Waziri Masauni awatangazia ‘kiama’ wanaomchafua Rais mitandaoni

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni akizungumza na waandishi wa habari hawapo pichani kuhusu mafanikio yaliyofikiwa na Wizara hiyo kwa kipindi cha miaka 60 ya Muungano wa Tanzania.

Dodoma. Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Tanzania, Hamad Masauni amesema Serikali haitakuwa na simile wala mswalie Mtume kwa yeyote atakayebainika anamchafua Rais mitandaoni.

Masauni ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Aprili 15, 2024 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio yaliyopatikana kwenye wizara hiyo, kwa kipindi cha miaka 60 ya Muungano wa Tanzania.

Kauli ya Waziri Masauni ameitoa siku chache tangu Mkuu wa Mkoa wa Arusha (RC), Paul Makonda kuwaonya watu mbalimbali wakiwemo mawaziri wanaowatuma watu kumtukana Rais Samia Suluhu Hassan mitandoni.

Makonda alitoa onyo hilo Aprili 12, 2024, katika ibada maalumu ya kumbukumbu ya miaka 40 ya kifo cha aliyekuwa waziri mkuu, hayati Edward Sokoine, nyumbani kwake Monduli Juu, mkoani Arusha. Rais Samia alikuwa mgeni rasmi.

Leo Jumatatu, Masauni amesema misingi ya Muungano wetu iliyoasisiwa  tangu wakati wa Mwalimu Julius Nyerere ni kujenga Taifa imara, lakini pamoja na mambo mengine lenye maadili kwa kufuata sheria za nchi.

“Kwa hiyo katika misingi hiyohiyo ya kuhakikisha tunaendelea kudumisha maadili na utamaduni, tuendelee kufuata sheria za nchi, hiyo haina simile wala mswalie Mtume,” amesema Masauni.

Amesema kama mtu atavunja sheria hadharani au chumbani kwake na akatuma taarifa kwenye mitandao kwa kufanya vitendo vya kuwachafua watu mitandaoni, lazima hatua zichukuliwe.

Ametoa wito kwa wananchi popote walipo kufuata sheria za nchi kwani hakuna mtu yeyote atakayevunja sheria akabaki salama, kwani Serikali haitamfumbia macho maana haikubaliki.

“Sasa kuna watu wao wanashabikia hawajui pengine na yeye kimetumwa kitu kwenye mtandao anasambaza au anaongezea chumvi na pengine mtu huyo upatikanaji wake ni mwepesi zaidi, msidhani kuna mtu amefanya hivyo hajachukuliwa hatua mkadhani ndiyo basi imepita hiyo itakapofika muda wa kuwatangaza watatangazwa,” amesema Masauni.

“Nasema haya kwa sababu nataka watu wazingatie sheria za nchi na tudumishe misingi ya Muungano wetu ya kujenga Taifa lenye nidhamu, heshima,  maadili na lenye kufuata sheria.”

Amesema sheria ni sheria hivyo kama unachokifanya kwenye mitandao ni kinyume cha sheria ya makosa ya mitandaoni au iwe sheria yoyote ni lazima hatua zichukuliwe, kwa kuwa hakuna aliye juu ya sheria na kwa kutokujua sheria hakuhalalishi mtu kuivunja.

Akizungumzia suala la Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), Masauni amesema mpaka sasa imefanikiwa kusajili watu 24,495,804 na kutoa namba za utambulisho kwa watu 20,832,225 na kuzalisha vitambulisho 20,286,420 lengo likiwa ni kumaliza malalamiko ya wananchi na jambo hilo kubakia historia.

Amesema mafanikio mengine ni kuondolewa kwa sharti la viza rejea kwa raia wa Ethiopia uamuzi uliopunguza wimbi la raia wa nchi hiyo waliokuwa wakisafirishwa kimagendo kupitia Tanzania kwenda nchi nyingine Kusini mwa Afrika.

Amesema uamuzi huo umepunguza gharama za kuwalisha wafungwa wa kigeni magerezani na  kupunguza mlundikano wa mahabusu.