Wazazi wacharuka watoto kurudishwa nyumbani kisa michango
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kikelelwa Kata ya Tarakea Motamburu Wilaya ya Rombo. Picha na Janeth Joseph
Muktasari:
Wananchi wa Kata ya Tarakea Motamburu, Wilaya ya Rombo Kilimanjaro wamepatwa na sintofahamu baada ya watoto wao kufukuzwa shule kwasababu ya kutokamilisha baadhi ya michango.
Rombo. Wananchi wa kata ya Tarakea Motamburu Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro wameiomba Serikali kuingilia kati suala la baadhi ya shule kukataa kuwaandikisha watoto darasa la awali wanaposhindwa kuchangia baadhi ya michango ya shule.
Wakizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Kikelelwa, wananchi hao wamesema kuwa baadhi ya walimu wamekuwa wakikataa kuwaandikisha watoto wao madara ya awali wanapopungukiwa kiasi kidogo cha fedha.
Consesta Mushi ambaye ni mkazi wa kijiji cha Kikelelwa amesema yeye ni miongoni mwa wazazi ambao watoto wake watatu walikataliwa kuandikishwa shule kwa kupungukiwa na kiasi kidogo cha fedha hali ambayo alisema ilimfedhehesha sana kama mzazi.
"Wananchi tunateseka sana, ukimwandikisha mtoto shule ya awali unatakiwa uende na Sh25,000 na darasa la kwanza ni Sh28,500 ukipungukiwa na Sh1000 mtoto haandikishwi shule,
Nilipungukiwa na Sh5000 nikarudshwa nyumbani na mtoto wangu na ukiangalia ile shule haina walimu na wanadaiwa kuwa ni kutokana na upungufu wa walimu"
"Kwa kweli wazazi tunateseka tena sana, Waziri wa Elimu tunaomba utusaidie katika hili maana wazazi kweli tunapata shida, nina watoto watatu na nawaza nawalipiaje shule maana nimeshindwa, tusaidie baba,"
Pamoja na mambo mengine, suala la uhaba wa walimu wa masomo ya sayansi katika baadhi ya maeneo wilayani humo limeelezwa kuwa ni changamoto hali ambayo inawafanya baadhi ya wakuu wa shule kuwachangisha wazazi fedha kwa ajili ya walimu wa masomo ya ziada (tuition)
Akizungumzia changamoto hiyo, Mkuu wa shule ya Sekondari ya Motamburu, Saidi Mkindi amesema shule hiyo inakabiliwa na uhaba mkubwa wa walimu wa masomo ya sayansi hali ambayo inawalazimu kuwatafuta walimu wa ziada wa masomo hayo na kupelekea kuwachangisha wazazi fedha kwa ajili ya kuwalipa walimu hao.
"Shule nzima ina mwalimu mmoja tu mwajiriwa wa somo la hesabu, Physics, wazazi wanaingia gharama kubwa kuchangia masomo ya ziada (tutuion) na michango mingine kwa ajili ya kuwalipa walimu wa masomo ya ziada na wakati walimu wapo mitaani wamemaliza vyuo vikuu hawana ajira,"
"Tunaomba utupelekee ujumbe huu kwa Rais wetu wa Tanzania ili aweze kuajiri walimu wetu wa masomo haya ili watoto wetu waweze kusoma vizuri na kufanya vizuri katika masomo yao ya sayansi,"amesema mwalimu Mkindi.
Kwa upande wake Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema suala la mzazi kushindwa kutoa michango halimfanyi mwanafunzi kukataliwa kuandikishwa shule kwani msimamo wa Serikali ni elimu bure hadi kidato cha nne.
"Hakuna kitu kama hicho ila viongozi mliopo katika maeneo haya naomba msimamie hilo kwasababu ni msimamo wa Serikali, kuna maeneo wazazi wanakaa na kukubaliana mambo ya kufanya sasa kama kuna mtu hawezi kulipa bado lazima mtoto aende shule,"
"Ila naomba kama mmekubaliana kwa kitu fulani pengine kuna uhaba wa walimu na mnataka kuchangia yazungumzwe kwa walimu maana hilo sio sharti la Serikali, elimu ni bure mpaka "form Four" huo ni msimamo wa Serikali yetu,"amesema Waziri Mkenda na kuongeza
"Ila wazazi wakaamua kukaa na kusema wachangie chakula cha mchana tuangalie utekelezaji na sio kumzuia mtoto kwenda shule,"