Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Maliasili kujikita kwa vijana, watoto utalii wa ndani

New Content Item (1)

Muktasari:

  • Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika onesho la saba la kimataifa la utalii (Site) kufanyika kuanzia Oktoba 6, wizara yajipanga kuongeza nguvu kuwatengenezea watoto utamaduni wa kupenda kutalii

Dar es Salaam. Wakati onesho la saba kimataifa la utalii (SITE) likitarajiwa kufanyika nchini kuanzia Oktoba 6 hadi 8 mwaka huu, Wizara ya Maliasili na Utalii imejipanga kutumia onesho hilo na fursa nyingine zilizopo kuhamasisha utalii wa ndani na kutengeneza kizazi cha watalii wa siku zijazo.

Onesho hilo ambalo linatarajiwa kukutanisha wadau wa utalii kutoka mataifa mbalimbali ulimwenguni, litahusisha pia uwepo wa bustani za wanyamapori, na hivyo kutoa fursa kwa watembeleaji kuwaona simba, chui, fisi na wengineo.

Waziri wa Maliasi na Utalii, Angellah Kairuki amesema leo Oktoba 3, 2023; kwamba Serikali inatambua umuhimu wa kuwafanya watoto kupenda utalii na itafanya kila linalowezekana kuhakikisha kundi hilo linajua maana na thamani ya kufanya utalii.

Amesema ili sekta hiyo ikue jitihada mbalimbali zifanyike ili kuwavutia watalii wa ndani na nje ya nchi, na kwamba ni muhimu kuanza kuwajengea watoto na vijana utamaduni wa kuona umuhimu wa kufanya utalii.

“Tunafahamu kundi la vijana na watoto ndiyo kubwa hapa nchini, hivyo ni lazima tuwe na mkakati wa kuhakikisha wanajenga utamaduni wa kufanya utalii, ndiyo maana hata kwenye onesho hili la kimataifa, tuna bustani ya wanyamapori, inawezekana mtu asiingie ndani lakini akaja kutalii pale na kuwaona wanyama,” amesema Kairuki.

Pamoja na hilo amesema Serikali inaendelea kupanua wigo wa kuhamasisha watalii zaidi kuja nchini ikiwemo kuliangalia kwa ukaribu eneo la utalii wa mikutano na tayari ina mpango wa kuongeza kumbi kwa ajili ya mikutano ya kimataifa.

Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Damas Mfugale amesema mkakati huo utahusisha kuanzisha klabu za watoto zitakazojikita kwenye kuhamasisha utalii sambamba na programu maalum za utalii wa ndani katika vyuo vikuu.

Mwenyekiti wa chama cha waongoza utalii, Samwel Diah amesema pamoja na utalii wa ndani kuongezeka ikilinganishwa na ilivyokuwa kabla ya mlipuko wa janga la Uviko 19, bado kuna changamoto ya  Watanzania wengi kuzimudu gharama.

“Utalii wa ndani unakua lakini changamoto tunayokutana nayo wengi hawamudu gharama zile za kulala porini kama ilivyo kwa wageni, katika hili tunashauri kuangaliwa uwezekano wa kutengenezwa vifurushi nafuu,” amesema Diah.

Akizungumzia onesho la SITE ambalo kwa mara ya kwanza lilifanyika mwaka 2014, waziri Kairuki amesema limekuwa jukwaa muhimu linalotoa ushawishi mkubwa kwa wadau walio katika mnyororo wa huduma za utalii kutoka ndani na nje ya nchi.

Amesema kwa mwaka huu onesho hilo litakuwa na ushiriki wa bodi za utalii kutoka za Afrika, mabalozi, waoneshaji zaidi ya 100 kutoka ndani na nje ya Tanzania pamoja na wanunuzi wa biashara za utalii kutoka masoko ya kimkakati ya kimataifa.

Rais Samia Suluhu Hassan ndiye anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye ufunguzi wa onesho hilo lililobebwa na kauli mbiu, ‘Utalii unaowajibika kwa maendeleo jumuishi’.