Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Waziri Homera aipa kongole Korea kuandaa kikao cha urithi wa dunia

Muktasari:

  • Tanzania itaendelea kushirikiana kikamilifu na Unesco ili kuhakikisha malengo na misingi ya Mkataba wa Urithi wa Dunia wa mwaka 1972 inaendelezwa na kutekelezwa kwa ufanisi

Dar es Salaam. Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Juma Zuberi Homera, ameipongeza Jamhuri ya Korea kwa kufanikiwa kuwa mwenyeji wa Kikao cha 48 cha Kamati ya Urithi wa Dunia ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco), kinachoendelea katika Jiji la Busan kuanzia jana Jumapili Julai 19 hadi 29, 2026.

Akichangia katika mjadala wa kikao hicho leo Jumatatu, Julai 20, 2026, Dk Homera ameishukuru Unesco kupitia Kituo cha Urithi wa Dunia kwa kuendelea kutoa usaidizi wa kitaalamu kwa nchi za Afrika, ikiwamo Tanzania, licha ya changamoto za kifedha zinazoikabili taasisi hiyo.

Amesema Tanzania inathamini mchango wake katika kuhifadhi na kusimamia maeneo ya urithi wa dunia, huku akisisitiza kuwa nchi itaendelea kushirikiana kwa karibu na shirika hilo katika kipindi chake cha uanachama wa Kamati ya Urithi wa Dunia.

“Tanzania itaendelea kushirikiana kikamilifu na UNESCO ili kuhakikisha malengo na misingi ya Mkataba wa Urithi wa Dunia wa mwaka 1972 inaendelezwa na kutekelezwa kwa ufanisi,” amesema.

Katika mjadala kuhusu ushirikishwaji wa watu wa asili katika utekelezaji wa Mkataba wa Urithi wa Dunia wa mwaka 1972, Dk Homera amesema Tanzania inatambua uwepo wa Azimio la Umoja wa Mataifa la mwaka 2007 kuhusu Haki za Watu wa Asili (UNDRIP), lakini akabainisha kuwa azimio hilo halina nguvu ya kisheria inayozifunga nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa.

Pia ameeleza kuwa Mkataba wa Shirika la Kazi Duniani (ILO Convention No. 169), unaohusu haki za watu wa asili na wa makabila, umeridhiwa na idadi ndogo ya nchi duniani.

Kutokana na hali hiyo, Tanzania imeomba ufafanuzi kuhusu msingi wa kisheria unaotumiwa na Unesco kupendekeza ushirikishwaji wa watu wa asili katika utekelezaji wa Mkataba wa Urithi wa Dunia wa mwaka 1972, hususan katika mazingira ambayo hakuna wajibu wa kisheria unaotokana na vyombo husika vya kimataifa.

Kikao hicho cha Kamati ya Urithi wa Dunia kinaendelea hadi Julai 29, 2026 na kinawakutanisha wajumbe kutoka nchi mbalimbali kujadili masuala ya uhifadhi, usimamizi na maendeleo endelevu ya maeneo ya urithi wa dunia.

Katika kipindi cha mkutano huo, Tanzania inatarajiwa kuandaa mkutano wa pembeni Julai 27, 2026 utakaowakutanisha wadau mbalimbali kujadili masuala ya uhifadhi, usimamizi na matumizi endelevu ya maeneo ya Urithi wa Dunia, pamoja na kubadilishana uzoefu kuhusu mbinu bora za kulinda urithi huo kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.