Waziri Mkuu apokea kero 305 Mbulu, aagiza mfumo wa uwajibikaji kila mwezi
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Mwigulu Nchemba
Muktasari:
- Aagiza mfumo wa kila mwezi wa kuripoti na kufuatilia utatuzi wake, asisitiza uwajibikaji kwa viongozi wote.
Mbulu. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, amepokea jumla ya kero na hoja 305 kutoka kwa wananchi wa Wilaya ya Mbulu, akiahidi kuanzisha utaratibu madhubuti wa kuzishughulikia kwa wakati na kwa uwajibikaji unaopimika.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Mpira wa Mbulu Mjini jioni ya Jumatatu, Machi 2, 2026, ikiwa ni hitimisho la ziara yake ya siku tatu mkoani Manyara, Waziri Mkuu amesema Serikali haitavumilia utamaduni wa kurundika malalamiko bila kuyapatia ufumbuzi.
“Kila kiongozi aliyeko ofisini anapaswa kushughulikia mambo ya wananchi. Ninaandaa utaratibu wa kila mwisho wa mwezi, kuanzia kijiji hadi mkoa, kutolewa taarifa ya kero zilizotatuliwa na zilizobaki pamoja na sababu zake. Tutafuatilia utekelezaji wake,” amesema.
Amefafanua kuwa mfumo huo hautakuwa wa ziara pekee, bali wa kudumu, akisisitiza matumizi ya vitabu vya wageni katika ofisi za umma ili wananchi waandike hoja zao rasmi kwa ajili ya ufuatiliaji.
“Hatukuanzisha ofisi za umma kwa ajili ya kugawana madaraka, bali kutatua matatizo ya wananchi. Kupuuza shida zao siyo lengo la Serikali,” ameongeza.
Akagua mradi wa barabara
Akiwa njiani kuelekea Mbulu, Dk Nchemba amekagua ujenzi wa kipande cha barabara ya kilomita 25 kutoka Mbulu hadi Garbabi, sehemu ya barabara kuu ya kiwango cha lami ya kilomita 389 inayounganisha Karatu–Mbulu–Haydom–Sibiti River–Lalago–Maswa.
Kwa mujibu wa taarifa ya mradi huo unaotekelezwa na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), ujenzi umefikia asilimia 41.7, huku gharama za kukamilisha zikikadiriwa kufikia Sh36.3 bilioni. Hadi sasa, Sh12.5 bilioni zimelipwa.
Mradi huo unatarajiwa kuboresha usafirishaji wa watu na bidhaa, kupunguza gharama za usafiri na kuchochea shughuli za kiuchumi katika ukanda huo wa Kanda ya Kaskazini na Ziwa.
Manyara yashika nafasi ya pili kitaifa
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga, amesema mkoa huo umeandika historia kwa kushika nafasi ya pili kitaifa katika matokeo ya kidato cha nne mwaka jana.
Amesema mafanikio hayo yanatokana na uwekezaji wa Serikali, hususan katika ujenzi wa shule za msingi na sekondari, madarasa na mabweni ili kupunguza umbali kwa wanafunzi, hasa kutoka jamii za wafugaji.
“Hii siyo bahati mbaya. Ni matokeo ya uwekezaji wa kimkakati katika elimu,” amesema.
Ziara ya Waziri Mkuu mkoani Manyara imelenga kukagua miradi ya maendeleo na kusikiliza kero za wananchi, huku akisisitiza kuwa kipimo cha uongozi bora ni uwezo wa kutatua changamoto za wananchi kwa wakati.