Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Waziri Mabula ataja sababu migogoro ya ardhi Dodoma

New Content Item (1)

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Angeline Mabula

Muktasari:

  • Mkoa wa Dodoma ni miongoni mwa maeneo yanayotajwa kuwa na migogoro mingi ya ardhi, mbali na Kinondoni uliokuwepo awali.

Dar es Salaam. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Angeline Mabula amesema kamati za madiwani za mipango miji ni miongoni mwa sababu ya migogoro ya ardhi katika Mkoa wa Dodoma.

Pamoja na hilo, tamaa ya halmashauri za Jiji hilo kutaka kuonekana zimekusanya fedha nyingi kwa ajili ya shughuli za ardhi ni sababu nyingine.

Mabula ametoa kauli hiyo leo, Jumapili ya Juni 25, 2023 alipotakiwa kueleza mikakati ya wizara hiyo kumaliza migogoro ya ardhi mkoani humo na Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo katika mkutano wa kuhitimisha ziara yake ya siku 10 Dodoma.

“Dodoma hii imeharibika kwa sababu tu ya tamaa ya kutaka kujipatia fedha ziwe nyingi kwamba halmashauri imefanya kazi kubwa kumbe katika kazi hiyo kuna namna ambavyo watu hawakutendewa haki,” amesema.

Sababu nyingine aliyoitaja ni mamlaka za upangaji hasa kamati za mipango miji za madiwani kuwa madalali wa viwanja.

“Hizi kamati zinapaswa kutekeleza wajibu wao na sio kuwa madalali wa viwanja ambao kwa sehemu kubwa wanachangia kuharibu Mji wetu,” amesema.

Hilo, amesema halipo Dodoma pekee bali Mwanza na maeneo mengine.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, uwepo wa watumishi wasio na nidhamu ni sababu nyingine, akisema hushirikiana na wananchi waliokuwa wanavamia maendeo na kuwataka wajenge haraka.


“Tumefukuza watumishi zaidi ya tisa kwa ajili ya kesi za ardhi zilizokuwa zinafanyika na hadi sasa kuna wengine wapo kwenye mashauri ya kiutumishi kutokana na kukiuka taratibu zao,” amesema.

Chanzo kingine cha migogoro katika Jiji hilo, amesema ni wingi wa vibarua kuliko wafanyakazi, ambao ndiyo walioshika miradi ya Dodoma na walichokuwa wanafanya ni kama watu wa kati.

“Mwezi uliopita tumefanya mkutano mkubwa mkoani kote na tulielekeza wote wasimame kazi na waingie kwa utaratibu wa kuingia kwenye mikataba.

“Walikuwa watumishi wa vibarua na walikuwa vigogo kuliko watumishi, unajiuliza mtu kama huyo amefikaje hatua hiyo,” amesema.

Upimaji shirikishi ni change kingine, amesema: “Wengi wamedhulumiwa naomba nikiri hilo na hasa kwenye udanganyifu wakati wa upimaji shirikishi, wanakubaliana mwananchi na halmashauri kwamba mwananchi atachukua asilimia 70 na halmashauri asilimia 70.

“Lakini kiuhalisia upimaji ulipofanyika hilo halikutekelezwa, wananchi wengi wamejikuta wanapata ardhi ndogo kuliko kile walichokusudia,” amesema.

Katika kutatua changamoto hizo, Mabula amesema katika Mkoa huo Serikali imelazimika kuweka makamishna wasaidizi wa ardhi wawili watakaosimamia maeneo mbalimbali.

Ameeleza Kamati iliyoundwa kushughulikia migogoro hiyo tayari imeshatembelea Kata nane ili kuhakikisha inaitambua yote na kujua namna ya kuitatua.

Kupitia mradi wa uboreshaji wa miliki, amesema Dodoma ni miongoni mwa maeneo yatakayonufaika na tayari Kata tatu zinatarajiwa kuanza kama kipaumbele.

Akizungumza katika Mkutano huo, Chongolo amesema badala ya Kinondoni Mkoa wa Dodoma ndiyo unaoongoza kwa migogoro ya ardhi kwa sasa.

Tabia za wananchi, amesema ni miongoni mwa chanzo cha migogoro hiyo na kutaka Wizara ieleze mikakati yake katika kukabiliana na hilo.