Wawili kortini wakituhumiwa kumbaka mama na wanawe

Washitakiwa Rashid Selemeni na Ramia Juma wakitoka kusikiliza mashtaka yao katika Mahakama ya Wilaya Handeni leo Aprili 12, 2024. Picha na Rajabu Athumani

Muktasari:

  • Watuhumiwa hao wanadaiwa kuwabakawakati wakiandaa futari nyumbani kwao, kwa kuwatisha na kuwataka wavue nguo.

Handeni. Wakazi wawili wa kata ya Kabuku Ndani, wilaya ya Handeni mkoani Tanga, wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya Handeni na kusomewa mashtaka matatu ya kubaka kwa kikundi mama na watoto wawili.

Watuhumiwa hao ni Rashid Selemeni (42) na Ramia Juma (48) wanaidaiwa kutenda makossa hayo Machi 18, 2024 katika kijiji cha Kwaludege kilichopo kata ya Kabuku Ndani wilayani hapa.

Akiwasomea mashtaka leo Aprili 12, 2024, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Nzagalila Kikwelele, alidai washtakiwa hao walivamia nyumbani kwa mwanamke huyo na kutekeleza uhalifu huo.

Ametaja makosa yao kuwa ni ubakaji wa kikundi kinyume na kifungu cha 130(1) na 131(A)(1) (2) vya kanuni ya adhabu ya makosa ya jinai, sura ya 16 marejeo ya mwaka 2022, kosa linalowahusu washtakiwa wote wawili.

Kosa la pili ni kubaka kinyume na kifungu cha 130(1) (2)(a) (b) na 131(1) vya kanuni ya adhabu ya makosa ya jinai, sura ya 16 marejeo ya mwaka 2022, linalomkabili mshtakiwa wa kwanza, Rashid Seleman akidaiwa alitumia nguvu na vitisho katika kutekeleza jambo hilo.

Kosa la tatu pia ni kubaka kinyume na kifungu cha 130(1)(2)(e) na 131(1) cha kanuni ya adhabu ya makosa ya jinai sura ya 16 marejeo ya mwaka 2022, ambalo linamuhusu mshtakiwa wa pili, Ramia Juma ambaye ameshtakiwa kwa kufanya kitendo cha ubakaji kwa  msichana aliye chini ya miaka 18.

Baada ya mwendesha mashtaka kuwasomea makosa hayo, washtakiwa wamekanusha tuhuma hizo na mwendesha mashtaka ameendelea na hoja za awali.

Katika hoja hizo za awali, mwendesha mashtaka Kikwelele amedai washtakiwa waliwafanyia wanawake hao kitendo cha ubakaji wakati wakiandaa futari kwa kuwatisha na kuwataka wavue nguo na walianza kwa mama yao na baadaye watoto wake wawili.

Ameeleza tukio hilo linadaiwa kufanyika sehemu ya wazi (sebuleni), huku watoto wote wakiona kilichokuwa kinaendelea huko kijijini kwao Kwaludege.

Baada ya kusikiliza maelezo hayo, Hakimu Veronica Siao amesema washtakiwa hao wana haki ya kupata dhamana na kila mmoja anatakiwa kudhaminiwa na watu wawili kwa udhamini wa Sh2 milioni.

Mshtakiwa Rashid Selemeni amekosa mdhamini, hivyo kurudishwa rumande na Ramia Juma amedhaminiwam hivyo kuachiwa kwa dhamana. Kesi itatajwa April 15, 2024.