Waziri Mkenda: Vyuo vikuu andaeni walimu elimu amali

Waziri wa Elimu Profesa Adolf Mkenda akizungumza na wenyeviti na wajumbe wa bodi wa mabaraza ya vyuo vikuu na maseneti leo Juni 2, 2023

Muktasari:

  • Profesa Mkenda avitaka vyuo vikuu kukaa mguu sawa kuandaa walimu watakaofundisha mkondo wa amali, akieleza kuwa zitatolewa ajira nyingi katika kada hiyo ili kulisha shule zinazotoa elimu ya amali.

Dar es Salaam. Wakati sera mpya ya elimu ikitarajiwa kuanza utekelezaji wake mwakani, Waziri wa Elimu Profesa Adolf Mkenda amevitaka vyuo vikuu kukaa mguu sawa kuwaandaa walimu watakaokwenda kufundisha katika shule za amali.

Amesema ili lengo la kuwa na mkondo wa amali liweze kutimia ni lazima shule hizo ziwe na walimu waliobobea katika fani mbalimbali za mafunzo ya ufundi na fani nyingine zilizoainishwa kwenye mkondo huo.

Profesa Mkenda ametoa maelekezo hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na wenyeviti na wajumbe wa bodi wa mabaraza ya vyuo vikuu na maseneti.

Amesema hadi sasa ni vyuo vichache vinavyotoa shahada ya ualimu katika fani za ufundi hivyo ni muhimu kwa vyuo kuwa tayari kutengeneza kada hiyo ambayo itategemewa zaidi katika utekelezaji wa sera mpya ya elimu inayohusisha mkondo wa amali.

“Tunataka vyuo vikuu viandae walimu kwa ajili ya kufundisha shule zote katika mkondo huu wa elimu ya amali, tunataka kunyanyua hizi shule zetu za ufundi hivyo ni lazima tuwe na walimu ambao wamesomea fani zitakazowawezesha kutoa mafunzo ya amali,”amesema Profesa Mkenda.

Waziri Mkenda ametaka pia kampasi mpya za vyuo zinazoanzishwa kupitia wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya kiuchumi (HEET) kujikita katika kutoa shahada za zilizojikita katika fani mbalimbali za mafunzo ya  amali.

Akizungumza katika mkutano huo Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas) Dk Harrison Mwakyembe ameomba Serikali kurudisha hospitali ya Mloganzila chini ya chuo hicho ili itumike kwa mafunzo.

“Najua hili suala halipo kwako ila unaweza kusaidia ile hospitali ni kazi ya Muhas na iliihitaji kwa ajili ya mafunzo, tulitaka kuwa na hospitali ya mafunzo lakini tumeona imewekwa chini ya Muhimbili. Nimeshaandika barua kwa mamlaka naomba usaidie kulifikisha hili tunahitaji hospitali ya Mloganzila kwa ajili ya mafunzo,” amesema Mwakyembe.