Waziri Mkuu ataka Mkoa wa Mara uwe kitovu cha utalii

Muktasari:

  • Waziri Mkuu ameuagiza uongozi wa Mkoa wa Mara kuanza kampeni maalumu ya uwekezaji ili kuufanya mkoa huo kuwa kitovu cha utalii nchini.

Musoma. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameutaka uongozi wa Mkoa wa Mara kuanza mara moja kampeni ya kuufanya mkoa huo kuwa kitovu cha utalii, kufuatia uwepo wa mradi wa maboresho na upanuzi wa uwanja wa ndege wa Musoma.Pia ameuagiza uongozi wa mkoa huo kuandaa mazingira rafiki kwa ajili ya uwekezaji hasa wa sekta za hoteli zenye hadhi ya kitalii, ili kuwa sehemu ya kivutio cha watalii kutoka ndani na nje ya nchi.Majaliwa ametoa maagizo hayo leo Februari 29, 2024 mjini Musoma baada ya kufanya ukaguzi wa maendeleo ya mradi wa ujenzi na maboresho ya uwanja wa ndege Musoma."Tutakuwa watu wa ajabu kama tutakaa kimya bila kuwa na mipango mikakati tena imara ya kuufanya mkoa huu kuwa kitovu cha utalii, tuna kila sababu na vigezo vya kufanya hivyo," amesema.Amesema hifadhi ya Taifa ya Serengeti ambayo kwa asilimia kubwa ipo mkoani Mara imekuwa bora duniani kwa zaidi ya miaka mitatu mfululizo, hivyo ni vema hali  hiyo ikatumika kwa ajili ya kuboresha sekta ya utalii na uchumi wa wakazi wa mkoa huo  na Taifa kwa ujumla."Msisubiri eti hadi uwanja ukamilike ndipo muanze mikakati, anzeni sasa wakati unajengwa ukikamilika na nyie mnakuwa mmekamilisha na hii sio kwa faida ya Taifa pekee bali ni kwa wakazi wa mkoa pia," ameagiza.Amesema uwanja wa ndege wa Musoma mbali na kuwa ni sehemu ya kumuenzi baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere lakini pia ni kichocheo cha utalii kutokana na ukweli kuwa ni rahisi zaidi kwa mtu kupitia uwanja huo kwenda katika hifadhi ya Serengeti tofauti na kutokea maeneo mengine.Majaliwa pia ameutaka uongozi wa mkoa kufanya mazungumzo na mmiliki wa sasa wa hoteli ya Musoma juu ya uwezo wake wa kuendesha hoteli hiyo kufuatia kushindwa kufanya kazi kwa muda mrefu sasa."Tulikuwa na hoteli hapa ilileta sifa sana lakini hivi sasa haipo tena pamevurugika. Huyo anayemiliki aulizwe kama anaweza kupatumia kama hawezi tumieni nafasi hiyo tangazieni wanaoweza waje waturudishie ile hoteli, ule ufukwe ndio unaoleta heshima," amesema.Amewataka watu wenye uwezo wa kujenga hoteli kuanzia nyota nne na kuendelea kufika mkoani humo kwa ajili ya uwekezaji huo.Awali akitoa taarifa ya uwanja huo, Meneja wa Wakala wa Barabara Nchini (Tanroads) Mkoa wa Kara, Vedastus Maribe amesema ujenzi wa uwanja huo unatarajiwa kugharimu zaidi ya Sh35 bilioni na ulianza Aprili 2020."Mradi umefika asilimia 55 na unatarajiwa kukamilika Desemba 2024 baada ya kushindwa kukamilika Desemba 2023 kutokana na changamoto mbalimbali," amesema Maribe.Maribe amesema ujenzi na ukarabati wa uwanja huo unahusisha kuongeza urefu wa njia za kuruka na kutua ndege kutoka kilomita 1.6 hadi 1.75, ujenzi wa maegesho ya ndege, barabara za kuingia na kutoka, jengo la zimamoto, njia ya ulinzi, uzio, jengo la umeme na miundombinu mingine.