Wazazi Dar wapatiwa mafunzo ya afya ya uzazi

Mratibu wa Huduma ya Afya na Uzazi wa Mtoto Mkoa wa Dar es Salaam, Agnes Mgaya.
Muktasari:
- Akina mama wenye watoto chini ya miezi sita katika Jiji la Dar es Salaam wamepatiwa mafunzo na elimu ya kuboresha huduma za afya ya uzazi na mtoto ili kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.
Dar es Salaam. Katika jitihada za kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi nchini, akina mama wenye watoto wenye umri chini ya miezi sita wamepewa mafunzo na elimu ya kutambua viashiria vya utoaji huduma bora za afya kwa mama na mtoto.
Mafunzo hayo yalitolewa kwa akina mama 50 kutoka wilaya nne za mkoa wa Dar es Salaam, zikiwemo Temeke, Kinondoni, Ubungo, na Ilala, kupitia mradi wa USAID Afya Yangu. Hafla hiyo ilidhaminiwa kwa kushirikiana na Ofisi ya Mganga wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya mafunzo hayo, Ofisa Mabadiliko ya Tabia wa Mradi huo, Patricia Mkude, alisema walijiunga na mkoa wa Dar es Salaam kutoa mafunzo hayo kupitia jukwaa la Naweza, linalojumuisha kifurushi cha uzazi na malezi ya watoto chini ya miaka mitano. Elimu hiyo inalenga kuunga mkono juhudi za serikali za kuboresha afya na ustawi wa jumla wa watoto kuanzia kuzaliwa hadi miaka mitano, kwa kuzingatia siku 1,000 za mwanzo.
"Malengo yetu ni kuwawezesha wazazi na walezi kupata taarifa, motisha, ujuzi, na msaada kutoka kwa mama rika na jamii, ili kufuata na kudumisha tabia chanya za kiafya zinazolenga kulinda afya na ustawi wa jumla wa mtoto," amesema Mkude.
Mratibu wa Huduma ya Afya ya Uzazi na Mtoto wa Mkoa wa Dar es Salaam, Agnes Mgaya, alisema walilenga akina mama wenye watoto chini ya miezi sita na wenye uzazi wa kwanza au wa pili, kwa kuwa bado watakuwa na muendelezo wa kuzaa.
"Mafunzo haya yalilenga kukumbusha viashiria muhimu katika utoaji huduma bora za afya kwa mama na mtoto, ili kupata elimu inayoweza kusaidia kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi," amesema Mgaya.
Aidha, Mgaya alisisitiza umuhimu wa kunyonyesha maziwa ya mama pekee ndani ya miezi sita ya mwanzo bila kumpa mtoto vyakula vya ziada. Pia aliwataka akina mama kutumia njia za kisasa za afya ya uzazi baada ya kujifungua ili kuzuia kupata mimba nyingine ndani ya miaka miwili, na hivyo kuruhusu mtoto kukua na kuwa na afya bora.
Akina mama hao pia walipatiwa elimu kuhusu umuhimu wa kuhakikisha mtoto mchanga anapata chanjo zote zinazohitajika na kumpeleka mtoto katika kituo cha afya mara tu anapogundua dalili za ugonjwa.
Sozy Edward, mkazi wa Kinyerezi, Ilala, aliyeshiriki mafunzo hayo, alisema amejifunza umuhimu wa chanjo ya saratani ya shingo ya kizazi na umuhimu wa kunyonyesha mtoto ndani ya muda wa nusu saa baada ya kujifungua.
Giveness Abbas kutoka Keko, Temeke, amesema amepata elimu ya lishe bora kwa mtoto na namna ya kujenga afya yake kupitia mafunzo hayo.