Waumini waibua maswali tume ya kuwachunguza masheikh
Muktasari:
- Bakwata, ilitangaza kuwasimamisha viongozi hao watatu Julai 14, mwaka huu kwa tuhuma za kukiuka maadili ya kiuongozi ya baraza hilo.
Dar es Salaam. Uamuzi wa Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata) kuunda tume ya kuwachunguza viongozi wake watatu, akiwamo Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Walid Alhad, umeibua mjadala na hisia tofauti miongoni mwa waumini wa dini hiyo.
Wapo wanaojiuliza sababu za kuundwa kwa tume hiyo, wakati taarifa ya awali ya kusimamishwa kwao, ilieleza kuwa hatua hiyo ilifikiwa baada ya uchunguzi uliofanywa na Baraza la Ulamaa kama chombo cha juu cha uamuzi ndani ya Bakwata.
Wengine wanaona hatua hizo zinaweza kuathiri taswira ya taasisi hiyo na kuibua sintofahamu kwa waumini, hasa pale zinapowahusu viongozi wenye ushawishi mkubwa kwa jamii.
Julai 14 mwaka huu, Bakwata ilitangaza kuwasimamisha Sheikh Walid wa Dar es Salaam, Sheikh Issa Nassor wa Singida na Hassan Kiburwa wa Kigoma, kwa madai ya kukiuka maadili ya kiuongozi ya baraza hilo.
Tume ya uchunguzi
Akisoma taarifa ya kuundwa kwa tume hiyo Julai 21, 2026, Katibu wa Baraza la Ulamaa, Sheikh Hassan Chizenga, amesema Mufti wa Tanzania, Sheikh Aboubakar Zubeir, ameunda tume maalumu kufanya uchunguzi na kuwasilisha ripoti ndani ya mwezi mmoja.
Amewataja Sheikh Shaaban Abdallah kutoka Arusha kuwa mwenyekiti wa tume, huku wajumbe wakiwa Dk Mussa Hans wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Dk Abdallah Tego wa Chuo Kikuu cha Waislamu Morogoro (MUM).
Wengine ni Ummy Kheri, Mwalimu Ally Abdallah ambaye ni Mkurugenzi wa Elimu Bakwata na Khamis Kalimwage kutoka Kamati ya utatuzi wa migogoro ya misikiti na madrasa.
Sheikh Chizenga, amewataka watu wenye taarifa zinazohusiana na suala hilo, kuziwasilisha kwa tume na kutoa ushirikiano utakaowezesha kupatikana kwa uamuzi wa haki kwa pande zote.
Waumini waibua maswali
Akizungumzia hatua hiyo, Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda, amesema kuundwa kwa tume hiyo, kumeibua maswali kuhusu mantiki ya mchakato unaoendelea.
Amesema viongozi hao walielezwa kuwa walisimamishwa baada ya kuchunguzwa na Baraza la Ulamaa, hivyo kuundwa kwa tume nyingine kunazua swali la chombo hicho kinakwenda kuchunguza jambo gani.
“Walitangaza kuwa uchunguzi ulifanyika na ndipo uamuzi wa kusimamisha viongozi hao ukachukuliwa. Sasa tume hii mpya inachunguza nini?” amehoji.
Sheikh Ponda, amesema mijadala ya aina hiyo haiwasaidii waumini na badala yake huongeza sintofahamu wakati jamii ikihitaji kujadili zaidi maendeleo na ustawi wa kiuchumi.
Hata hivyo, amesisitiza kuwa Bakwata ni taasisi inayojisimamia na uamuzi wake ni sehemu ya masuala yake ya ndani.
Mjadala huo umehamia pia kwenye mitandao ya kijamii, huku baadhi ya waumini wakionyesha kutoridhishwa na hatua zilizochukuliwa.
Katika ukurasa wa Instagram, Madame-chioma9, aliandika kuwa taasisi hiyo ilipaswa kufanya uchunguzi wa kina kabla ya kuchukua hatua za kinidhamu.
“Mlikimbilia kuhukumu kabla ya kuchunguza, muacheni Sheikh aendelee na maisha yake...’’ameandika.
Kwa upande wake, jiwa_tz alihoji sababu ya viongozi wanaoonekana kuwa na ushawishi mkubwa, kulengwa zaidi na hatua hizo, huku akitaka Bakwata kuwa makini katika kushughulikia masuala yanayogusa waumini wengi.
“Uchunguzi huo iwe kwanini uwe kwa wale wanaoonekana wana ushawishi mkubwa na jamiii imewakubali? tunawataka muwe serious (makini) na mambo ya Waislamu,” ameandika.
Mtumiaji mwingine, selamanimluwale75, alionya dhidi ya hatua zinazoweza kuongeza mgawanyiko kati ya waumini na viongozi wa taasisi hiyo.
“Mrudisheni huyo Sheikh Walid, hiyo tume kama itatenda haki Walid atarudi kama haitendi haki watajenga chuki kati ya Bakwata na Waislam. Hili bomu mnalitengeneza…,” ameandika.
Nguvu ya ushawishi
Muumini wa dini hiyo, Ibrahim Hassan, amesema kinachoshuhudiwa sasa katika sakata la masheikh wa Bakwata, kinaonyesha namna baadhi ya viongozi wa dini wanavyokuwa na ushawishi mkubwa kwa waumini wao.
Amesema hali hiyo inafanana kwa kiasi fulani na mjadala ulioibuka wakati Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Kijitonyama, Eliona Kimaro, aliposimamishwa na kusababisha hisia kali miongoni mwa waumini wake.
Amesema matukio hayo yanaonyesha kuwa taasisi za dini zinapaswa kutathmini kwa kina athari za uamuzi kwa waumini, hasa unapohusu viongozi wanaokubalika na kupata uungwaji mkono mkubwa kutoka kwa jamii.
“Yanayoendelea kuhusu Sheikh Walid yanaonyesha namna baadhi ya viongozi wanavyokubalika kwa waumini wao. Hivyo, uamuzi wa aina hii unahitaji umakini mkubwa ili kuepusha migawanyiko isiyo ya lazima,” amesema.
Alipotafutwa kuzungumzia maoni hayo ya waumini, Sheikh Chizenga alijibu ni vigumu kusema chochote hadi atakapopata idhini ya Mufti kufanya hivyo.
“Nitumie maswali yako niyawasilishe kuomba ridhaa, Mufti akiniruhusu nitakujibu,” amesema.
Hata alipotumiwa maswali hayo tangu saa 5:31 asubuhi hadi saa 9:52 alasiri hakuwa amejibu.