Waziri Mchengerwa atoa maagizo wanyama waliovamia makazi ya watu waondolewe

Askari wa jeshi la Uhifadhi misitu na wanyamapori waliohitimu mafunzo kituo cha Mlele wakionesha gwaride kwa mgeni rasmi Waziri wa Maliasili na Utalii Mohamed Mchengerwa. Picha na Mary Clemence
Muktasari:
- Waziri Mchengerwa aagiza taasisi za hifadhi za wanyamapori na misitu kushirikiana na askari 231 waliohitimu mafunzo ya Jeshi Usu Kituo cha Mlele kuwaondoa wanyama wakali wanaosababisha taharuki kwa wananchi.
Katavi. Waziri wa Maliasili na Utalii Mohamed Mchengerwa ameziagiza taasisi za serikali hifadhi za wanyamapori na misitu kuwatumia askari 231 waliohitimu mafunzo ya Jeshi la Uhifadhi Kituo cha Mlele, kuwatoa wanyama wakali wanaovamia maeneo ya wananchi na kusababisha taharuki kubwa.
Waziri Mchengerwa ametoa agizo hilo Aprili 26, 2023 katika hafla ya ufungaji mafunzo hayo iliyofanyika katika kituo hicho cha mafunzo Mlele kwa askari wa Hifadhi ya Ngorongoro na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS).
Amesema wanyama hao wakali na waharibifu wa mali za wananchi wanasababisha malalamiko, masononeko, majeraha na wakati mwingine vifo miongoni mwao hususani wanaoishi karibu na maeneo ya hifadhi.
“Kwa msingi ule ule kama tunavyowahimiza wananchi kuondoka kwenye maeneo ya hifadhi na sisi kama wizara tunapaswa kutimiza wajibu,”amesema.
“Nakuelekeza Katibu Mkuu kuhakikisha wanyama hao wanaondoshwa na kurejeshwa maeneo yao ya hifadhi, hivyo watumieni askari hawa kabla hawajakwenda sehemu zao za kazi walizopangiwa,”amesema Mchengerwa.
Mbali na hilo amewataka wahitimu wa mafunzo hayo kufanya kazi kwa weledi na kuwa wabunifu, kutoa elimu stahiki kwa wananchi kuhusu umhimu wa kutunza rasilimali za wanyama na misitu.
“Nendeni mkafanye kazi kwa kushirikiana na wengine mtakaowakuta ili kuhakikisha changamoto zote zilizozungumzwa nanyi pamoja na makamishna zinamalizika.
Awali kisoma risala ya wahitimu Mwita Msama amesema lengo la mafunzo hayo ni kuandaa askari wakakamavu watakaolinda na kuimarisha uhifadhi wa wanyamapori na misitu, kupambana na majingili na biashara haramu ya nyara na mazao ya misitu.
“Mafunzo yalianza Novemba 01,2022 na kufungwa April 26,2023 yakiwa na askari 46 kutoka NCAA na 185 TFS kati yao wanafunzi wa kiume 165 na wa kike 66, hakuna mwanafunzi aliyefukuzwa au kusimamishwa kwa utovu wa nidhamu,” amesema Msama.
Mkuu wa mafunzo hayo Kanali Fred Lukilana amesema wanafunzi hao wamejifunza masomo tofauti kwa nadharia na vitendo ikiwemo utimamu wa mwili na nidhamu ya kijeshi.
“Uchunguzi wa makosa ya jinai, ramani na matumizi ya GPS, elimu ya afya na huduma ya kwanza, kwata tofauti, silaha na matumizi yake,usalama wa habari, mawasiliano ya redio na doria na mengineyo,”amesema Lukilana.