Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Waziri Gwajima asisitiza elimu dhidi ya ukatili wa kijinsia

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na wenye Mahitaji Maalumu, Dk Dorothy Gwajima (katikati), akisikiliza mada zilizokuwa zikitolewa kwenye mkutano mkuu wa 21 wa Mewata .

Muktasari:

Waziri Gwajima amesema hayo alipokuwa akifungua mkutano mkuu wa 21 wa Chama cha Madaktari Wanawake Tanzania (Mewata) unaofanyika kila mwaka

Dar es Salaam. Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na wenye Mahitaji Maalumu, Dk Dorothy Gwajima amewataka wanachama wa Chama cha Madaktari Wanawake Tanzania (Mewata),  kutoa elimu kwa jamii kuhusu masuala ya ukatili wa kijinsia hasa ukeketaji kwa watoto.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana Jumapili Aprili, 21 2024, alipokuwa akifungua mkutano mkuu wa 21 wa Mewata unaofanyika kila mwaka, Dk Gwajima amesema jambo la muhimu hivi sasa ni kuwafikia wananchi hususan wa vijijini, ambao idadi kubwa inaonyesha wengi wao hawapati elimu ya ukatili wa kijinsia.

Amesema zipo sehemu hapa nchini wanajamii wanaendelea kuwakeketa watoto wa kike bila kujali madhara wanayoweza kuwapata mabinti hao na kuwasababisha kupoteza uhai na hata kukatisha ndoto zao.

“Mewata jukumu lenu kubwa ni kuangalia namna gani ya kuweza kuifikia jamii kwa kutoa elimu mbalimbali kuhusu ukatili wa kijinsia, lakini niwaombe kuendelea kutoa ushirikiano serikalini kusaidia suala afya ya mama na watoto inakuwa salama wakati wote.

“Tuendelee kuwa na mifumo ya kifikra itakayosaidia kutatua changamoto zinazojitokeza katika jamii, wapo ambao wanauana na ndoa kuvunjia lakini mila kandamizi, ukeketaji kwa watoto bado upo hapa nchini. Mewata ni jukumu lenu kuangalia namna nzuri ya kuifikia jamii na kutoa elimu,” amesema.

Akitaja takwimu za jumla kupitia Ofisi ya Takwimu ya Utafiti wa Demografia na Afya (2015-2016), amesema zinaonesha asilimia 40 ya wanawake wenye umri wa miaka kati ya 15-49 wamefanyiwa ukatili wa kimwili na asilimia 17 ya wanawake wamefanyiwa ukatili wa kijinsia.

Amesema jamii bado inakabiliwa na changamoto ya mila na desturi kandamizi zinazowazuia wanawake na watoto kufikia ndoto zao na kutoa mchango wao katika ustawi wa jamii na Taifa kwa ujumla.

Mbali na hayo, Dk Gwajima amewasihi wanachama wa chama hicho kuacha kuwa na  aibu mara wanapopata migogoro yoyote itakayowasilishwa na kuwa wawazi kuwaambia tatizo ni nini ili kusaidia kulitatua mapema.

“Tusione aibu wala kuficha tatizo unapoliona, tunapaswa kusema ukweli utakaosaidia kutatua migogoro itakayojitokeza, ni matumaini yangu katika majukumu yetu ya kazi tutatanguliza kusema ukweli bila kujali tatizo lolote, tuingie mkataba wa kuangalia namna nzuri ya kuisaidia jamii,” amesema.

Kwa upande wake, Rais wa Mewata, Dk Zaitun Bhokhary amempongeza Waziri Gwajima kwa ushirikiano alioutoa na kuahidi kuwa watatembelea ofisi ya waziri huyo na kuhakikisha wanaingia mkataba utaokasaidia afya ya mama na watoto.

Ametaja kaulimbiu ya mkutano huo kuwa ni: “Tushirikiane kutoa kipaumbele kwa afya ya wanawake na watoto kwa ustawi wa jamii,” ikiwa na lengo la kukuza mshikamano na uhusiano katika kuhimiza na kukuza utafiti wa kuboresha huduma ya afya kwa wanawake na watoto.

Naye, Makamu wa Rais Mewata, Dk Marry Mwanyika, amesema wapo tayari kutoa elimu kwa jamii na kuangalia namna nzuri ya kuondoa masuala ya ukatili wa kijinsia unaoendelea katika baadhi ya sehemu nchini.

Mratibu wa Kamati ya Haki za afya ya uzazi kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi (Muhas), Emmanuela Maira  amesema hivi karibuni wataandaa jarida litakalobeba maudhui mbalimbali ya kuielimisha jamii dhidi ya masuala ya ukatili wa kijinsia.