Waziri Mkenda aeleza nzige wanavyodhibitiwa

Muktasari:

  • Waziri wa Kilimo nchini Tanzania, Profesa Adolf Mkenda amesema nzige wa jangwani walioingia wilayani Siha mkoani Kilimanjaro wakitokea Longido wamedhibitiwa.


Moshi. Waziri wa Kilimo nchini Tanzania, Profesa Adolf Mkenda amesema nzige wa jangwani walioingia wilayani Siha mkoani Kilimanjaro wakitokea Longido wamedhibitiwa.

Profesa Mkenda amesema nzige hao ambao wapo kwa makundi walitokea nchi jirani ya Kenya  walianza kuingia Wilaya ya Mwanga na baadaye kusambaa katika Wilaya  za Same na Siha.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Ijumaa Februari 26, 2021,  Profesa Mkenda amesema ndani ya siku mbili nzige hao watakuwa wameshaangamizwa wote na wizara itatoa taarifa rasmi.

"Leo niko Siha na nzige wengi sana wamekufa  ndani ya siku mbili tutatoa taarifa rasmi ya kwamba  tumewaangamiza nzige hawa.”

"Sasa hivi hali sio mbaya kuna kundi moja la kumalizia, hili ambalo limekimbilia msitu wa Kinapa kwa spidi tunayokwenda nayo tutalimaliza haraka sana na tumejipanga vizuri endapo likiingia kundi jingine likitokea nchi jirani tutalishambulia kwa haraka sana," amesema Profesa Mkenda