Wazazi kitanzini mmonyoko wa maadili kwa watoto

Mwanasaikolojia mbobevu, Padre Leons Maziku (wa kwanza kushoto) akifafanua jambo wakati wa Mdahalo wa Maadili na Mmonyoko wa Maadili ulioandaliwa na Dawati la Jinsia la Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (Saut) Mwanza. Wengine ni Mhadhiri wa Sheria Saut, Mwasi Mbegu (wa pili kushoto), Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Mwanza, Mary Mlade na Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Mwanza, Janeth Shishila (wa kwanza kulia). Picha na Mgongo Kaitira.
Mwanza. Mwanasaikolojia mbobevu, Padre Leons Maziku amewatupia lawama wazazi na walezi kwa kushindwa kutimiza wajibu na jukumu la malezi ya watoto wao.
Akizungumza leo Jumanne Aprili 25, 2023 wakati wa mdahalo maalum kujadili mmonyoko wa maadili ulioandaliwa na Dawati la Jinsia la Chuo cha Mtakatifu Augustino Padre Maziku amesema baadhi ya wazazi na walezi wameacha jukumu la malezi na makuzi ya watoto kwa wasaidizi na wafanyakazi wa majumbani.
Huku akisikilizwa kwa makini na wanazuoni na wanafunzi zaidi ya 400 kutoka Bewa (Kampasi) Kuu ya Saut Mwanza waliohudhuria mdahalo huo, Mwanasaikolojia huyo amepongeza uamuzi wa Serikali kuzuia wanafunzi wanaosoma darasa la nne kurudi chini kuishi bwenini akisema utawezesha watoto kuishi karibu na familia zao.
Padre Maziku ambaye pia ni Mhadhiri Chuo cha Saut ametaja faida za watoto kuwa karibu na wazazi wangali wadogo kuhisi kuwa salama, kujiamini, kukua na kuimarika kimwili na kiakili.
"Ndiyo maana tunapofungisha ndoa huwa tunawauliza, wanandoa iwapo wako tayari kuwapokea kwa mapendo watoto watakaojaaliwa na Mungu. Inashangaza kuona sasa wazazi wametelekeza jukumu la malezi ya watoto wao kwa wasaidizi wa kazi za nyumbani," amesema Padre Maziku
Kaimu Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Mwanza, Janeth Shishila amewashauri wazazi kuwalinda watoto wao dhidi ya matatizo wanayoweza kukumbana nayo wakitumia vibaya maendeleo ya teknolojia.
"Hatuwezi kuikwepa Teknolojia, bali tunatakiwa kukimbizana nayo huku tukiwafundisha watoto wetu kuwa na utashi wa kutambua mambo ya kuchukua na kupuuza wanapotumia teknolojia ikiwemo mitandao ya kijamii. Tuwaongezee watoto ulinzi na udhibiti," amesema Shishila
Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Mwanza, Mary Mlade amewahimiza wazazi, hasa wanawake kudhibiti nyendo zao wakati wa ujauzito kwa sababu matendo ya mama wakati wa ujauzito yanaweza kuwa na athari katika tabia ya mtoto atakapozaliwa.
Mwanafunzi wa Shahada ya Sheria Saut, Festo Chachali amewataka wazazi kuacha kuitupia lawama maendeleo ya teknolojia kuhusu suala la mmonyoko wa maadili kwa watoto, badala yake watimize wajibu katika makuzi na malezi.
"Tuna nafasi ya kurejea tatizo la mmomonyoko wa maadili kwa wazazi ma walezi kuangalia walipojikwaa na kujirekebisha badala ya kusingizia tekonolojia. Kila mzazi atomize wajibu kuwalea na kuwalinda watoto kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo,” amesema Festo