Wawakilishi wakunwa na uwekezaji gesi Mtwara

Muktasari:

  • Kiasi kikubwa cha gesi asilia kinatajwa kuwepo kwenye kina kirefu cha bahari huku futi za ujazo 57.54  zikiwa tayari zimeshagundulika nchini.

Mtwara. Zaidi ya futi za ujazo 57.54 za gesi asilia zimeshagundulika nchini huku kiwango kikubwa kikiwa kwenye kina cha bahari ambapo bado hakijachimbwa.

Hayo yameelezwa na Mjilojia wa Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (Pura)  Mussa Itombo  wakati wa ziara ya siku moja ya Kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar, katika miundombinu ya gesi asilia Mnazibay pamoja na kiwanda cha kuchakata gesi asilia Madimba.

Amesema, “unajua mpaka sasa gesi inayotumika Songosongo na Mnazibay ni kwenye maeneo ya nchi kavu, bado kiasi kingi cha gesi asilia kipo kwenye kina kirefu cha bahari.”

Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mwanaasha Khamis Juma amesema lengo la ziara hiyo ni kujifunza kuhusu miundombinu ya gesi.

 “Tumekuja kujifunza kuona miundombinu ya gesi asilia kwa sababu sasa tunayo mamlaka hiyo ambayo imeanzishwa ndio maana tunashirikiana ili kuona namna gani wenzetu wanazalisha gesi, kiufupi tumefurahishwa na tumejifunza vitu vingi ambapo  tumeona wenzetu walivyopiga hatua.”

“Sisi kama wajumbe na wawakilishi wa baraza tunaenda kuishauri Serikali huu ni uwekezaji mkubwa tunaamini kuwa Zanzibar  tukipata gesi itatuwezesha kwenda mbali, ambapo tunaamini kuwa tutanufaika na kwa wananchi italeta tija” amesema Juma.

Mjumbe wa kamati hiyo,  Yusuph Hassan Iddi   amesema kuwa kwenye mafuta na gesi kuna uwekezaji mkubwa umefanyika. 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mwendeshaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Utafutaji wa Uchimbaji wa Mafuta na Gesi asilia Zanzibar, Adam Abdulla Makame  amesema kuwa kwa sasa wametangaza kufungua maeneo mapya na wanakaribisha wawekezaji.