Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Waziri Kairuki mguu sawa kuipaisha SITE kimataifa

Muktasari:

  • Kairuki ahitimisha onesho la SITE akiwaita wadau kutoa maoni ya kuliboresha ili lizidi kufikia viwango vya kimataifa na kuwavutia wanunuzi nguli wa bidhaa za utalii.

Dar es Salaam. Onesho la saba la kimataifa la utalii (SITE) lililofanyika jijini Dar es Salaam kwa siku tatu limeitimishwa leo Jumapili Oktoba 8, 2023, wito ukitolewa kwa wadau kutoa maoni yanayolenga kuboresha onesho hilo ili liingizwe kwenye kalenda ya kimataifa ya maonesho ya utalii duniani.

Wito huo umetolewa na Waziri Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki wakati akihitimisha onesho hilo lilofanyika kuanzia Oktoba 6 likihusisha wanunuzi wa bidhaa za utalii kutoka katika Mataifa mbalimbali ulimwengu, waoneshaji na watoa huduma za utalii.

Akizungumza katika halfa ya kuhitimisha onesho hilo Kairuki amesema licha ya mafanikio makubwa yaliyopatikana katika tukio hilo bado kuna fursa ya kutoa maoni ili maboresho zaidi yafanyike kuzidi kulipa hadhi ya kimataifa.

“Tunataka SITE iingie kwenye kalenda za maonesho ya utalii duniani, tayari kuna wadau wa kimataifa wametupongeza kwamba angalau mwaka huu tumepiga hatua sasa tunaendelea kupokea maoni wapi tuboreshe ili kuvifikia viwango hivyo vya kimataifa.

“Lengo hilo likitimia wadau katika sekta ya utalii wataiweka SITE kwenye ratiba zao hivyo idadi ya wahudhuriaji itaongezeka na itazidi kutangaza utalii wa taifa letu, tukiendelea kufanya jitihada za kufikisha idadi ya watalii milioni tano kufikia 2024,”

Kufuatia hilo Waziri Kairuki aliwataka wanaohusika na onesho hilo kuanza mapema maandalizi ya SITE itakayofanyika Oktoba mwakani.

Onesho hili lililofanyika kwa mwaka wa saba linalenga kuwakutanisha wadau wa utalii kutoka ndani na nje ya utalii wakiwemo wafanyabiashara na wanunuzi wa bidhaa za utalii kutoka katika masoko ya kimkakati pamoja na kutangaza fursa za uwekezaji katika sekta hiyo.

Baadhi ya walioshiriki kwenye onesho hilo wameeleza namna lilivyotengeneza fursa ya kukutana na wadau ambao wanahusika kwenye biashara na utangazaji wa bidhaa katika sekta ya utalii na uwekezaji.

Ofisa leseni wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela), Koyan Abubakar amesema taasisi hiyo imetumia onesho hilo kukutana na wateja wa ndani na nje ya nchi na kuwapa elimu kuhusu huduma zinazotolewa kokote duniani kupitia mtandao.

“Hapa tumekuja kukutana na wafanyabiashara na wawekezaji kwenye sekta ya hii ya utalii, lengo ni kuwapa elimu ya kutumia huduma za mtandao zinazotolewa na Brela, wakati mwingine sio lazima mtu afunge safari huduma zetu nyingi zinapatikana kwa mtandao mwekezaji anaweza kufanya hata akiwa nchini kwake,” amesema Abubakar.

Taasisi ya Mifupa (MOI) nayo ilishiriki kwenye onesho hilo kuonesha huduma zinazotolewa katika dhana ya kutangaza utalii wa kimatibabu.

Mkurugenzi wa tiba za upasuaji wa ubongo na uti wa mgongo wa MOI, Dk Lemeli Mchome  amesema ushiriki wa taasisi hiyo ya matibabu katika onesho la utalii unalenga kupanua wigo wa utoaji tiba na kuvuka mipaka ya nchi.

“MOI tumeshafungua tawi la huduma kwa wagonjwa wanaotoka nje ya nchi, hii ni kwa ajili ya kuunga mkono jitihada za Serikali za kuwa na utalii wa kimatibabu. Pamoja na hilo tuna huduma za kibobevu na kwa kuanzia tuna mikono bandia ambayo ni smart.

“Hapa namaanisha kwamba mikono hii ya kisasa inawekwa kwa watu ambao hawana mikono na inaweza kushika kitu, yote hii ni kuhakikisha huduma zetu tunaziweka katika viwango vya kimataifa ndiyo maana tunawakaribisha wagonjwa kutoka mataifa mengine kuja kupata huduma,” amesema Dk Mchome.

Dk Mchome ameweka wazi kuwa pamoja na huduma za kibingwa zinazotolewa na taasisi hiyo upo mpango wa kuendelea kuziongeza na kuzitoa katika viwango vya kimataifa ili kuwavuta wahitaji wengi kutoka nchi jirani.