Waziri Kalemani aagiza mkandarasi akamatwe

Waziri Kalemani aagiza mkandarasi akamatwe

Muktasari:

  • Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani ameagiza kukamatwa kwa mkandarasi ambaye ni kampuni ya Njarita kwa madai ya kushindwa kukamilisha miradi ya umeme wilayani Same kwa wakati.

Same. Waziri wa Nishati, Dk Medard Kaleman ameagiza kusakwa na kukamatwa kwa mkandarasi wa kampuni ya Njarita kwa madai ya kushindwa kukamilisha mradi wa Rea kwa wakati na kutokuwepo eneo la mradi.

Mbali na hilo, Waziri ametoa miezi miwili kwa kampuni tatu za usambazaji wa umeme vijijini kwa Mkoa wa Kilimanjaro, kuhakikisha vijiji vyote vinafikiwa na umeme na kwa kampuni itakayoshindwa mkandarasi akamatwe.


Dk Kalemani alitoa agizo hilo jana Julai 29, 2021 wakati akizindua mradi wa ujazilizi awamu ya pili (2A) katika Kijiji cha Maore, Wilaya ya Same, ambapo amesema Serikali inalipa fedha nyingi kwa ajili ya wananchi kupata huduma.


Kampuni zilizopewa miezi mitatu kukamilisha miradi ya umeme ni Ubarn & Rural Engineering Services, Octopus Engineering na Njarita Contractor huku akiagiza kampuni ya Ubarn, mkandarasi akatwe asilimia 10 kutokana kuchelewesha mradi.


"Kuna kampuni nyingi Kilimanjaro, kampuni ya Njarita haijafikisha umeme kwa miaka sita na ndizo nguzo mnaziona zimesimikwa, hazina waya na wananchi hawajaunganishiwa umeme na leo haiko hapa,"alisema Waziri Kalemani.


"Nataka maelezo kwa nini kampuni ya Njarita haiko hapa, DC (Mkuu wa Wilaya) naomba Njarita asakwe, mpaka apatikane na akipatikana ahojiwe kwa nini hayuko hapa, tunamlipa pesa halafu hayupo hapa, mimi nipo hapa na yeye hayupo, hatuwezi kwenda namna hiyo, awekwe korokoroni,"alisisitiza.


Waziri alisema baada ya miezi miwili, atarudi Wilaya ya Same kufanya ufuatiliaji kuona kama wakandarasi wamemaliza kazi yao na endapo atakuta hawajakamilisha, hatua zitachukuliwa mara moja.


Awali akizungumza mbele ya Waziri, Ofisa Tarafa ya Gonja Wilaya ya Same, Malisa Ibrahim alisema vipo vijiji vitatu ambavyo havijafikiwa na huduma ya umeme huku mkandarasi akiwa amepeleka nguzo na kuziteleleza toka mwaka 2020.