhambi.

Kwa nini? Kwa sababu ndani ya Kristo tumefanywa huru. Tulikuwa watumwa wa dhambi, lakini sasa tumekombolewa. Hivyo basi, kurudi tena kuishi kwa mwili ni sawa na kurudi utumwani baada ya kupewa uhuru. Ni kinyume na mapenzi ya Mungu na ni hatari kwa maisha yetu ya kiroho.

Anatuonya pia kwa uzito mkubwa tukiyaishi maisha ya mwili, mwisho wake ni kifo. Lakini tukiyafisha matendo ya mwili kwa Roho, tutakuwa na uzima. Hii inaonesha kuwa maisha ya Kikristo siyo ya kukaa tu, bali ni mapambano ya kila siku.

 Ni vita ya ndani kati ya mwili na Roho. Ushindi hauji kwa nguvu zetu wenyewe, bali kwa msaada wa Roho Mtakatifu anayefanya kazi ndani yetu.

Katika aya hizi pia tunaona jambo la muhimu kwamba tumeasiliwa kuwa watoto wa Mungu.

Hii siyo nafasi ndogo. Katika tamaduni za Kirumi, kuasiliwa kulimaanisha kuacha kabisa maisha ya zamani na kuingia kikamilifu katika familia mpya, ukiwa na haki zote za urithi.

Vivyo hivyo, sisi tulipompokea Kristo, tuliondolewa katika familia ya dhambi na kuingizwa katika familia ya Mungu. Sasa tunaweza kumwita Mungu ‘Baba’, kwa ukaribu na ujasiri.

Huu ni utambulisho mpya. Sisi siyo tena watumwa wa hofu, bali watoto wa Mungu. Roho Mtakatifu anashuhudia ndani yetu kwamba sisi ni wake. Pia kama sisi ni watoto, basi sisi ni warithi, tena warithi wa Mungu pamoja na Kristo. Hii ni neema kubwa isiyostahiliwa. Tulikuwa wenye dhambi, lakini sasa tumefanywa wana wa Mungu.

Hata hivyo, Paulo hatufichi ukweli mmoja muhimu kuwa watoto wa Mungu kunahusisha pia mateso. Kama Kristo aliteswa, nasi tutapitia changamoto. Lakini mateso hayo siyo mwisho kwani ni njia ya kuelekea utukufu.

Hakuna utukufu bila msalaba. Hivyo basi, tusivunjike moyo tunapokutana na magumu, kwa maana Mungu anafanya kazi ndani yetu.

Ndugu zangu, ujumbe wa leo unatuita kujitathmini. Tunaishi kwa kufuata nini mwili au Roho? Mawazo yetu yako wapi? Kumbuka, akili ni uwanja wa vita. Tunapojaza mawazo yetu mambo ya mwili, tunakaribisha mauti. Lakini tunapowaza mambo ya Roho, tunapata uzima na amani.

Ndani ya Kristo tunakuwa viumbe vipya. Maisha ya zamani yanapita na mapya yanaanza. Hii siyo kuboresha tabia tu, bali ni kubadilishwa kabisa. Ni kuwa na mwelekeo mpya, mawazo mapya, na uhusiano mpya na Mungu. Hii ndiyo sababu ya kushangilia katika siku hii kwa sababu Mungu ametufanya wapya.

Sasa basi, sisi kama watoto wa Kristo Yesu tunapaswa kuwa mfano mwema katika jamii zetu.

Tunaitwa kuishi maisha ya haki, upendo na unyenyekevu ili watu waone matendo yetu mema na kumtukuza Mungu. Kwa vitendo vyetu vya kila siku katika familia, kazini, na mahali popote tunapaswa kuonesha tabia ya Kristo ya kusamehe, kusaidia wahitaji, kusema kweli na kuepuka uovu.

Haya ndiyo matunda ya Roho yanayothibitisha kuwa kweli tunaishi ndani ya Kristo.

Vilevile, tunapaswa kusimama imara katika imani na kuwa mashahidi wa Injili.

Dunia inahitaji kuona tofauti kati ya wale wanaoishi kwa mwili na wale wanaoishi kwa Roho. Hivyo, tusione aibu kumkiri Kristo, bali tuishi kwa ujasiri tukiongozwa na Roho Mtakatifu. Kwa kufanya hivyo, tutakuwa nuru na chumvi ya dunia, tukiwavuta wengine wamjue Mungu na kuingia katika familia yake.

Hivyo basi, chagua kuishi kwa Roho. Kataa tamaa za mwili. Kubali uongozi wa Roho Mtakatifu kila siku. Maisha haya mapya ni zawadi, lakini pia ni wajibu. Mungu atusaidie tuishi maisha yanayompendeza yeye. Mungu akubariki uwe uwe baraka katika familia, popote unapoishi watu wamuone Kristo kupitia wewe.


Amina.