Waziri atoa siku saba kwa timu kuchunguza mabadiliko mto Mara

Muktasari:

  • Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Suleiman Jaffo leo Jumamosi Machi 12, 2022 ametangaza timu ya watu 11 itakayochunguza chanzo cha mabadiliko katika mto Mara yaliyopelekea maji kubadilika kuwa meusi huku viumbe hai wakiwepo samaki kufa.

  


Musoma. Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Suleiman Jaffo leo Jumamosi Machi 12, 2022 ametangaza timu ya watu 11 itakayochunguza chanzo cha mabadiliko katika mto Mara yaliyopelekea maji kubadilika kuwa meusi huku viumbe hai wakiwepo samaki kufa.

Jaffo ametoa siku saba kukamilisha kazi hiyo kwa timu hiyo inayoongwa na mwenyekiti Profesa Samuel Mayere ambaye ni mhandisi katika idara ya kemia na madini Chuo Kikuu Dar es Salaam

Waziri amemtaja katibu wa kamati hiyo kuwa ni Mkurugenzi wa Mkuu wa Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (Nemc), Dk Samuel Gwamaka na wajumbe wengine wakiwa ni Dk Charles Kasanzu kutoka Idara ya Jiolojia Chuo Kikuu cha Dar es salaam.

Wajumbe wengine ni Mkurugenzi wa Udhibiti Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Daniel Nio, Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la ziwa Victoria, Renatus Shinu, Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Samaki (Tafiri) kanda ya ziwa, Baraka Sekadende na mjumbe mmoja kutoka ofsi ya Rais.

Wengine ni Yusufu Kuwaya kutoka ofisi ya mkuu wa mkoa wa Mara na mkurugenzi msaidizi masuala ya Baionuwai kutoka ofisi ya makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Faraja Ngeregeza, Mkuu wa idara ya kemia Chuo kikuu cha Dar es salaam Dk Kessy Kiruya na Dk Nedovuto Mollel kutoka mamlaka ya afya ya mimea na usimamizi wa viatilifu.

Ameitaka kamati hiyo kutoa mapendekezo ya hatua zipi zichukuliwe zitakazosaidia kukabiliana na uharibifu.

" Hii kamati ina watu mchanganyiko kutoka idara tofauti lengo tupate majawabu sahihi ili tujue nini kifanyike kwa sababu huwezi kutoa tiba wakati haujajua unaugua ugonjwa gani" amesema